loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wanawake wasiwe wapigadebe, wasindikizaji katika uchaguzi

TAMKO la Kimataifa Kuhusu Haki za Binadamu (UDHR 1948), Mkataba wa Kimataifa wa Kutokomeza aina zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW 1979) katika Kifungu cha 7: (a,b na c) na Mapendekezo ya Baraza la Usalama (UNSC 1325 (2000) yanatoa na kutambua haki za wanawake kushiriki katika uchaguzi kama wapigakura na wanaowania nafasi za uongozi, wanaoteuliwa na kugombea hatimaye kushinda katika nafasi mbalimbali za uongozi kwa kupitia uchaguzi.

Aidha, haki hiyo inayotambuliwa na kutajwa pia katika mikataba mbalimbali ya kimataifa, kikanda na katika sheria, sera na katiba ya nchi, imo pia katika Mpango Kazi wa Beijing (1995), Malengo ya Milenia ya Maendeleo (Lengo la 3), pamoja na Mkataba wa Afrika Kuhusu Haki za Binadamu.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) nayo inabainisha haki za wanawake kushiriki katika nafasi mbalimbali za uamuzi, ikiwa ni pamoja na ushiriki wao katika uchaguzi wakiwa wapigakura na wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi.

Kana kwamba hiyo haitoshi, Dira ya Taifa ya Mwaka 2025 inabainisha azma ya Tanzania kutokomeza aina zote za ubaguzi wa kijinsia. Pamoja na mikataba na miongozo yote hiyo ikiwamo ya kimataifa, bado siasa za Tanzania hasa katika baadhi ya vyama, zinakiuka na kumwona mwanamke kama mwenye jukumu pekee la kuwapigia debe wagombea wanaume, kuwa wasindikizaji na waburudishaji katika misafara na kampeni za wagombea.

Hili si jambo jema kwa Tanzania ya sasa. Vyama vingi wanawake hawachaguliwi wala kuteuliwa katika nafasi za juu. Ni kwa msingi huo, Tanzania inapoelekea katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, 2020 ambao mchakato wake unaendelea katika vyama na taasisi mbalimbali wadau wa uchaguzi wanasema, wanawake hawapaswi kuachwa ili wengi waendelee kutumika kama wapigadebe, wasindikizaji na waburudishaji katika kampeni za uchaguzi, bali wenye ushiriki kamili wa kuchagua na kuchaguliwa katika uongozi kwa kadiri wanavyoonekana kufaa kwa wapigakura. Ikumbukwe kuwa, nchini Tanzania, vyama vya siasa ndiyo njia pekee ya wananchi kuingia katika kinyang’anyiro cha uchaguzi.

Huu ndio utaratibu waliojiwekea Watanzania kwamba, hakuna mgombea binafsi na hali hii, inasaidia kupata viongozi bora wanaoanza kumulikwa na vyama kabla sauti ya wananchi haijasikika. Ilani ya Uchaguzi ya Wanawake: Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 na Uchaguzi Mkuu 2020: Ajenda ya Mwanamke, Turufu ya Ushindi 2019/2020, inasema: “Vyama vya siasa ni walinzi wa lango kuu la kuingia kwenye siasa za uchaguzi.”

Kimsingi, vyama vya siasa ndivyo huamua ni nani aingie na ni nani aachwe, ni nani awezeshwe kushinda na pia ni nani aachwe akiogelea mwenyewe kwenye uwanja wa ushindani usiyo haki na huru kwa wanawake walio wengi.

Ndiyo maana hivi karibuni mradi uitwao ‘Wanawake Sasa’ unaofadhiliwa na taasisi ya African Women Development Fund (AWDF), uliendesha mafunzo kwa wanahabari kutoka katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Dodoma na Zanzibar yakilenga kuhamasisha na kuchochea ushiriki kamilifu wa wanawake katika siasa na uongozi.

Wakili Mary Mwita ambaye ni mwezeshaji wa masuala ya kijinsia anasema katika mafunzo hayo kuwa, katika uchaguzi huu jamii iachane na mila kandamizi zinazombagua mwanamke katika masuala ya siasa na uongozi kwani hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 inatoa haki kwa kila mwenye sifa kuchagua au kuchaguliwa kuwa kiongozi.

Akitoa mfano wa uadilifu na uwezo mkubwa walio nao wanawake katika uongozi, Mary anamtaja Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akisema: “Uwezo wa uongozi wa Makamu wa Rais; Mama Samia, ni mfano tosha kuwa wanawake wana uwezo mkubwa katika uongozi na ni waadilifu na wachapakazi.”

Miongoni mwa wanawake walioonesha uwezo mkubwa katika uongozi ni pamoja na Makamu wa Rais, Samia ambaye ni mwanamke wa Kwanza Tanzania kuwa makamu wa rais, na Anne Makinda ambaye ni Spika Mstaafu na mwanamke wa kwanza kuwa Spika katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alistaafu mwaka 2015 baada ya kuliongoza vyema Bunge. Kwa mujibu wa Wakili Mary, moja ya kasumba zinazochangia ukatili wa kuwabagua na kuwaacha wanawake wengi nyuma kisiasa na kiuongozi, ni imani potofu iliyojengeka hata kwa wanawake wengi katika jamii na makabila mbalimbali kuwa mwanamke hawezi na hapaswi kuwa kiongozi jambo analosisitiza kuwa siyo sahihi.

Anasema: “Hapa inabidi wanawake wabadilike na waungane mkono; waache chuki; wasipingane na badala yake, pale wanapoona mwanamke mwenzao anazo sifa na uwezo, wamuunge mkono kwa kumpigia kampeni na kumpigia kura.”

Mintarafu changamoto ya rushwa ya ngono katika uteuzi au uchaguzi wa kisiasa ndani ya vyama, anasema: “Wanawake wasiruhusu udhalilishwaji huu; mwanamke simamia taaluma na uwezo wako wa kiungozi na kimaadili kamwe usiruhusu madai ya rushwa ya ngono kupata nafasi na pia, wanahabari wawe kioo cha kutoruhusu kutumika kudhalilisha wanawake…”

Naye Stelius Sane ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari, anaishauri Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuongeza nguvu zaidi na kutumia mbinu zake kuwabaini, kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wote wanaojaribu kudai rushwa ya ngono kwa wagombea au wanachama ili wapitishwe katika nafasi za uteuzi kwa kuwa kitendo hicho ni kinyume na Kifungu cha 25 cha Sheria Namba 11 ya Mwaka 2007 ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa wakati wa uchaguzi. Changamoto nyingine kwa mujibu wa mwezeshaji huyo, ni ukosefu wa rasilimali fedha na majukumu mengi ya kifamilia.

“Dawa ya mambo haya, ni Watanzania wenye matashi mema kusaidia kwa namna mbalimbali, ikiwa ni pamoja na usafiri na mahitaji mengine huku familia zikijitokeza kuwaunga mkono na kufanya mgawanyo bora wa majukumu unaowapa wanawake nafasi ya kuendelea na mchakato au kampeni wakati wa uchaguzi,” anasema Mary.

Kijoli Chikopa aliyeomba kuteuliwa katika viti ubunge wa viti maalumu kupitia Vijana mkoani Pwani anasema: “Pesa inahitajika hata katika uchukuaji wa fomu yaani Sh 100,000; wanawake wengi ni vigumu kuipata na kuhusu muda, ni changamoto maana unahitaji kuhudumia familia, lakini pia unahitaji kuwafikia wapiga kura ili wakufahamu vizuri maana wengine tulitia nia, lakini watu wengi hawatujui vizuri, lakini yote hayo, lazima kujipanga …”

Anasema katika hatua zinazoendeleaza uchaguzi wa mwaka huu, Watanzania wanahitaji kushirikiana kwa dhati kupata viongozi bora bila kutanguliza rushwa, wala ubaguzi, unyanyasaji na udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya wanawake maana wanawake wengi wana uwezo mkubwa wa uongozi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Rose Reuben, anasema kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020, wanawake wanapaswa kushirikishwa kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi tangu awali.

“Wakishirikishwa vizuri katika vyama vyote, Tanzania itaimarika zaidi kidemokrasia na ndiyo maana tunajiandaa kuhamasisha zaidi hili lifanikiwe,” anasema Rose na kuongeza: “Vyama vyote vya siasa vihakikishe vinatoa nafasi na mazingira wezeshi kwa wanawake…”

Rose Reuben anasema: “Ili wanawake wasiwe wasindikizaji, wapigadebe na waburudishaji katika kampeni za uchaguzi wa kisiasa, vyombo vya habari navyo vitoe fursa sawa kwa wagombea wote wa kike na wa kiume wakati wa kampeni na visitumike kuendeleza lugha za matusi, kejeli na udhalilishaji dhidi ya wanamke hasa wanaowania uongozi wakati wa uchaguzi.”

Watu mbalimbali wanasema ipo haja jamii na serikali kwa jumla, kuboresha mazingira ili yawe wezeshi na salama zaidi kwa wanawake wakati wote wa mchakato wa uchaguzi. Watetezi wa haki za binadamu na usawa wa kijinsia wanataka wadau wa uchaguzi wazingatie misingi ya ushindani wa haki na huru na usawa wa jinsia kama ilivyoainishwa kwenye katiba, sheria, sera, mipango ya nchi na kubainishwa kwenye mikataba ya kimataifa na kikanda ambayo Tanzania imeiridhia.

Kimsingi, yapo mambo muhimu ya kufanya ili uchaguzi mkuu wa mwaka huu uwe shirikishi kwa jinsia zote, ikiwa ni pamoja na vyombo vyote vilivyopewa dhamana ya kusimamia uchaguzi vikiwamo vyombo vya kuzingatia miongozo, na sheria zenye kulinda wanawake dhidi ya matendo ya udhalilishwaji wakati wa uchaguzi.

Wanawake wenyewe wanadai kuwapo uzingatiaji wa misingi ya haki na usawa hasa kuanzia wakati wa uteuzi wa wagombea wanawake ndani ya vyama ili nao wateuliwe kugombea katika nafasi muhimu.

Wadau hao wanavihimiza vyombo vya habari kuelimisha jamii mintarafu haki za wanawake na kutoa fursa kwa wagombea wanawake ili wajinadi kwa wapigakura kwa bei nafuu hali itakayowafanya wasiwe wasindikizaji wala waburudishaji katika kampeni, bali washindani wa kweli katika siasa.

Vyombo vya habari viepuke kasumba ya kuwadhalilisha wanawake kwa picha na kauli zenye kuwadhalilisha na kuwatisha na kuwakatisha tamaa.

Wadau wanataka vyama vya siasa viwajibike kuweka misingi na mfumo wezeshi wa ushiriki kamilifu wa wanawake katika uongozi ndani ya vyama na nje ya vyama kwa kujiwekea kanuni zinazowajibisha viongozi wa vyama kutokunyanyasa wanawake ama ndani, au nje ya vyama.

TANZANIA imeridhia mikataba na matamko mbalimbali ya kimataifa yanayotoa haki ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi