loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Presha inapanda na kushuka kwa wagombea ubunge CCM

VIKAO vya mchujo vinaendelea ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa lengo la kupata jina la moja la atakayepeperusha bendera ya chama kwa madiwani, ubunge na uwakilishi huku matumaini na presha vikitawala miongoni mwa wagombea waliopigiwa kura za maoni.

Kauli ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyoitoa juzi akihutubia Baraza la Idd al Haji, akisema wajumbe katika kura za maoni wametoa mwongozo lakini uamuzi uko juu, ni uthibitisho kwamba vikao hivyo vinaweza kuja na matokeo tofauti na kura za maoni hivyo walioongoza wakaenguliwa na waliodhaniwa wameshindwa wakaibuka washindi.

Waziri Mkuu alimtania aliyegombea ubunge jimbo la Handeni Vijijini, Hussein Msopa (Shehe Sharif Majini) akisema, “mchakato unaendelea tunakuombea sana basi kile kikao cha mwisho kikurudishe.

Lakini waliokupa ni wajumbe… wametoa mwongozo tu. Maamuzi yako juu huko tunaamini Inshallah kule Handeni utakuwa mbunge. Tunakuombea.”

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alipohojiwa hivi karibuni katika kipindi cha Mizani kilichorushwa na Televisheni ya Taifa (TBC) chini ya mada ya ‘Mchakato wa kupata wagombea wa CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu’, alisema kwa kuzingatia Ibara ya 67 ya katiba ya chama, mchakato wa awali wa kura za maoni unawapatia picha.

Kulingana na kauli ya Polepole, Kamati ya Siasa ya Wilaya kwa mujibu wa ratiba imeshakamilisha kazi yake, imejadili majina na kuweka mapendekezo kwa majina matatu na kueleza sababu za kupendekeza mojawapo.

Kamati ya Siasa ya Mkoa pia ilipaswa kujadili na kutoa mapendekezo kabla ya juzi (Julai 30) kwa kujadili majina yote na kama yanawiana na ya Kamati ya Siasa ya Wilaya wanaridhia na kama hawaridhii, wanapendekeza mwingine.

“Lakini wana haki ya kusema hapana, sisi tumempendekeza mwingine, huyu waliyempendekeza wilaya hapana kwa sababu wana taarifa za maadili na mambo kama hayo,” alisema Polepole.

Baada ya Kamati ya Siasa ya Mkoa, wanapelekewa viongozi watendaji wa taifa kwa maana ya Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ambayo kwa mujibu wa Polepole, watapitia taarifa nyingi zaidi ambazo ni za kiusalama na maaadili.

“Na chama kina intelijensia kubwa sana na imejengwa kwa madhubuti. Tumekuwa tukifuatilia mienendo ya wagombea hawa muda mrefu kwa hiyo taarifa zao tunazo na sisi tutasema huyu anastahili ila huyu hastahili na dhambi zake ni kama ifuatavyo.

“Baada ya hapo tutakwenda kwenye Kamati Kuu, itajadili halafu baada ya hapo, itapeleka kwenye Halmashauri Kuu na mwenyekiti ni Ndugu Magufuli (Rais John), watapiga kura kuchagua jina moja ambalo mtu huyo atakuwa ndiye mgombea wa chama chetu cha mapinduzi katika kugombea ubunge katika majimbo,” alisema Polepole.

Upande wa Viti Malumu, majina yataingia kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa kwa mazingatio. Upande wa udiwani, Kamati ya Siasa ya Kata baada ya kujadili na kuweka mapendekezo na kupeleka kwenye Kamati ya Siasa ya Wilaya.

Kisha majina yatakwenda kwenye Kamati ya Siasa ya Mkoa na baadaye Halmashauri Kuu ya Mkoa itakayofanya uteuzi wa mwisho wa atakayepeperusha bendera ya CCM.

Kulingana na ratiba iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Polepole, jana (Agosti Mosi) na leo, vinakaa vikao vya kamati za siasa za CCM wilaya kujadili wagombea na kutoa mapendekezo yake kwa kamati za siasa za mkoa.

Agosti 4 hadi 5 vitaketi vikao vya kamati za siasa za kwa ajili ya kutoa mapendekezo kwa vikao vya juu. Vigezo vinavyozingatiwa Polepole alifafanua kwamba mchujo unazingatia sifa za msingi za kiongozi kwenye chama kama zinavyoanishwa na katiba na kanuni ikiwamo kutosheka, kutotawaliwa na tamaa.

Sifa zilizopo kwenye kanuni ni awe asiyetiliwa shaka katika eneo lake, muadilifu na anayekubalika na wananchi kwa jumla. Alipozungumza na waandishi wa habari hivi karibuni kuhusu ratiba ya mchakato wa kupata wagombea, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Polepole alisisitiza kwamba kura za maoni zinapigwa zisaidie kuangalia mwelekeo lakini uamuzi utaendana na mapendekezo ya vikao kabla ya uteuzi wa mwisho kupitia kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa.

Waliocheza rafu Kauli za viongozi hao wa chama zinakuja kukiwa na malalamiko kwamba katika baadhi ya maeneo, kura za maoni zilitawaliwa na vitendo vya rushwa huku baadhi ya wagombea wakinyooshewa vidole hali inayozua presha kwa wanaotuhumiwa na kutengeneza matumaini kwa waliopata kura chache bila kutoa rushwa.

Miongoni mwa waliolalamika ni baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Jimbo la Kilolo mkoani Iringa waliotuhumu kuwapo vitendo vya rushwa kwenye kura za maoni.

Msimamizi wa Uchaguzi huo, Lazaro Manila alipozungumza na waandishi wa habari alisema “tunatarajia kupokea taarifa mbalimbali zikiwamo pia za vyombo vya dola na kama kuna malalamiko kutoka kwa wapiga kura au wagombea, utaratibu unataka wayawasilishe kwa mamlaka zinazohusika yafanyiwe kazi.”

Mei mwaka huu, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu mchakato wa uchaguzi ndani ya chama kuelekea Uchaguzi Mkuu, Polepole alisema chama kinafahamu waliofanya vurugu kwenye majimbo ya uchaguzi na kata.

Alisema, “tunawafahamu wote, tuna ushahidi wenu wa sauti, wa video, picha barua za malalamiko… nataka kuwatangazia kwa niaba ya chama, wavurugaji wote na walioanza kampeni kabla ya wakati hawatapewa uongozi wowote kwenye Chama Cha Mapinduzi .

Hivyo chama kinatambua waliofanya.” Wiki hii Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) ilinukuliwa na gazeti hili ikikiri kukamata wagombea 20 mkoani Arusha wakituhumiwa kutoa rushwa.

Uchaguzi 2015 Katika uchaguzi wa mwaka 2015, baadhi ya wagombea walioongoza kwa kura nyingi kwenye kura za maoni walitupwa nje na kuchukuliwa mshindi wa tatu.

Baadhi ya majimbo yalilazimika kurudia kupiga kura za maoni na mengine kuhesabu upya kura zilizopigwa baada ya kujitokeza malalamiko miongoni mwa wagombea.

KATIBU Tawala wa Wilaya ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi