loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tanzania yaijibu Kenya zuio la raia

MAMLAKA ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imefafanua sababu za kufuta kibali kilichokuwa kikiruhusu ndege za Shirika la Ndege la Kenya (KQ) kutua nchini ikisema serikali ya Kenya ndiyo ilianza kuvunja sheria za kibiashara za kimataifa kwa kufanya kitendo cha kibaguzi kwa Tanzania.

Sakata hilo limeibua hisia za watu wa kada tofauti kupitia mitandao ya kijamii, vyombo vya habari miongoni mwao wakiwa ni wanasiasa, wanadiplomasia na wachumi nchini wakiunga mkono uamuzi huo wa serikali.

Wakati wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wameshauri mawaziri wa pande mbili kukutana haraka kunusuru uchumi, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amesema kutakuwa na mkutano na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kujua chanzo cha Kenya kuzuia ndege za Tanzania kutua nchini humo. Ingawa Kenya kupitia kwa Waziri wake mwenye dhamana ya uchukuzi kuruka kimanga kuwa wamezuia ndege za Tanzania, watu waliozungumza na Habari- Leo Jumapili, wamesema pamoja na Tanzania kupata athari kiuchumi, uamuzi uliochukuliwa ni sahihi na Kenya itapoteza zaidi.

Muhimu kuheshimiana Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari alisema mikataba ya biashara ya anga ni ya usawa na ndiyo maana Tanzania ilivyofungua anga lake, haikubagua nchi yoyote jambo ambalo limekuwa tofauti kwa Kenya ilipoamua kufungua anga lake jana.

“Msingi mkubwa wa mikataba ya kimataifa ni usawa, sisi tumewapa fursa ya kufanya biashara kwetu lakini wao katika orodha ya nchi 11 walizoruhusu kufanya biashara ya usafiri wa anga, Tanzania haikuwamo hivyo hatukuwa na namna nyingine zaidi ya kutafuta usawa wa kibiashara,” alisema Johari.

Kwa mujibu wa Johari, Kenya iliomba kuanzisha huduma ya usafiri wa anga kwa kufanya safari 19 kwa wiki ikiwa ni mara 14 kwa Dar es Salaam, mara nne Kilimanjaro na mara mbili Zanzibar.

Ingawa mkurugenzi mkuu huyo alisema uamuzi uliofanywa na TCAA una athari kadhaa kwa nchi kwa kuwa ndege hizo zilikuwa zikiwaleta watalii nchini na kulipa mapato mbalimbali, alisema ni lazima kuheshimiana kwani Tanzania imeifungulia Kenya biashara lakini wao wanaifungia.

Hata hivyo, akizungumza kwenye kipindi cha Super Breakfast kinachorushwa na Redio ya East Africa, Mkurugenzi Mkuu huyo alisema hali ya namna hiyo ni kawaida katika biashara na kusema Tanzania imeamua kuchukua uamuzi sawa na uliochukuliwa na Kenya.

“Tumefikia uamuzi huo kwa sababu katika sheria na taratibu zinazosimamia uendeshaji wa usafiri wa anga kati ya nchi na nchi mataifa yanatakiwa yawe sawa kwa sawa, Kenya waliomba kuja Tanzania kuanzia leo (jana) kutua katika viwanja vya Dar es Salaam, Zanzibar na Kilimanjaro na sisi hatukuwa na tatizo tukawapa ruhusa, lakini baadaye tukasikia wao wanatuzuia tusiende kwao,” alisema Johari.

Aliongeza “Mwaka 2015 walizuia gari za watalii zisiingie Kenya, na sisi tukafanya hivyo baada ya siku mbili wao wakaondoa kikwazo walichotuwekea, tumetendewa kitu ambacho si sahihi na sisi inabidi tufanye hivi badala ya kukaa kimya na kuwaacha wao waendelee kufanya wanachotaka.

” Kenya yaruka kimanga Kwa upande wake, akihojiwa na East Africa Radio, Waziri wa Uchukuzi wa Kenya, James Macharia , alikanusha kuzuia ndege za Tanzania kutua nchini humo.

“Hakuna ndege ya Tanzania ambayo imezuiliwa kuingia Kenya, sisi tulisema hizo nchi tulizoziweka kwenye hiyo orodha watu wao wakifika hapa hawatakaa karantini, lakini kama nchi haipo kwenye hiyo orodha watawekwa karantini, sisi taarifa ya kuzuiwa kuingia Tanzania tumeipata lakini tutazungumza na wenzetu na tutasikilizana” alisema Macharia.

Watakaoathirika zaidi Mchambuzi wa masuala ya Kisera wa Mpango wa Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (Sagcot), Prudence Lugendo alisema uchumi wa Kenya unategemea zaidi sekta ya usafiri wa anga ambayo ndio moyo wa sekta ya utalii ya nchi hiyo ikitegemea zaidi safari za ndege za kimataifa.

Alisema pamoja na kutegemea utalii, hawana vivutio vingi na vizuri vyautalii kama ilivyo Tanzania na ambacho wamekuwa wakifanya ni kufaidika kupitia mgongo wa vivutio vya Tanzania ikiwamo Mlima Kilimanjaro.

“Walikuwa wakijitangaza kwa kutumia vivutio vyetu na kuwapata watalii, hapo walitumia ndege zao na kuwapitisha Nairobi ambako walilala katika hoteli zao na kujipatia kipato kisha kuwaleta Tanzania katika viwanja vitatu vya KIA, JNIA na Zanzibar,” alisema Lugendo.

Alisema hata wakati wa kurudi walitumia ndege zao kutoka Tanzania hadi Nairobi ambako wanalala na baadaye kurudi nyumbani kwao, huku wakiacha fedha nyingi nchini mwao.

Akiunga uamuzi wa kuzuia ndege za nchi hiyo, Lugendo alisema “Kuna athari kubwa na ya moja kwa moja katika uchumi wao kwa sababu watapata hasara kubwa kutokana na matangazo wanayotumia kujitangaza katika vyombo vya habari vya kimataifa.”

Wengi wanaozungumzia uamuzi wa Tanzania kuzuia ndege za nchi hiyo wanasema kwa Kenya unamaanisha kwamba watalii wao waliokuwa wakitumia KQ kuja nchini wakipitia Nairobi, watalazimika kutumia mashirika mengine kuja moja kwa moja nchini jambo ambalo ni faida.

Vile vile usafirishaji wa mazao ya kilimo ikiwamo maua kwa ajili ya kulisha masoko ya nje, pia umeathiriwa na hatua hii iliyochukuliwa na TCAA.

Usafiri wa anga unatajwa na wachumi kuwa ni nyenzo muhimu katika kulisha masoko ya nchi hiyo hivyo kuzuiwa kwa ndege zao kuingia Tanzania kunamaanisha soko litakosa bidhaa hizo na hivyo kuingia hasara.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Mohamedi Bakari aliliambia Habarileo kuwa kinachoendelea kati ya Tanzania na Kenya ni mikakati ya kiuchumi ya kushinda soko baina ya washindani wawili na siyo tahadhari ya Virusi vya Corona kama inavyosemwa.

“Hapo ndo tunaona kuwa suala hili ni mikakati ya kiuchumi ili kushinda soko baina ya nchi hizi. Kenya siku zote katika Afrika Mashariki inajua kuwa mshindani wake ni Tanzania kwa hiyo wanataka soko lote liwe mikononi mwao,” alisema.

Wabunge EAC washauri Akizungumzia na gazeti hili jana, Mwenyekiti wa Wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)kutoka Tanzania, Dk Abdullah Makame alisema uamuzi wa nchi hizo kufungiana hauna afya kwa jumuiya kwani lengo la kuwa na mtangamano ni kuondoa mipaka baina ya nchi zote za EAC.

Dk Makame alishauri mawaziri katika nchi hizo kukutana mapema kujadiliana na kufikia muafaka huku akisema suala hilo likiachwa kwa wiki moja, athari za kiuchumi zitakuwa kubwa kwa pande zote mbili .

“Hili siyo suala la marais kukaa bali ni mawaziri kwa kuwashirikisha wataalamu katika nyanja husika ,hakika hali hii siyo nzuri ,lakini sidhani kama litakaa kwa muda mrefu kwani ikichukua muda mrefu inaweza kuathiri na katika maeneo mengine muhimu,”alibainisha.

Alisema licha ya kuwa suala hilo siyo zuri lakini katika uhusiano wa kimataifa ,jambo hilo siyo jipya kutokea kwa Tanzania na Kenya.

Lakini alisema ni vema pande hizo zikalimaliza kwani tangu kulipuka kwa corona, mambo hayajakaa sawa kati ya nchi hizo.

Alisema taswira iliyopo ni mbaya kwa EAC kwa kuonesha kama vile viongozi wao ambao wanatakiwa kuunganisha wananchi wanatengana. Urusi yaifungulia Tanzania Katika hatua nyingine, Serikali ya Urusi imeanza kufungua safari zake za ndege za kimataifa na miongoni mwa nchi ambazo ndege zake zitakwenda nchini humo ni Tanzania.

Nyingine ni Uingereza na Uturuki ikiwa ni zaidi ya miezi minne baada ya kufungwa kwa mipaka yake kutokana na ugonjwa wa covid-19.

KATIBU Tawala wa Wilaya ...

foto
Mwandishi: Selemani Nzaro, Theopista Nsazugwanko na Rahel Pallangyo.

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi