loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mboga, maua, matunda vyaingiza Dola za Marekani milioni 779

JUMLA ya Dola za Marekani milioni 779 zimepatikana kutokana na mauzo ya mazao ya mboga, matunda, maua na viungo nje ya nchi mwaka jana.

Akizungumza kwenye maonesho ya Wakulima, wafugaji na wavuvi maarufu Nanenane yanayoendelea kitaifa katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu, Meneja Mazingira ya Biashara wa Asasi ya Sekta Binafsi ya kuendeleza kilimo cha mazao (TAHA), Kelvin Remen alisema kilimo hicho kina faida endapo wakulima watazingatia kanuni za ugani.

Alisema kila mwaka wakulima wa mazao hayo wanaboresha kilimo hicho na kulima kwa tija hivyo kupata mazao bora na mengi yenye soko zuri ndani na nje ya nchi.

Remen alisema TAHA ilianzishwa mwaka 2004 na imekuwa jukwaa la sauti za wadau wa mazao hayo katika mnyororo wa thamani na imewawezesha wakulima na wadau wengine ndani ya mnyororo huo kulima kwa tija na kuongeza mavuno na kupata masoko zaidi nje ya nchi.

Alisema mauzo ya mazao hayo nje ya nchi yanaongezeka mwaka hadi mwaka na kwamba mwaka 2006 mauzo ya mazao hayo nje yalikuwa Dola milioni 64 tu na kwamba ilipofika mwaka 2019 mauzo yaliongezeka na kufikia Dola milioni 779.

“Haya ni mapinduzi makubwa yamefanywa kweli kilimo cha mboga, maua, matunda, viungo na uzalishaji mbegu wa mazao hayo, tumewasaidia wakulima kulima kwa kufuata kanuni bora na pia tumefanikisha kuwezesha mazao hayo kupata masoko nje na tunayasafirisha katika magari maalumu kutoka mashambani hadi kufika viwanja vya ndege, ndio maana kiwango cha mauzo nje kinaongezeka,” alisema Remen.

Alisema hivi sasa fursa katika kilimo hicho ni kubwa na mahitaji yameongezeka na kwamba wakulima sio lazima walime eneo kubwa, bali wanaweza kuanza au kuwa na eneo dogo na kulima mazao hayo kwa kufuata taratibu za ugani na kufanikiwa ndani ya muda mfupi.

Alisema hadi sasa TAHA ina jumla ya wanachama 40,000 ambao ni wazalishaji au wakulima wadogo na wa kati nchi nzima ambao wako katika vikundi na wengine ni mtu mmoja mmoja.

Aidha TAHA pia ina wanachama wengine 150 ambao ni wakulima wakubwa na watoa huduma ambao ni kama vile wazalishaji mbegu,viuatilifu na watoa usafiri wa magari maalumu ya kubeba mazao hayo.

foto
Mwandishi: Ikunda Erick, Bariadi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi