loader
Mapokezi Simba usipime

Mapokezi Simba usipime

SIMBA jana ilipokewa kishujaa na mashabiki ikitokea mkoani Rukwa, walikochukua ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam baada ya kuifunga Namungo FC kwa mabao 2-1 kwenye mchezo wa fainali uliofanyika Uwanja wa Nelson Mandela, Mjini Sumbawanga.

Shangwe hizo za mapokezi zilianzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere Dar es Salaam, ambapo mashabiki walifurika kuipokea na kuandamana nayo katika mitaa mbalimbali kabla ya kuwasili makao makuu ya klabu yao mtaa wa Msimbazi.

Wachezaji wa kikosi hicho pamoja na baadhi ya viongozi walipanda gari ya wazi wakiwa wamebeba makombe yote matatu, lile la Ligi Kuu, Ngao ya Jamii na lile la Shirikisho la Azam au Kombe la FA.

Mbali na mashabiki waliotembea kwa miguu wakifuata msafara huo, mashabiki wengine wakiwa katika pikipiki na wengine katika magari yao binafsi walipita barabara za Nyerere, Mandela, Uhuru na Msimbazi yaliko maskani yao.

Msafara huo ulipofika Msimbazi ulipokewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na Mbunge wa Ilala, Mussa Hassan Zungu aliyekuwa pamoja na Mkurugenzi wa Kampuni ya Michezo ya Kubahatisha, Abbas Tarimba.

Kwa upande wake, nahodha wa kikosi hicho John Bocco ambaye kwenye mchezo wa fainali alifunga bao la ushindi alifurahishwa na umati wa mashabiki waliojitokeza kwenye mapokezi hayo na kubainisha kwamba wanastahili kufanya hivyo kwa kuwa wametoka mbali.

“Mashabiki na wachezaji niwapongeze wote kwa kuwa tunategemeana tumepambana na tumetoka mbali, umati uliojitokeza unastahili kuendelea kufurahia matunda ya mafanikio tuliyopata ndani ya msimu huu,” alisema Bocco.

Clatous Chama aliyeka bidhiwa kitita cha Sh milioni 1 na wadhamini wakuu wa Simba, SportPesa ya mchezaji bora, aliwapongeza mashabiki kwa kumpigia kura pamoja na wachezaji wenzake, ambayo aliahidi kuitoa kwa watoto yatima Kinondoni.

Zungu aliwapongeza wachezaji na viongozi wa Simba kwa kufikia mafanikio makubwa ya kutwaa mataji matatu ndani ya msimu mmoja na kwamba ni mwaka wa kihistoria na kuwaomba kuendelea kujipanga ili kuwakilisha vyema kimataifa.

“Umekuwa msimu wa mafanikio kwenu kwani mmefanikiwa kubeba makombe matatu, na hiyo inaonesha mlivyojipanga, ni wakati sasa wa kujipanga kufanya vizuri kimataifa ili kuendeleza mlipofikia,” alisema Zungu.

Tarimba aliwapongeza Simba na kubainisha kwamba mafanikio hayo yanazidi kukoleza uhusiano wa kufanya kazi pamoja na kampuni hiyo na kuhakikisha wanafanya vizuri kimataifa.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/85d4a281f26fd224cecaaa42d5a557b1.jpg

WAZIRI wa Afya,  Ummy Mwalimu ...

foto
Mwandishi: Tuzo Mapunda

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi