loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wiwanda vya kahawa vyapewa ushauri

KATIBU Tawala Mkoa wa Kagera, Profesa Faustine Kamuzora, amewaomba wamiliki wa viwanda vinavyosaga na kukoboa kahawa kuanzisha migahawa ya kunywa na kuuza kinywaji hicho ili kuhamasisha soko la ndani.

Profesa Kamuzora alitoa rai hiyo alipotembelea kiwanda cha uzalishaji wa kahawa ya unga cha Amimuza kilichopo manispaa ya Bukoba kwa ajili ya kujionea uzalishaji wa kahawa yenye ladha tofauti.

Alisema nchini ni asilimia saba tu ya Watanzania wenye mazoea ya kunywa kahawa, ambapo mkoa wa Kagera unazalisha kahawa nyingi lakini ukiwa na watumiaji wachache zaidi.

"Mara nyingi utakuta viwanda vinalalamika kuwa kahawa haisafirishwi, changamoto za mipaka baada ya covid-19, lakini kama walau tungekuwa na soko linalofikia asilimia 50 la ndani, huenda hata malalamiko yasingekuwapo, hivyo wamiliki wa kiwanda wanaosafirisha kahawa nje wajenge migahawa ya kuhamasisha kunywa kahawa nchini."

“Nimetembelea nchi nyingi duniani, lakini hakuna sehemu iliyoandikwa kuwa kahawa isitumiwe na mtu yeyote au italeta maradhi ya moyo, alisema Profesa Kamuzora. Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Amri Hamza, alisema kwa sasa kinafanyiwa upanuzi ambao ukikamilika kitatoa ajira 200 za kudumu na 1,000 za muda.

Alisema kiwanda hicho kinauza kahawa yake katika nchi 36 duniani na kimeomba kuuza katika nchi nyingine sita ili kutangaza ubora wa kahawa ya Tanzania.

Hamza alitaja changamoto mbalimbali zinazokabili kiwanda hicho kuwa ni pamoja na upanuzi wa kiwanda kusimama kutokana na uhaba wa mtaji, benki kukopesha kwa riba kubwa na vifungashio kutofika kwa wakati kutoka nchi za Ulaya.

Kiwanda icho kikikamilika kinatarajia kusindika kahawa ya unga tani 33,000 na kuendelea kutoa ajira zaidi ya 1,000, ambapo kwa sasa kinatoa ajira za kudumu 42 na za muda 200.

foto
Mwandishi: Diana Deus, Bukoba

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi