loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mkapa: Bado sioni ubora wa upinzani

HII ni hotuba ya Rais wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, Benjamim Mkapa aliyoitoa Desemba 31, 2004, ikiwa ni salamu za mwaka mpya wa 2005 ambao ulikuwa ni mwaka wa uchaguzi ulioshuhudia Jakaya Kikwete akichaguliwa kuongoza Tanzania.

Ndugu Wananchi, Leo tena tunaungana na wanadamu wenzetu duniani kuhitimisha mwaka wa 2004, na kuukaribisha kwa furaha mwaka wa 2005. Naomba kila mmoja kwa imani yake, tumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuifikia siku hii ya leo.

Baadhi ya wenzetu wameitwa naye katika mwaka huu unaoisha. Tuungane kuwaombea ili Mwenyezi Mungu aziweke roho zao mahali pema peponi. Binafsi ninazo sababu nyingi za kumshukuru Mwenyezi Mungu, ikiwemo kwa kusikia dua zenu na zangu kwa ajili ya afya yangu, na kwa ajili ya amani na umoja wa Watanzania. Najua wapo Watanzania wengi ambao kila mara wanamwomba Mwenyezi Mungu, mchana na usiku, kwa ajili yangu na kwa ajili ya nchi yetu.

Itaendelea Jumatatu

Ninawashukuru sana wote hao. Ninaomba waendelee pamoja nami kumwomba na kumshukuru Mwenyezi Mungu ili azidi kutusikia maombi yetu na kutujalia yote yaliyo mema na ya heri. HALI YA KISIASA Ndugu Wananchi: Tumekuwa na mfumo wa kisiasa wa vyama vingi kwa miaka 12 sasa.

Ungetazamia kuwa baada ya muda huo ushindani wa kisiasa ungeboreka, ukawa ushindani wa kiungwana na wa hoja; ushindani unaoboresha mfumo wenyewe kwa maslahi ya taifa; ushindani unaotoa kipaumbele kwa maendeleo ya wananchi na taifa.

Nionavyo mimi, ongezeko lililopo hasa ni la idadi ya vyama vya siasa na idadi ya waheshimiwa wanaoongoza vyama hivyo; na si ongezeko la ubora wa ushindani. Kwa wastani, kinazaliwa chama kipya cha siasa kila mwaka. Faida yake kwenu wananchi siijui. Leo, nina uhakika ukiwauliza Watanzania wataje majina ya vyama vyote vya siasa na viongozi wake wakuu, wengi hawataweza kutaja zaidi ya nusu.

Tujiulize Watanzania. Utitiri huu wa vyama unaboresha au unadhoofisha hali ya kisiasa nchini? Vyama vipya, lakini hakuna jipya! Ninapokaribia kumaliza kipindi changu cha uongozi wa taifa, nadhani huu ni wakati mzuri kuangalia upya namna ya kuimarisha mageuzi ya kisiasa ili yalete manufaa mengi zaidi kwa wananchi na taifa, na hasa ili yasiwe mbegu ya kuwagawa Watanzania na kudhoofisha umoja wao.

Wapo wanasiasa wa vyama mbalimbali, na waandishi wa habari na makala, ambao hawaishi kulinganisha Awamu ya Kwanza ya uongozi wa taifa letu, na awamu zilizofuata. Kwa hakika, Baba wa Taifa anastahili sifa zote anazopewa.

Hapana shaka kuwa mfumo wake wa utawala, mfumo wa chama kimoja, ulisaidia sana kuweka misingi ya umoja wa taifa, na kuelekeza nguvu za viongozi wa kisiasa kwenye mambo ya msingi ya utawala na maendeleo. Mimi siamini kuwa wingi wa idadi ya vyama una uhusiano wa moja kwa moja na ubora wa mfumo wa kisiasa, au ubora wa utawala katika mazingira yetu na hatua yetu ya maendeleo.

Na tusipoangalia, kila itokeapo migogoro ndani ya vyama, na mara nyingi migogoro hiyo haihusiani hata kidogo na maslahi ya chama wala taifa, vyama vitameguka na kuzaa vyama vingine.

Nasema, vyama vingi, sawa; wala sina nia ya kuvizuia; lakini kama wananchi tujiulize, tutaacha lini kuanzisha vyama ili tuimarishe vyama? Kwa maoni yangu: Kwanza, tunahitaji vyama vichache makini vitakavyojishughulisha kwa dhati na masuala muhimu ya taifa, masuala yenye umuhimu kwa wananchi, badala ya masuala ya kibinafsi. Hivi sasa ukisoma au kusikia habari za kisiasa unaona wazi kuwa sehemu kubwa ya siasa nchini ni siasa za kibinafsi, kwa maslahi binafsi.

Utaona pia watu wanabishana juu ya mambo mengine madogo, au hata ya kipuuzi kabisa. Lakini ubishi huo ndiyo unaitwa ushindani wa kisiasa, unaochangamkiwa pia na vyombo vya habari.

Pili, tunahitaji kuwa na vigezo vya demokrasia, na vigezo vya uwazi na uwajibikaji, ndani ya kila chama cha siasa. Umuhimu wa sifa hizo, na vigezo hivyo, si kwa chama tawala tu, ni kwa vyama vyote vya siasa.

Tatu, tunahitaji kuwa na kanuni za tabia, na maadili ya kisiasa, kuongoza shughuli za kisiasa za vyama vyote, na hasa kanuni na maadili wakati wa uchaguzi. Ndugu Wananchi: Nasema haya kwa vile hatukuanzisha mfumo wa siasa wa vyama vingi ili watu wetu wachukiane, watishane kwa kunoa mapanga, waumizane, wauane au waharibiane mali zao.

Hatukuanzisha mfumo wa siasa wa vyama vingi ili kudhoofisha utaifa wetu, umoja wetu na mshikamano wetu. Taifa hili na Katiba yake, kwa asili yake, linaheshimu haki za binadamu, ikiwemo haki ya kuishi.

Sasa inakuwaje tunafika mahali uchaguzi wa vitongoji na mitaa unasababisha vifo? Aibu gani hii? Fujo zinazotupelekea huko, chanzo chake ni nini? Wapo waliodiriki kugeuza vifo hivyo vya kusikitisha kuwa mtaji wa kisiasa.

Hiyo nayo ni aibu, na wala si hulka ya Watanzania. Na wala si busara kulaumu tulipoangukia, badala ya kulaumu tulipojikwaa. Swali la msingi ni hili –ilikuwaje na ilianzaje mpaka ikabidi kutumika nguvu ya kudhibiti hali iliyosababisha kifo? Ndugu Wananchi: Taifa hili na Katiba yake, kwa asili yake, linatoa haki sawa za uraia kwa wananchi wote, ikiwemo haki ya kuchagua au kuchaguliwa kiongozi.

Lakini mwaka huu tumeona tabia mpya ya kutaka kuwanyima wengine haki hiyo kwa visingizio mbalimbali. Haki ya kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapigakura nayo ni haki ya kila raia mwenye sifa za kupiga kura.

Hakuna mwenye haki ya kumtisha au kumzuia mwenye sifa asijiandikishe, au asipige kura siku ya uchaguzi. Kumtisha au kumzuia raia mwenzako mwenye sifa asijiandikishe, au asipige kura, ni ubinafsi na ukosefu wa uvumilivu, na ni kinyume cha sheria.

Pale mtu anaporidhika kuwa anayetaka kujiandikisha, au aliyejiandikisha, hana sifa, ufumbuzi si kuanza ugomvi. Upo utaratibu wa wazi, wa kisheria, wa kupinga. Sasa vitisho na fujo katika baadhi ya vituo ni za nini?

Na vitisho na fujo zikianza tutazamie nini kutoka kwa vyombo vya dola vyenye wajibu wa msingi wa sheria, ulinzi na usalama? Ndugu Wananchi: Kazi ya kuandikisha wapigakura kwenye daftari la kudumu inaendelea. Tujifunze na kujirekebisha kutokana na uzoefu wa maeneo ambayo tayari kazi imekamilika. Naomba sana tukamilishe vizuri na kwa amani kazi hii muhimu ya kuandikisha na kujiandikisha.

Ufanisi katika kazi hii utasaidia sana kuimarisha amani na heshima ya nchi yetu. Na ninarudia kumtaka kila Mtanzania mwenye sifa za kupiga kura ahakikishe anajiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.

Ndugu mwananchi, usikubali kutishwa au kukatishwa tamaa. Maana, usipojiandikisha, utakosa haki yako ya kuchagua viongozi unaowataka, na kuwaachia uwanja hao wanaohujumu demokrasia wakuchagulie wewe viongozi wanaowataka wao.

Ndugu Wananchi: Hatukuanzisha mfumo wa vyama vingi vya siasa ili kujenga chuki miongoni mwa Watanzania. Hivyo, tuwaogope sana wanaohubiri chuki kwa kisingizio cha ushindani wa kisiasa. Ushindani tunaoutaka sisi ni wa hoja, ni wa fikra, ni wa mikakati na mipango ya maendeleo. Tunashindanisha Ilani za Uchaguzi za Vyama.

OKTOBA 28, 2020 Tanzania itafanya Uchaguzi Mkuu kuchagua rais, wabunge ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi