loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ulinzi wa misitu Tao la Mashariki sasa kufanywa kielektroniki

TAO la Mashariki ni safu ya milima ya kale iliyofunikwa na misitu yenye unyevu pamoja na mbuga katika nchi za Tanzania na Kenya ya kusini mashariki.

Wanasayasi wanaamini kwamba, misitu ya Milima ya Tao la Mashariki imekuwepo kwa zaidi ya miaka milioni 30.

Tao la Mashariki linaunganisha milima (vilele) 13, na linakadiriwa kuchukuwa eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 23,000 ambapo kilometa za mraba takribani 4,000 ni misitu ya kitropiki, yenye bayoanuai kubwa.

Maelfu ya aina mbalimbali za mimea na wanyama wanapatikana katika misitu hii pekee na si mahali pengine duniani.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), Dk Revocatus Mushumbusi anabainisha  haya alipofungua kikao-kazi cha wadau kilicholenga kutoa mapendekezo ya kuboresha mfumo wa kielektroniki katika kutoa taarifa za uhalifu wa misitu iliyopo kwenye milima ya tao hilo.

Dk Mushumbusi anafafanua kwamba ndani ya misitu hiyo kuna aina zaidi ya 100 viumbe kama ndege, mamalia (wanyama wanaonyoyesha), wanyama jamii ya vyura na nyoka na mijusi.

Kaimu mkurugenzi huyo mkuu wa Tafori anazidi kubainisha pia kwamba kuna aina kama 800 za mimea na idadi kubwa ya viumbe wadogo wadogo kama vipepeo, nyuki na jamii ya majongoo.

Anasema hapa nchini, milima ya Tao la Mashariki inajumuisha maeneo ya Pare Kusini/Kaskazini (wilaya za Same na Mwanga) na Usambara Magharibi na Mashariki (Wilaya za Muheza, Lushoto na Korogwe).

Maeneo mengine ni Nguu (Wilaya ya Kilindi), Nguru (Wilaya ya Mvomero ) na Uluguru (Wilaya za Morogoro na Mvomero).

Pia tao hilo linahusisha aneo la Ukaguru (Wilaya za Gairo na Kilosa), Rubeho (Wilaya za Mpwapwa na Kilosa), Malundwe (Wilaya ya Morogoro), Udzungwa (Wilaya za Kilombero, Mufundi na Kilolo) na Mahenge (Wilaya ya Ulanga).

Dk Mushumbusi anasema maeneo mengi ya misitu yamepotea ndani ya kipindi cha miaka 100 kwa sababu ya upanuzi wa maeneo ya kilimo, ukataji miti ovyo na uchomaji moto.

Anasema eneo kubwa la Misitu ya Milima ya Tao la Mashariki lipo chini ya uhifadhi wa serikali kuu na halmashauri za wilaya lakini kutokana na upungufu wa rasilimali fedha na watu shughuli za uhifadhi wa eneo hilo umekuwa haufanyiki ipasavyo.

Dk Mushumbusi anasema juhudi mbalimbali zimefanywa na serikali pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuhifadhi maeneo haya kutokana na umuhimu wake kwa taifa.

Katika azma hiyo ya uhifadhi anasema, baadhi ya maeneo ndani ya Misitu ya Tao la Mashariki yamepandishwa hadhi na kuwa Hifadhi ya Mazingira Asili na Hifadhi ya Taifa ya wanyama kwa lengo la kuimarisha zaidi uhifadhi.

Anazitaja hifadhi hizo na maeneo yake katika mabano kuwa ni Hifadhi ya Mazingira Asili ya Chome ( Same na Mwanga), Magamba (Lushoto), Nilo (Korogwe) na Amani (Muheza na Korogwe).

Hifadhi nyingine ni Mkingu (Mvomero), Uluguru (Morogoro na Mvomero), Kilombero (Kilombero na Kilolo), pamoja  na Udzungwa Scarp (Kilombero, Kilolo na Mufindi).

“Pamoja na kupandishwa hadhi kwa  haya maeneo, bado kuna uharibifu unaofanywa ndani ya maeneo haya," anasema Dk Mushumbusi.

Anaeleza kuwa misitu iliyopo kwenye milima ya Tao la Mashariki ni muhimu kwa taifa letu hasa katika kuendeleza uchumi wa viwanda na kuboresha maisha ya wananchi.

Anafafanua kwamba zaidi ya asilimia 25 ya watanzania wanategemea misitu ya milima ya Tao la Mashariki kwenye upatikanaji wa maji katika shughuli mbalimbali za kujikimu na kipato kwani vyanzo kadhaa vya maji vinaanzia katika misitu hiyo.

Anafafanua kwamba uchumi wa viwanda unategemea zaidi maji ambayo pia yanatumika katika kuzalisha nishati ya umeme, na maji hayo yanayotoka kwenye mito mbalimbali ambayo imekuwa na manufaa makubwa kwa Taifa.

“Kwa mfano mito ya Wami, Kilombero, Ruvu, Zigi, Ruaha na Pangani yote inatiririka kutoka miinuko ya maeneo mbalimbali katika Misitu ya Milima ya Tao la Mashariki na ina manufaa makubwa kwa shughuli za kilimo kwenye maeneo ya mabondeni,” anasema Dk Mushumbusi.

Halikadhalika anasema mito ya Kilombero na Ruaha inatiririsha maji ambayo ni muhimu sana katika kuzalisha umeme  hapa nchini katika vituo vya Mtera, Kidatu, Kihansi na kwenye mradi mpya mkubwa wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere.

Dk Mushumbusi anasema hata kabla ya mradi wa Julius Nyerere, nishati ya umeme inayotumia maji kutoka misitu ya Milima ya Tao la Mashariki imekuwa ikichangia takribani asilimia 50 ya nishati ya umeme wa Taifa.

"Ili nchi kujihakikishia umeme wa uhakika na kushusha gharama za umeme nchini, Serikali ya awamu ya tano ya Rais Dk John Magufuli imeamua kutekeleza mradi wa uzalishaji umeme katika Mto Rufiji unaotarajia kuzalisha umeme wa megawati 2,115.

Anasema katika kutimiza azma hiyo ya Serikali ya Awamu ya Tano na kufanya upatikanaji wa maji kuwa endelevu uhifadhi wa Milima ya Tao la Mashariki unazidi kuwa na umuhimu mkubwa, vinginevyo bwawa letu hilo litakosa maji ya kutosha.

Dk Mushumbusi anasema mito ya Kilombero na Ruaha inatiririsha maji ambayo ni muhimu katika kuzalisha umeme hapa nchini katika vituo vya Mtera, Kidatu, Kihansi na sasa kwenye mradi mpya wa Julius Nyerere.

Hata hivyo, anasema pamoja na manufaa yote haya, Misitu ya Tao la Mashariki imeendelea kukumbwa na changamoto zinazohatarisha uwepo wake.

Anasema utafiti umeonesha eneo lenye misitu katika Tao la Mashariki limepungua kutoka kilometa za mraba 18,000 ya eneo la asili hadi kilometa za mraba 4,750 katika miaka ya hivi karibuni.

Pia anasema utafiti umeonesha kuwa takribani kiasi cha asilimia 0.1 cha uoto wa tao hilo hupotea kila mwaka  kutokana na uharibifu unaohusisha upanuzi wa mashamba kwenye maeneo ya misitu, ukataji miti ovyo, uchimbaji wa madini na uchomaji wa moto. Uanzishaji wa mashamba unatajwa kuwa sababu kubwa ya uharibifu wa misitu ya asili.

Licha ya changamoto hii, anasema serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kukabiliana uharibifu wa misitu ikiwemo kuimarisha ulinzi wake.

Mratibu wa mradi wa mfumo wa kielektroniki katika kutoa taarifa za uhalifu wa misitu iliyopo kwenye milima ya tao hilo, Dk Chelestino Balama, anasema utengenezaji wa mfumo ni miongoni mwa miradi iliyofadhiliwa na na Mfuko wa Uhifadhi wa Milima ya Tao la Mashariki katika mwaka 2019/2020.

Dk Balama anasema lengo la mfumo huo ni kusaidia jamii kutoa taarifa za uhalifu wa misitu kwa mamlaka zinazohusika ili ziweze kuchukua hatua stahiki na kwa wepesi na kwa wakati ili kupunguza athari za uhalifu katika misitu ya Tao la Mashariki.

Anasema watafiti wa Tafori walikusanya mahitaji ya mfumo huo kutoka kwa wadau, wakautengeneza, kuujaribu na kutoa mafunzo kwa baadhi ya vijiji vinavyozunguka misitu ya milima ya Tao la Mashariki.

“Mfumo huu ni wa kielektroniki kwa maana ya kutumia simu. Ni mfumo thabiti na una usiri mkubwa wa mtoa taarifa na utasaidia kudhibiti uhalifu kwenye misitu ya Tao la Mashariki," anasema.

Anaongeza: "Mfumo huu utaanza  kutumika mwaka huu wa fedha wa 2020/ 2021 kwa vile tayari mafunzo yametolewa kwa vijiji vinavyozunguka milima ya tao la Mashariki." 

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Uhifadhi wa Milima ya Tao la Mashariki, Raymond Killenga, anasema   misitu ya tao hilo ina vivutio mbalimbali, hivyo kutoa fursa kwa utalii wa ekolojia.

Pia anasema misitu hiyo inahifadhi viumbe hai ambavyo havipatikani mahali pengine duniani, hali ya hewa na mandhari nzuri iliyoko katika misitu hiyo inawezesha kilimo cha mazao mbalimbali.

Anasema, kilimo hicho kinachangia kwa kiasi kikubwa katika kulisha jamii za mijini, kuinua kipato kwa jamii za wakulima na hatimaye kupunguza umaskini wa wananchi.

Anasema Watafiti wa Tafori kupitia ufadhili wa Mfuko wa Uhifadhi wa Milima ya Tao la Mashariki (EAMCEF) walifanya utafiti uliowezesha kupatikana kwa mfumo wa kielektroniki katika kutoa taarifa za uhalifu wa misitu iliyopo kwenye milima ya tao hilo.

Katika kuunga mkono juhudi za watafiti hawa kwa upande wake, mwanakijiji cha Kining’ina, kata ya Michenga, halmashauri ya Mji wa Ifakara mkoani Morogoro, Rafael Rusau amebuni na kutengeneza jiko la oven linalotumia nishati inayotokana na malighafi ya maranda ya mbao au mpunga.

Rusau anasema ubunifu wa jiko hilo ni kwa ajili ya matumizi ya wananchi ili  kupunguza ubaribifu wa misitu inayokatwa kwa ajili ya mkaa ndani ya wilaya ya Kilombero. 

Mbunifu huyo ni mara yake ya kwanza kuonesha teknolojia hiyo rahisi kwenye  maonesho ya wakulima, wafugaji na wavuvi ya mwaka huu katika viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwa kwenye Banda la Halmashauri ya Mji wa Ifakara.

Rusau anasema mbali na uchomaji mkaa kuhatarisha uwepo wa misitu lakini umekuwa pia ukipatikana kwa gharama kubwa ambayo wananchi wa vipato vya chini vijijini na mijini hawamudu  kununua.

Anasema kuwa jiko hilo limetengenezwa kwa kutumia chuma ngumu inayotokana na bodi za magari na kwamba linatumika kuivisha na kukausha  vyakula kama wali, karanga, maharage, viazi, ndizi, ugali, samaki na dagaa na vyakula vingine vya aina mbalimbali.

 “Nimebuni na kutengeneza jiko hilo si kupata faida tu bali kusaidia taifa katika utunzaji wa misitu na kuboresha mazingira," anasema Rusau.

Mbunifu huyo anasema malighafi ya maranda ya mbao na pumba za mpunga zinapatikana kwa wingi katika halmashauri mbalimbali za mkoa wa Morogoro kutokana na kilimo cha mpunga na uwepo wa viwanda vya mbao.

Anasema, bado uzalishaji wa majiko hayo ni mdogo kutokana na kukosa mtaji wa kutosha. Anaamini kwamba endapo taasisi na wadau mbalimbali watajitokeza ku msaidia ataweza kutengeneza majiko hayo kwa wingi zaidi ili kusaidia kulinda  misitu.

Licha ya jiko hilo, pia alibuni na kutengeneza ndoo za kunawa mikono  kwa njia ya kukanyaga na miguu, akabuni na kutengeneza zana za kilimo za kufyekea majani kwa kutumia bomba za chuma zinazotokana na malighafi ya vyuma vya chakavu.

 

 

SIGARA ina kemikali zaidi ya 4,000 ...

foto
Mwandishi: John Nditi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi