loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Huduma za maji kuboreshwa

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kwa kushirikiana na Wizara ya Maji (WM) zimejipanga kuboresha huduma ya majisafi jijini humo, ukiwemo kuwa na mpango wa muda mrefu wa kuchukua maji kutoka Ziwa Victoria.

Mipango hiyo ya Duwasa ilielezwa na Meneja Ufundi, Kashilimu Mayunga kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Duwasa, David Pallangyo katika mkutano wa wafanyabiashara na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge.

Mkutano huo ni wa pili kufanyika baada ya wa kwanza kufanyika Julai 7, mwaka huu, na hivyo ulikuwa ukitoa majibu ya malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu upungufu wa huduma ya maji katika baadhi ya maeneo katika jiji hilo.

Mayunga alisema mpango wa muda mrefu wa kuchukua maji kutoka Ziwa Victoria unaratibiwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Mamlaka za Maji za Mkoa wa Dodoma, Singida na Kahama.

“Tayari upembuzi yakinifu wa awali umekamilika na umeonesha uwezekano mkubwa wa kufikisha maji ya Ziwa Victoria katika jiji la Dodoma,” alisema.

Katika mpango wa muda wa kati alisema, Duwasa inatekeleza mradi wa ujenzi wa Bwawa la Farkwa katika wilaya ya Chemba ambao unaratibiwa na Wizara ya Maji. Katika kutekeleza miradi huo, tayari wananchi wanaoishi katika maeneo ya ujenzi wa Bwawa wamelipwa fidia ya Sh bilioni 7.6 kwa sasa wizara inatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo.

Katika mipango ya muda mfupi, Duwasa inaendelea na uchimbaji visima katika maeneo ya pembezoni mwa Jiji hilo ili kupata vyanzo vya nyongeza vya maji vinavyojitegemea na kuhudumia wananchi walio karibu.

“Duwasa tayari imeshachimba visima katika mji wa serikali Ihumwa na Mtumba. Uchimbaji huo wa visima unafanyika katika maeneo ya Zinja, Nytuka, Michese, Mbwanga na Mpamaa,” alisema.

Alisema ni kweli kwamba katika siku za hivi karibuni kulikuwa na upungufu wa maji, lakini ni kutokana na hitilafu ya pampu kubwa mbili za visima. Pampu hizo ziliagizwa nje ya nchi lakini kutokana na changamoto ya Covid-19 zilichelewa kuwasili.

Pampu hizo moja iliwasilishwa Juni 17 na kufungwa Juni 22, mwaka huu wakati nyingine tatu ziliwasili Julai 12 na tayari zimeshafungwa. Kwa sasa hali ya upatikanaji wa maji imeendelea kuimarika kwenye maeneo mbalimbali na maeneo ya miinuko nayo yameanza kupata maji.

Kuhusu suala la matumizi ya maji bwawa la Farkwa, Mayunga alisema mradi wa bwawa hilo umezingatia pia matumizi mengine yakiwemo ya kilimo cha umwagiliaji na unyweshaji mifugo kwa wananchi wa Wilaya ya Bahi, Chemba, Kondoa na Dodoma.

MGOMBEA Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi