loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

DAS aja na mkakati wa elimu ya Uchaguzi Mkuu

KATIBU Tawala wa Wilaya Ndogo ya Kisiwa cha Tumbatu Mkoa wa Kaskazini Unguja, Khatib Habib amesema wataitumia Redio Jamii ya Tumbatu iliyopo katika kisiwa hicho kwa ajili ya kujenga mshikamano na kuwapatia wananchi elimu ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ili kujiepusha na uvunjifu wa amani.

Habib amesema hayo wakati akizungumza na HabariLEO kuhusu matumizi ya Redio jamii iliyopo katika kisiwa hicho na matayarisho ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28 mwaka huu.

Amesema kisiwa cha Tumbatu chenye wakazi takriban 5,000 wapo wafuasi wa vyama viwili vya siasa CCM na ACT-Wazalendo ambapo katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu joto la kisiasa huongezeka kupanda na wakati mwingine wananchi kupandwa na jazba za chuki na kuhatarisha uvunjifu wa amani.

Amesema tayari wafanyakazi wa redio hiyo wameanza kutayarisha vipindi mbalimbali vyenye kujenga mshikamano, amani na upendo kwa wananchi wake.

“Tunayo redio jamii katika kisiwa cha Tumbatu kwa ajili ya kuwapatia wananchi elimu ya matukio mbalimbali ikiwemo kilimo na njia za uvuvi bora unaozingatia mazingira, hivi sasa redio yetu itajikita zaidi kuwapatia wananchi elimu ya uchaguzi na kujenga mazingira ya uvumilivu wa kisiasa,”amesema.

Ofisa mtayarishaji wa vipindi katika Redio jamii ya Tumbatu, Ali Iddi amesema tayari wamekamilisha jumla ya vipindi 10 ambavyo vitakuwa vikitolewa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu ambavyo vimejikita katika kutoa elimu na kusisitiza amani na utulivu.

“Vipindi vyetu tulivyotayarisha vyote vimejikita katika  kutoa elimu ya uchaguzi na kuwataka wananchi kuepuka na siasa za chuki na jazba katika kipindi cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu,”amesema.

Sheha wa Shehia ya Tumbatu Jongowe, Miza Ali Sharif alisema matumizi ya redio jamii kwa kiasi kikubwa yatasaidia kupunguza joto la kisiasa ambalo katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu huongezeka kiasi cha kutishia uvunjifu wa amani.

MGOMBEA Urais kwa tiketi ...

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman, Zanzibar

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi