loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kufuga samaki kutumia vizimba ‘ndio habari ya mjini’

MPANGO wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016 – 2021) unaosisitiza nchi kuwa ya viwanda, unahimiza pia shughuli zote za maendeleo zifanywe kwa kutumia teknolojia za kisasa na zenye tija ili kuongeza uzalishaji.

Ni katika muktadha huo, sekta mbalimbali zimeanza kutekeleza mpango huo huku zikishirikisha wadau mbalimbali, na sasa matokeo chanya yameanza kuo nekana.

Mfano mmojawapo ni sekta ya uvuvi. Kupitia Maonesho ya 27 ya wakulima, wafugaji na wavuvi yaliyoanza rasmi Agosti mosi mwaka huu huku yakiwa na kaulimbiu isemayo: ‘Kwa maendeleo bora ya uvuvi, kilimo, chagua viongozi bora,’ yamekuwa chachu kwa washiriki kupata fursa ya kujifunza na kuona zana bora za kilimo zinazotumika sasa kuleta tija kwenye uzalishaji.

Kitaifa maonesho hayo maarufu kama Nanenane yanafanyika katika viwanja vya Nyakabindi wilayani Bariadi, mkoa wa Simiyu.

Halikadhalika maonesho kama haya yanaendelea kwenye kanda nyingine tano nchini yakilenga kuonesha teknolojia za kisasa na mbinu mpya zinazobuniwa na wadau mbalimbali zikilenga kuongeza tija kwenye sekta hiyo.

Katika sekta ya uvuvi, ufugaji samaki kwa kutumia mabwawa ndiyo njia iliyozoeleka na inayotumiwa na wananchi wengi, lakini kuna njia nyingine mbili; ufugaji samaki kwenye madumu/ matangi ambao makala haya hayatauangazia kwa kina na ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba (cages) katika maji ya asili ambayo ni maziwa, mito au bahari.

Ufugaji huu wa vizimba ambao ndio utaangaliwa zaidi katika makala haya, unaanza kwa mtu kutengeneza kizimba, na kisha kizimba hicho kukitumbukiza kwenye maji mengi (maziwa au bahari), kuweka vifaranga vya samaki na kuanza kufuga.

Ufugaji huu wa samaki kwenye vizimba ni mfumo ambao samaki wanawekwa kwenye uzio uliotengenezwa kwa nyavu unaoelea kwenye maji. Uzio huo unatakiwa uruhusu maji kuingia na kutoka ili kuwezesha kuingiza hewa na kutoa uchafu.

Kuhusu utengenezaji wa vizimba inaelezwa kwamba vifaa au zana zinazotumika kutengeneza kizimba lazima ziwe imara, nyepesi, zisizopata kutu, zisizo na sumu na zinazohimili mabadiliko ya hali ya hewa. Vifaa vinavyotumika kutengeneza vizimba inaelezwa kwamba ni pamoja na nyavu, mabomba, mbao, maboya, kamba na nanga na kwamba vizimba vinaweza kutengenezwa katika umbo lolote.

Aidha, maumbo yaliyozoeleka ni mstatili, mraba au duara. Vizimba vidogo vinatoa urahisi wa kuvihudumia kuliko vizimba vikubwa. Ofisa uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Oscar Mashiranga, anasema ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba katika ziwa Victoria umeanza kueleweka kwa wananchi.

Anasema teknolojia hiyo ilianza kutolewa nchini mwaka 2016 baada ya utafiti kufanywa na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (Tafiri) wa kutafuta njia bora za ufugaji samaki.

Matokeo ya utafiti huo kwa mujibu wa Mashiranga ulionesha kuwa ufugaji samaki kwa kutumia vizimba una faida kwa sababu kizimba kimoja chenye ukubwa wa mita tano upana kwa mita tano urefu na kina cha mita nne, kina uwezo wa kufuga samaki 10,000.

Anasema samaki hao wakifugwa vizuri kila baada ya miezi sita mfugaji anavuna na kwamba kwa bei ya sasa ya jumla kilogramu moja ya samaki aina ya sato ni kati ya shilingi 5,000 hadi 7,000 hivyo mfugaji akiuza samaki hata nusu ya hao 10,000 bado anapata faida nzuri.

“Ufugaji samaki kwenye vizimba katika Ziwa Victoria una matokeo mazuri, wafugaji walioanza kufuga wanapata faida kwa sababu eneo dogo linafuga samaki wengi,” anasema Mashiranga.

Akizungumzia eneo linalofaa kuweka vizimba, anasema ni muhimu liwe na vigezo vifuatavyo: Kina cha maji kati ya vizimba na sakafu ya ziwa isiwe chini ya mita tano; kuwe na mkondo wa maji wa kiasi; lisiwe eneo la wazi ambapo upepo unavuma kwa kasi kwani unaweza kuzoa vizimba; vizimba viwekwe maeneo yanayofikika kirahisi kuwezesha utoaji wa huduma, ulishaji na matengenezo mengine; Lisiwe eneo ambalo ni njia ya vyombo vya usafiri vya kwenye maji; lisiwe eneo linalotumika kwa shughuli za uvuvi na lisiwe eneo la mazalia ya samaki.

Anasema baada ya teknolojia hiyo kuanzishwa nchini mwaka 2016 elimu ilianza kutolewa kwa wafugaji waliokuwa wakifuga kwa kutumia mabwawa na baadhi waliona fursa na kuamua kuanzisha vizimba kwa ushirikiano na Idara hiyo ambapo mwaka huo, jumla ya vizimba 109 vilijengwa.

Ndani ya miaka minne sasa anasema kuna jumla ya vizimba 431 vilivyojengwa na vinafanya kazi vikimilikiwa na wafugaji 28 walio kwenye ziwa hilo.

“Ufugaji wa samaki kwa vizimba ni njia mpya na yenye tija kwa sababu ya mazao mengi yanayozalishwa, ingawa mwanzo kuna gharama za kuanzisha mradi huo lakini faida nzuri huanza kuonekana kwenye mavuno ya pili na kuendelea,” anabainisha Mashiranga.

Aki zungumza na wananchi waliotembelea banda hilo kujionea ufugaji samaki na uzalishaji vifaranga wa samaki, Mashiranga anawashauri kujiunga kwenye vikundi na kuanzisha vizimba vya ufugaji bora wa samaki.

Elinsa Massawe ni Ofisa Uvuvi Mwandamizi ambaye pia ni Msimamizi wa Idara ya Ukuzaji viumbe maji wa wizara hiyo mkoani Mwanza.

Yeye anasema pamoja na wananchi kuelimishwa umuhimu wa kufuga samaki kwa kutumia vizimba, bado mwamko ni mdogo huku baadhi ya wafugaji wakiona ni gharama kubwa kuanzisha mradi wa aina hiyo.

Massawe anasema ufugaji samaki kwa ku tumia vizimba ndio ufugaji bora na wa kisasa zaidi kwa sababu eneo dogo linazalisha samaki wengi na kwamba masuala ya gharama kwa mwanzo wa mradi ni jambo lisilokwepeka.

Gharama za kuanzisha ufugaji huo kwa kizimba kimoja kwa mujibu wa mchanganuo uliowekwa ni Sh milioni 20 ambazo zinahusisha vifaranga 10,000, na gharama za ujenzi na vibali vyote muhimu.

Massawe anashauri wafugaji wanaopenda kuanza ufugaji kwa njia hiyo waungane kwenye vikundi na kupata nguvu ya kuanzisha kizimba kimoja kisha wataendelea kuongeza vingine kadri wanavyokua kibiashara na kujipatia faida.

Massawe anawashauri wananchi wanaoshiriki kwenye maonesho hayo kutembelea banda la wizara hiyo, sekta ya uvuvi ili kupata elimu itakayobadilisha maisha yao na kuyaboresha kwa kufuga samaki kisasa na kwenye eneo dogo.

Joseph Mabula, mkazi wa Ukerewe mkoani Mwanza alitembelea maonesho hayo na kujifunza jinsi ya kuboresha ufugaji wa samaki na kusema amepata elimu na kutamani kuanza ufugaji wa njia hiyo.

Hata hivyo, anasema ataenda kujipanga na kushawishi wengine ili wajiunge kwenye kikundi na kuanzisha mradi huo.

“Nimetembelea maonesho haya kwa sababu ninajua nitarudi nyumbani na kitu cha maana kichwani, na kwa kweli kwenye sekta hii nimejifunza ufugaji wa samaki na nitaenda kuanza kwa kushirikiana na wenzangu kwa kuwa eneo ninaloishi ni pembezoni mwa Ziwa Victoria.

TANZANIA imeridhia mikataba na matamko mbalimbali ya kimataifa yanayotoa haki ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi