loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Buriani Mzee Mkapa, wadau wa Kiswahili tutakukumbuka daima

MAKALA haya yanaandikwa katika juma ambalo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iko katika majonzi makubwa ya kumpoteza Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.

Mzee Mkapa alifariki dunia jijini Dar es Salaam, usiku wa kuamkia tarehe 24/7/2020. Kwa mujibu wa maelezo ya familia, Mzee Mkapa alifariki dunia kutokana na mshituko wa moyo.

Wakati naandika makala haya, mwili wa Benjamin Mkapa ulikuwa ukiagwa katika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam kwa siku tatu, kuanzia tarehe 26-28/7/2020, kabla ya kusafirishwa kwenda kijijini kwake Lupaso, Wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara ambako alizikwa juzi, Jumatano 29/7/2020.

Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) linatoa pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Magufuli, mjane Mama Anna Mkapa pamoja na wanafamilia, Watanzania wote na watu wote barani Afrika na duniani kote walioguswa na msiba huu. Mkapa alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa vipindi viwili vya miaka mitanomitano.

Aliingia madarakani katika uchaguzi wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi mwaka 1995. Mzee Mkapa alichaguliwa tena katika uchaguzi wa mwaka 2000 na kuhitimisha kipindi chake cha uongozi mwaka 2005.

Mambo mengi yenye mafanikio yalifanyika katika kipindi chake cha uongozi. Baadhi ya mambo hayo ni mageuzi katika uchumi, ukusanyaji mzuri wa kodi, ujenzi wa miundombinu, udhibiti wa mfumuko wa bei, mapambano dhidi ya rushwa, hatua thabiti za ustawi wa watumishi wa umma na wasio watumishi wa umma, ufutaji kodi na ada mbalimbali, kuendelea kuimarisha Muungano, kudumisha amani na utulivu, usawa wa kijinsia, kukua kwa sekta za michezo na sanaa, elimu bora n.k. Makundi ya wananchi walio katika sekta mbalimbali yameeleza namna walivyonufaika na uongozi thabiti wa Mkapa katika sekta zao.

Nasi, wadau wa Kiswahili tungependa kuungana na wenzetu katika kuelezea namna ambavyo lugha ya taifa ilifaidika na uongozi wa Mheshimiwa Mkapa. Tutakuwa wachoyo wa fadhila kama tukikaa kimya ilihali Mzee Mkapa alifanya mambo mengi ya kukiendeleza Kiswahili. Mchango wake katika Kiswahili ulikuwa na manufaa makubwa na ndiyo msingi wa sura tunayoiona sasa katika maendeleo ya lugha ya Kiswahili kitaifa na kimataifa.

Rais huyo wa awamu ya tatu ya uongozi wa nchi yetu, licha ya kubobea katika lugha ya Kiingereza kutokana na historia ya elimu yake, bado aliipa thamani kubwa lugha ya Kiswahili katika shughuli zake. Kabla ya kuingia madarakani, alifanya kampeni zake kwa kutumia Kiswahili fasaha na sanifu akizunguka nchi nzima ya Tanzania. Miaka miwili baada ya kuingia madarakani, mwaka 1997, alikutana na wadau wa Kiswahili kuzungumzia maendeleo ya lugha ya Kiswahili kwa ujumla.

Kikao hicho kilichofanyika ikulu chini ya uratibu wa BAKITA kiliwahusisha wadau kama vile Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI), sasa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chama cha Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania (UKUTA) n.k.

Majadiliano yaliyofanyika katika kikao hicho yalikuwa na manufaa makubwa katika maendeleo ya lugha ya Kiswahili. Miongoni mwa manufaa hayo ilikuwa ni kauli yake ya kuzitaka asasi za Kiswahili kuendesha mijadala ya kitaifa kuhusu Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia katika ngazi zote za elimu.

Kama ilivyo kaulimbiu yake ya ‘Ukweli na Uwazi’ alitaka suala hili lijadiliwe na umma wa Watanzania kupitia majadiliano ya wazi ambayo msingi wake uwe nguvu ya hoja. Katika kuitikia mwito huo BAKITA na wadau wengine wa Kiswahili waliandaa mijadala, makongamano na mikutano mbalimbali iliyojadili kuhusu Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia katika ngazi zote za elimu.

Maoni yaliyotolewa na yanayoendelea kutolewa na wananchi yamekuwa yakikusanywa na BAKITA ili kuwa ithibati ya msimamo wa wananchi kuhusu Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia katika ngazi zote za elimu nchini.

Mwaka 1997 Sera ya Utamaduni ilizinduliwa rasmi ambapo kuhusu lugha ya Kiswahili Sera hiyo ilitamka kwamba, ‘Kiswahili kitatamkwa rasmi kuwa Lugha ya Taifa na kauli hii itazingatiwa katika Katiba ya Nchi’.

Aidha, katika sera hiyo inaelezwa kwamba, ‘Baraza la Kiswahili la Taifa litakuwa na jukumu la kutafiti, kuneemesha na kuendeleza matumizi ya lugha ya Kiswahili. Baraza la Kiswahili la Taifa na taasisi nyingine za ukuzaji wa Kiswahili zitaimarishwa na kupatiwa nyenzo na fursa ya kutekeleza majukumu yake kikamilifu. Lugha za asili zitaendelea kutumika kama hazina na chanzo cha kukuza Kiswahili’.

Vilevile, Sera hiyo ya Utamaduni inafafanua kwamba, ‘Jitihada za serikali yoyote ile ya kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa kwa kutumia Mfumo Rasmi wa Elimu ambao hautumii lugha ya Taifa kama lugha ya kufundishia zinasababisha siyo tu uharibifu wa urithi wa utamaduni wa nchi, bali pia zinachangia katika kuleta na kuendeleza umaskini na mtafaruku katika jamii’.

Inaendelea kueleza kuwa, ‘Kama tutaendelea kufundisha kwa lugha ya Kiingereza sayansi na teknolojia ambayo tunaihitaji sana kwa maendeleo ya taifa letu katika karne ya ishirini na moja itaendelea kuwa haki ya watu wachache wanaofahamu Kiingereza’.

Kwa kuzingatia hayo yote sera hiyo, inatamka kwamba, ‘Mpango maalunu wa kuiwezesha elimu na mafunzo katika ngazi zote kutolewa katika lugha ya Kiswahili utaandaliwa na kutekelezwa’.

Aidha, ili kujiandaa na hatua hiyo muhimu kwa taifa, Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) mwaka 1999 ilichapisha kitabu kinachoitwa Kiswahili katika Elimu, katika kitabu hicho wataalamu waliliangalia suala la lugha ya kufundishia kwa upana na kusisitiza hatua ya Sera ya Elimu ya kutumia Kiswahili katika elimu ya ngazi zote.

Kitabu hiki ni mkusanyiko wa mawazo ya watafiti kuhusiana na matumizi ya lugha ya awali katika utoaji na upokeaji wa elimu. Makala yaliyomo katika kitabu hiki yanazungumzia faida ya kutumia Kiswahili katika kufundishia elimu ya juu Tanzania, hasa kutokana na ukweli kwamba ndiyo lugha iliyoenea kuliko lugha nyingine Tanzania.

Fauka ya hayo, hatua zaidi ziliendelea kupigwa katika kipindi hicho cha utawala wa Mkapa kwa asasi za Kiswahili kutafsiri vitabu vya masomo ya elimu ya sekondari na pia kuandaa vitabu vya kiada katika shule hizo.

Vitabu vyote hivyo vilitafsiriwa kutoka katika lugha nyingine hasa Kiingereza kwenda katika Kiswahili na kuandika vile vya kiada kwa lugha ya Kiswahili. Mwaka 2005 Baraza la Kiswahili la Taifa lilichapisha kitabu cha Istilahi za Kiswahili.

Lengo la kitabu hiki lilikuwa ni kuendelea kuongeza msamiati zaidi utakaowezesha Kiswahili kutumika kama lugha ya kufundishia katika ngazi zote za elimu na kutumiwa kiufasaha katika nyanja nyingine za maisha katika jamii yetu.

Miongoni mwa istilahi zilizo katika kitabu hiki ni zile za: Baolojia, Kemia, Fizikia, Hisabati, Jiografia, Historia, Biashara na Uchumi, Uzazi wa Mpango, Magonjwa ya Mimea, Wanyama na Wadudu Waharibifu, Saikolojia, Agronomia na Ufugaji, Saikatria, Tathmini katika Elimu, Lugha, Ufundi Magari, Uhandisi Kilimo n.k.

BAKITA na wadau wengine wa Kiswahili wanaamini kwamba hatima ya agizo hili la Mzee Mkapa itafikiwa kwa wananchi kuunga mkono hoja hii kutokana na ushahidi mwingi unaotokana na tafiti kuonesha kwamba ni vigumu kuendelea na kuibua ubunifu kwa wanafunzi kwa kutumia lugha ambayo hawaielewi vema na isiyo yao.

Ni matumaini ya wadau wa Kiswahili kuwa jitihada hizi zilizoanzishwa wakati wa Awamu ya Tatu ya uongozi wa nchi yetu ndizo zilizosababisha tamko katika Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 kwamba, ‘Lugha ya Taifa ya Kiswahili itatumika kufundishia na kujifunzia katika ngazi zote za elimu na Serikali itaweka utaratibu wa kuwezesha matumizi ya lugha hii kuwa endelevu na yenye ufanisi katika kuwapatia walengwa elimu na mafunzo yenye tija kitaifa na kimataifa’. Asasi za Kiswahili zitaendelea na jitihada za kuhakikisha kwamba utekelezaji wa tamko hili unazingatiwa.

Mafanikio mengine katika lugha ya Kiswahili chini ya utawala wa Mkapa yalikuwa ni yale ya mwaka 2004, Kiswahili kilipoingia katika Umoja wa Afrika na Bunge la Afrika.

BAKITA kwa kushirikiana na asasi nyingine za Kiswahili zilitoa Tuzo kwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa wakati huo Jakaya Kikwete. Mheshimiwa Kikwete alitunukiwa Tuzo ya Heshima kwa juhudi zake za kukitetea Kiswahili mpaka kufanikisha kuingia katika Umoja wa Afrika.

Aidha, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ilipewa Ngao kwa kutoa ushirikiano kwa juhudi hizo. Tuzo na ngao hiyo vilitolewa katika Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili yaliyofanyika katika ukumbi wa Arnatoglou, jijini Dar es Salaam tarehe 10 Februari, 2005.

Aidha, Mei 2005, aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera), William Lukuvi aliagiza taarifa za mikutano, semina na warsha nchini zitolewe kwa Kiswahili kwa manufaa ya wananchi. Pia, taarifa za miradi inayohusu wananchi ni lazima zitolewe kwa lugha ya Kiswahili, ikiwa ni pamoja na vipeperushi na nyaraka zinazohusu miradi. Jitihada zote hizi zilikisaidia Kiswahili kupiga hatua chini ya Rais Mkapa.

Mzee Benjamin William Mkapa ameutumia sana msemo maarufu wa ‘Mtaji wa Maskini ni Nguvu zake Mwenyewe’. Msemo unaowahamasisha watu kufanya kazi kwa bidii kwa kutumia nguvu zao badala ya kutegemea misaada kutoka kwa watu wengine. Athari ya kutegemea misaada ni kubwa kwani mtu ana hiari ya kukupa au kutokupa msaada huo.

Kwa kutumia msemo huu wananchi walihamasika kufanya kazi kwa bidii ili waweze kuendesha maisha yao. Vilevile, chini ya utawala wake programu mbalimbali hususani katika elimu zilianzishwa. Programu hizi zilipewa finyazo mbalimbali za Kiswahili kama vile, MKUKUTA - Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini, MMEM - Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi, MEMS - Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari, MEMKWA - Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Watoto Waliokosa, MKURABITA - Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania na nyingine nyingi.

Finyazo hizi za Kiswahili zilisaidia programu hizi kueleweka na kutekelezwa kwa urahisi. Kuhusu kitabu chake cha My Life, My Purpose, Mkapa alipokuwa anazungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bwiru iliyoko jijini Mwanza, alikiri kwamba yeye si mjuzi wa lugha ya Kiswahili, pamoja na kuwa wengi tumeshuhudia mambo mengi mazuri aliyoyafanya kuhusiana na Kiswahili. Hata hivyo, aliwaahidi wanafunzi hao kwamba jitihada za kukitafsiri kwa Kiswahili kitabu hicho zinafanywa na mchapishaji wake.

Aidha, katika mazungumzo hayo, alisema kuwa amevutiwa na mswada unaohusu maisha ya Rais wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi ulioandikwa kwa lugha ya Kiswahili, alimsifu Mzee Mwinyi kwa ujuzi wake wa lugha ya Kiswahili.

Mkapa aliamini na kuthamini utaalamu wa wengine wenye weledi na waliobobea katika Kiswahili, na hili linadhihirika pale hotuba zake za kila mwezi zilipokusanywa na kuletwa BAKITA ambapo zilihaririwa lugha na kupewa ithibati ya lugha na BAKITA kabla ya miswada hiyo ya mfululizo wa Ukweli na Uwazi kuchapwa na kuwa vitabu.

Vitabu hivi vitakuwa mchango wake katika Kiswahili utakaodumu kwa miongo mingi hapa duniani. Siyo rahisi kuyamaliza yote yaliyofanywa na Mkapa katika uga wa lugha ya Kiswahili kwani ni mengi mno.

Sisi wadau wa Kiswahili tunaahidi kuyaendeleza yote yaliyoasisiwa na kukubalika katika kipindi chake kama njia mojawapo ya kumuezi. Tuhitimishe kwa kumtakia mzee wetu pumziko la milele. Bwana ametoa Bwana ametwaa Jina lake lihimidiwe, Amin.

Mwandishi wa makala haya ni mhariri Mkuu, Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA).

OKTOBA 28, 2020 Tanzania itafanya Uchaguzi Mkuu kuchagua rais, wabunge ...

foto
Mwandishi: Richard Mtambi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi