loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Sababu kupanda bei za limao, ndimu zatajwa

IMEBAINIKA kupanda ghafla kwa bei ya limao na ndimu katika masoko ya jijini Dar es Salaam kunatokana na bidhaa hizo kuwa na mahitaji makubwa katika masoko ya Nairobi na Mombasa nchini Kenya, ambako wanatumia kama tiba ya asili dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu (covid-19) unaosababishwa na virusi vya corona.

Mahitaji ya limao na ndimu ambazo zinalimwa kwa wingi wilayani Muheza, mkoa wa Tanga, katika masoko hayo bei imepanda kwa kasi kwa kipindi cha wiki mbili zilizopita.

Inaelezwa kuwa kati ya njia iliyoisaidia Tanzania kukabiliana na tatizo hilo ni kutumia njia za asili za kujifukiza kwa kutumia mchanganyiko wa vitu mbalimbali yaki wemo malimao na ndimu, hali ambayo imewavutia baadhi ya wananchi wa nchi hiyo jirani yenye maambukizi makubwa ya corona.

Wakizungumza na HabariLEO kwa nyakati tofauti wilayani Muheza jana, baadhi ya wakulima na wafanyabiashara wa limao na ndimu wanaopeleka bidhaa hizo katika masoko ya Kenya na Dar es Salaam, walisema kwa muda wa mwezi mmoja uliopita bidhaa hiyo ilikuwa ikipatikana kwa wingi, lakini sasa zimekuwa adimu kutokana na kuwapo mahitaji makubwa.

Walisema hali hiyo inatokana na wafanyabiashara kutoka Dar es Salaam, Unguja, Mombasa na Nairobi, kuja wilayani hapa kwa wingi kutafuta bidhaa hizo kutoka mashambani.

Mustafa Rashidi, mkulima wa malimao, machungwa, ndimu na machenza katika kijiji cha Kwemkunde, alisema mwanzoni mwa Julai kiroba kimoja cha malimao kilikuwa kikiuzwa kwa Sh 40,000 shambani lakini sasa kimepanda hadi Sh 90,000, wakati limao moja likiwa shamba liliuzwa kati ya Sh 30 hadi 50 lakini sasa linauzwa kati ya Sh 250 hadi 300 wilayani hapa.

Alisema debe moja la bidhaa hiyo lenye ujazo wa kilo 20 lilikuwa likiuzwa Sh 15,000, lakini sasa limepanda hadi kufikia Sh 30,000.

Kwa upande wa ndimu, alisema kiroba kimoja kwa sasa kinauzwa kati ya Sh 95,000 hadi Sh 100,000 kutoka Sh 60,000 na debe moja linauzwa Sh 40,000 kutoka Sh 20,000. Mfanyabiashara, James Huruma, anayesafirisha malimao kutoka Muheza kupeleka Dar es Salaam, alisema jijini humo bidhaa hiyo imepanda bei ghafla kutokana na uchache, ambapo kwa sasa katika masoko ya Ilala, Temeke Stereo, Tegeta na Mabibo, limao moja kwa bei ya jumla linauzwa kati ya Sh 500 hadi Sh 700 na kiroba kimoja kwa bei ya jumla kinauzwa Sh 200,000.

“Dar es Salaam katika masoko maarufu ya Ilala, Temeke, Mabibo, Tegeta ukiwa na malimao sasa hivi unafanikiwa kutokana ni bidhaa hiyo kuwa adimu na ina mahitaji makubwa kwa sasa kutokana na kupelekwa zaidi Kenya kuliko Dar es Salaam,” alisema.

Kwa upande wake, Odhiambo Otieno, mfanyabiashara wa Kenya ambaye amekuja Muheza kuchukua bidhaa hiyo, alisema imekuwa na uhitaji mkubwa baada ya kuona Watanzania wamefanikiwa kudhibiti virusi vya corona kwa njia ya asili kwa kutumia malimao.

“Baada ya kugundua hilo katika masoko makubwa ya Kongowea Mombasa katika mkoa wa Pwani na soko kub wa la Mavare jijini Nairobi, limao moja linauzwa kati ya Sh za Kenya 30 sawa na Sh za Tanzania 650 hadi 700 na Sh 50 za Kenya ambayo ni sawa na Sh 1,100 hadi Sh 1,200 za Tanzania.”

“Magari mengi ya Tanzania ya mizigo yanakwenda Kenya na magari ya Kenya yenye namba za usajili wa Kenya yapo hapa Muheza si kwa ajili ya kufuata machungwa kama ilivyozoeleka, bali ni kwa ajili ya malimao kuwa na mahitaji makubwa na yanatumika kama tiba dhidi ya virusi vya corona,” alisema.

Mwandishi wa habari hii alimtafuta  kwa njia ya simu Ofisa Mfawidhi wa Forodha wa kituo cha pamoja cha mpaka wa Tanzania na Kenya (OSBP) kwa upande wa Tanga, Horohoro, Bakari Athumani, kutaka kujua idadi ya magari yanayopita katika mpaka huo kwa siku yenye bidhaa hiyo lakini hakupatikana.

 

MGOMBEA Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia ...

foto
Mwandishi: Cheji Bakari, Muheza

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi