loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wanawake wenye ulemavu wanavyofungiwa nje ya uongozi

OKTOBA 28, 2020 Tanzania itafanya Uchaguzi Mkuu kuchagua rais, wabunge na madiwani ukiwa ni uchaguzi wa sita katika mfumo wa siasa wa vyama vingi.

Vyama mbalimbali vya siasa ambavyo ni mhimili mkubwa wa demokrasia shirikishi na ya ushindani, vipo katika hatua mbalimbali za kupata wagombea watakaoviwakilisha kwa ngazi mbalimbali kufika mbele ya wananchi ambao ni wapigakura na kuomba ridhaa.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977), Ibara ya 39 (1) (c), vyama vya siasa ni walinzi wa lango kuu la kuingilia katika kinyang’anyiro cha uchaguzi kwani inamtaka kila anayewania uongozi, kupendekezwa na chama cha siasa.

Kwa msingi huo, vyama vina uwezo mkubwa wa kuamua nani aingie kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi na nani atolewe, vile vile ikibidi, nani ashinde; ama mwanaume au mwanamke, mwenye ulemavu, au asiye na ulemavu.

Hata hivyo, wanawake ambao ndio wapigakura wengi, wamekuwa wakijitokeza kwa wingi katika mikutano ya kampeni na katika upigaji kura, lakini kwa uchache, wanashiriki kwa kiwango kidogo katika kugombea, kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa viongozi.

Hii ni kutokana na kukumbana na vigingi mbalimbali vinavyowafungia nje ya uongozi na matokeo yake, ama wanabaki kuwa watazamaji, au wasindikizaji wa wanaume kwenda kushinda katika uchaguzi au kuteuliwa.

Mwezeshaji katika mafunzo ya hivi karibuni yaliyofanyika jijini Dar es Salaam chini ya mradi wa ‘Wanawake Sasa’ unaofadhiliwa na taasisi ya African Women Development Fund (AWDF), Mary Mwita, anasema katika mchakato wa uchaguzi wa kisiasa, wanawake wanakumbwa na changamoto nyingi.

Washiriki katika mafunzo hayo chini ya mradi huu unaolenga kuhamasisha na kuchochea ushiriki kamilifu wa wanawake katika masuala ya siasa, uchaguzi na hata katika ngazi mbalimbalI za maamuzi, walikuwa wanahabari kutoka Arusha, Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar. Mary, ambaye ni wakili, anazitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na wengine kudaiwa rushwa ya ngono ili ‘wavushwe’ katika hatua mbalimbali, ukosefu wa rasilimali fedha kwa ajili ya kufuatilia taratibu mbalimbali na kuwafikia wapigakura, pamoja na mila na desturi za baadhi ya makabila kumtambua mwanamke kama pekee mwenye jukumu la kulea familia hasa suala la mapishi na kuangalia watoto.

Anasema kingine kinachowafungia wanawake nje ya ushiriki kamilifu wa mchakato wa uchaguzi wa kisiasa, ni wanawake wenyewe kukatishana tamaa na kutoungana mkono wakiamini kuwa mwanamke ni dhaifu katika uongozi na hali ikiwa mbaya zaidi kwa wanawake wenye ulemavu. Anasema:

“Waandishi wa habari, na nyie msiruhusu vyombo vyenu vitumike kudhalilisha wanawake na wenye ulemavu na kuwakatisha tamaa katika mchakato huu.” Katibu Mkuu wa Sauti ya Wanawake wenye Ulemavu Tanzania (Swauta), Stella Jailos yeye anakwenda mbali na kusema, katika mchakato wa uchaguzi wa kisiasa na uongozi, wanawake wanakumbana na vigingi vingi, lakini wanawake wenye ulemavu wanakumbwa na vigingi vingi zaidi.

Jailos mwenye ulemavu wa kutokuona anasema, vigingi vinavyowatesa wanawake wenye ulemavu na kuwafungia nje ya ushiriki kamilifu wa mchakato wa uchaguzi wa kisiasa ni pamoja na Katiba ya nchi na hata vyama vya siasa kutokuwa na agizo maalumu la kuwapo viti maalumu kwa ajili ya wanawake wenye ulemavu katika ngazi ya ubunge na udiwani hali inayofanya wachache wapate kwa huruma ya kanuni za baadhi ya vyama, lakini siyo katiba.

“Kutokana na hali hiyo, hata inapotokea mwanamke mwenye ulemavu akapata nafasi hiyo, asipowasemea wenzake wenye ulemavu, hakuna mwenye nguvu za kumhoji na kumwajibisha kwa kuwa anajiona amefika pale kwa jitihada zake mwenyewe na siyo kutumwa maana haombi kura kwa wenye ulemavu wenzake,” anasema.

Anaongeza: “Kigingi (changamoto) kingine ni kuwa, ‘movement’ (nyendo) zetu ni ngumu hivyo siyo rahisi kupitia watu mitaani kuomba kura , hivyo kura kwa mwenye ulemavu, huombea ukumbini pekee.”

Kwa mujibu wa uchunguzi wa mwandishi wa makala haya, ukosefu wa fedha kwa ajili ya vyombo vya usafiri na miundombinu mibovu, njia au barabara mbovu, milima na mabonde sambamba na umbali wa kuwafikia wapigakura, hukwamisha juhudi za wenye ulemavu hasa wa viungo, wasioona au wenye ulemavu wa ngozi kutowafikia kirahisi wapigakura kama wanavyofanya wagombea wenzao wasio na ulemavu.

Katibu Mkuu huyo wa Swauta anasema pia kuwa, katika baadhi ya makabila, bado wapo wanajamii wenye kasumba ya kutokuamini wala kutaka kuongozwa na mwanamke na kwamba, anapokuwa mwanamke mwenye ulemavu hali inazidi kuwa mbaya.

Hata hivyo, anavipongeza baadhi ya vyama vilivyoonesha nia na mfano bora wa kuwateua wanawake wenye ulemavu katika nafasi mbalimbali za uwakilishi ukiwamo wa bungeni.

“Hapa napo kuna changamoto kwamba, wengine wanapofariki kama ilivyokuwa kwa Regia Mtema (Januari 14, 2012) na Dk Elly Macha (Machi 31, 2017), nafasi zao hazikurejeshwa kwa wanawake wenye ulemavu kwa kuwa katiba hazisemi chochote kuhusu nafasi ya wanawake wenye ulemavu…” Dk Amina Mollel aliyetia nia kuomba ubunge wa viti maalumu wanawake mkoani Arusha, anasema tatizo siyo mfumo wala jamii, bali washindani wenye nguvu dhaifu wanapoona dalili za kushindwa ndio huanza kupotosha wananchi kwa vigezo vya ujinsia na maumbile. Dk Mollel anasema:

“Kwa sasa jamii imeelewa sana haya mambo; wanajali hoja na namna wanavyokufahamu kwa uadilifu na uchapakazi; suala la kuwa mwanamke mwenye ulemavu halipo kabisa isipokuwa, washindani dhaifu ndio hutumia kigezo cha mtu kuwa mwanamke au kuwa na ulemavu kutaka kupotosha watu.”

Katika mazungumzo na HabariLEO jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Polisi, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), David Misime anasema: “Wakati wa kampeni, polisi wanawajibika kulinda amani na usalama likiwamo suala la ulinzi wa wagombea na kuhakikisha kampeni zinafanyika kwa uhuru, usalama na sawa kwa wagombea wote.” Misime anaongeza:

“Ni wajibu wa kila mgombea kuwaelimisha wafuasi wake umuhimu wa amani, usalama na utulivu katika kipindi chote cha uchaguzi.” Akirejea kitabu kiitwacho: ‘Haki na Wajibu wa Mpigakura:

Ulinzi Shirikishi katika Mchakato wa Uchaguzi’ kilichotolewa na Jeshi la Polisi Tanzania mwaka 2010, SACP Misime anasema ni makosa kwa mgombea au wafuasi wake kutumia lugha ya matusi, kashfa, kejeli, ubaguzi au udhalilishaji wa kijinsia au kimaumbile dhidi ya mgombea mwingine…

” Wadau mbalimbali wanavitaka vyama vya siasa kuweka utaratibu thabiti wa kuwakemea na hata kuwaondoa kwenye kinyang’anyiro, wagombea watakaotumia lugha za matusi au udhalilishaji kwa wagombea wanawake wakiwamo wenye ulemavu wakilenga kuwakatisha tamaa na kuwadhoofisha kisiasa Ndiyo maana wadau mbalimbali wanazitaka mamlaka kupiga marufuku na kuchukua hatua dhidi matumizi ya lugha ya kashfa hasa zenye kudhalilisha wagombea wa kike/wenye ulemavu na changamoto nyingine.

Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Rose Reuben katika mazingira mbalimbali anasisitiza ushiriki wa wanawake katika mchakato wa uchaguzi wa kisiasa akisema:

“Vyama vya siasa vioneshe nia ya kweli ya kupambana na ufisadi na rushwa za aina zote ikiwamo rushwa ya ngono.” Reuben anaongeza: “Iwe marufuku kwa chama chochote kumbagua mwanachama kwa misingi ya jinsi, na maumbile yake na vyama vyote vizingatie na kuheshimu kanuni za maadili ya uchaguzi ili kujenga heshima na utu wa wagombea, hasa wanawake wakiwamo wenye ulemavu wakati wote wa uchaguzi ili kuimarisha amani na umoja wa kitaifa.”

Wadau wanasema hata katika uchaguzi wa mwaka huu, vyama vinapaswa kutoa nafasi maalumu kwa wanawake wakiwamo wanawake wenye ulemavu.

Kwa mujibu wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu na Mkataba wa Nyongeza (2006), Ibara ya 6 inayohusu wanawake wenye ulemavu, wanawake na wasichana wenye ulemavu wanakabiliwa na aina nyingi za ubaguzi, na kwa maana hiyo, zichukuliwe hatua kuhakikisha wananufaika kikamilifu na haki zote za binadamu na uhuru wa msingi. Ibara ya 29 ya Mkataba huo inasisitiza ushiriki wa wenye ulemavu katika siasa na kuhudumia umma ukisema:

“Waliouridhia Mkataba huu wanawahakikishia watu wenye ulemavu haki za kisiasa na fursa ya kunufaika na haki hizo kwa misingi ya usawa na watu wengine.”

Mkataba unazitaka nchi husika kuhakikisha kuwa, wenye ulemavu wanaweza kushiriki kikamilifu katika medani ya siasa na huduma kwa umma kwa misingi iliyo sawa na wengine moja kwa moja au kwa kupitia wawakilishi waliochaguliwa kwa misingi huru sambamba na fursa ya wenye ulemavu kupiga kura na kuchaguliwa.

Mkataba unataka kuwapo utaratibu wa kupiga kura na kuhakikisha vifaa na nyenzo ni sadifu, vinafikika, na vinaeleweka na kutumika kwa urahisi na pia kuwapo na kulindwa kwa haki ya watu wenye ulemavu kupiga kura kwa siri wakati wa uchaguzi na bila kudhalilishwa, na kugombea, kuchukua dhamana za uongozi.

Wadau wanataka uwepo utaratibu wa kikatiba unaotoa nafasi maalumu kwa kundi la wanawake wenye ulemavu kuchaguana wenyewe katika jamii yao kama ilivyo kwa makudi mengine ya viti maalumu likiwamo la wafanyakazi.

TANZANIA imeridhia mikataba na matamko mbalimbali ya kimataifa yanayotoa haki ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi