loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mitaji yamiminika kutoka ughaibuni

TANZANIA imeimarisha uhusiano na nchi mbalimbali duniani, hatua inayoibeba kiuchumi, kijamii kutokana na mataifa husika kuelekeza mitaji ya uwekezaji na fursa nyingine ikiwamo ongezeko la watalii nchini.  

Taarifa ya Kituo cha Uwekezaji (TIC) inaonesha katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano, miradi yenye uwekezaji kutoka nje iliendelea kuboreka, hatua inayotokana na imani kubwa kwa wawekezaji katika juhudi za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini. 

Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Dk Maduhu Isaac alisema utafiti wa mwenendo wa mitaji ya uwekezaji kutoka nje wanaofanya kwa kushirikiana na Benki Kuu (BoT) na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, unaonesha kuwapo kwa mwenendo chanya wa uingiaji wa mitaji hasa katika sekta za uzalishaji viwandani, taasisi za fedha na bima, madini na sekta ya mawasiliano.

“Mwenendo huu wa uingaji wa mitaji kutoka nje umechangiwa na jitihada za uwekezaji katika miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuboresha mazingira ya uwekezaji,” alisema Dk Maduhu akizungumzia mafanikio ya kituo katika miaka mitano ya serikali chini ya Rais John Magufuli. 

Miradi inayovuta mitaji kutoka nje ni pamoja na wa ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme wa maji la Julius Nyerere unaotarajiwa kuzalisha Megawati 2115, Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), upanuzi wa bandari, kufufuliwa kwa Shirika la Ndege, kusambaza umeme nchini pamoja na kuboresha viwanja vya ndege. 

Taarifa ya TIC inaonesha kati ya miradi 1,312 iliyosajiliwa ndani ya miaka mitano, miradi 571 sawa na asilimia 43 ni ya wawekezaji wa kigeni; miradi 376 sawa na asilimia 29 ni ya ubia baina ya Watanzania na wageni kutoka nchi za nje na miradi 365 sawa na asilimia 28 ni ya wawekezaji wa ndani.

TIC kwa kushirikiana na ofisi za balozi zilizoko nje, imefanikiwa kuhamasisha kuvutia uwekezaji  na katika miaka mitano, kituo kimepokea wawekezaji wanaotafuta fursa mbalimbali za uwekezaji kutoka Thailand, India, Misri, Indonesia, Singapore, Italia, Iran, China, Vietnam, Marekani na Ujerumani. 

Nchi nyingine ni Poland, Korea, Czech, Uingereza, Oman, Uturuki, Kenya, Malaysia, Hongkong, Ethiopia, Uganda, Pakistani, Urusi, Ukraine, Belarus, Sudan, Japan, Ghana, Canada, Syria, Tunisia na Afrika Kusini.

Akipokea nakala ya hati ya utambulisho kutoka kwa Balozi wa Marekani, Dk Donald John Wright hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi alisema jumla ya miradi 3,179 ya wawekezaji kutoka Marekani ipo nchini na imetengeneza ajira 550,000. 

Waziri Kabudi alisema pia mauzo ya bidhaa Marekani yanaongezeka mwaka hadi mwaka huku mwaka jana ikiwa imeuza bidhaa zenye thamani ya Sh bilioni 119.

Alipowasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara  ya  wizara yake, Waziri Kabudi alieleza ushirikiano na nchi katika kanda mbalimbali duniani unavyovyoleta manufaa  kiuchumi na kijamii kwa kutaja nchi mbalimbali.

Utalii

Fursa nyingine zinazochagizwa na ushirikiano na mataifa mengine ni ongezeko la watalii. Kwa mujibu wa Bodi ya Utalii (TTB), lipo ongezeka la asilimia 32 kutoka jumla ya watalii wa kimataifa 1,137,182 (2015) hadi watalii 1,505,702 (2018). 

TTB katika taarifa yake inasema inashirikisha balozi za Tanzania zilizoko nje kuweka mikakati ya kutangaza utalii  na  Juni 9 mwaka huu ilifanya mkutano mtandaoni na mabalozi katika nchi za ukanda wa Asia na Australasia. Itafanya mikutano pia na mabalozi wa Marekani, Ulaya na Afrika. 

Waziri Kabudi katika hotuba yake bungeni , kuanzia mwaka 2015 hadi 2018, watalii 5,234,448 kutoka nchi za Afrika, Ulaya, Amerika ya Kaskazini, Asia, Mashariki ya Kati; Australia na nchi za Karibeani walitembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini. 

Oktoba na Desemba mwaka jana, wizara iliratibu ujio wa watalii 2,000 kutoka Israel na Julai iliratibu mapokezi ya watalii 120 kutoka Hong Kong, China waliotembelea mbuga za wanyama za Serengeti na Ngorongoro.

Akizungumza na HabariLeo, Balozi wa Tanzania nchini Israel, Job Masima, alisema Tanzania inashika namba ya tano kwa kwa vituo pendwa vya watalii wanaotoka nchi hiyo ya Mashariki ya Kati. 

Akielezea uhusiano mzuri uliopo, Balozi Masima alisema Serikali ya Israel ina utaratibu wa kutoa tahadhari kwa raia wake dhidi ya nchi na maeneo hatari kwa raia lakini katika orodha ya mwisho iliyohusisha nchi 45 , Tanzania haikuwemo. 

Akihojiwa na redio ya Dodoma FM juzi, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi alisema Tanzania inaongoza kupokea na kuvutia wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali. Gazeti hili pia lilimnukuu akieleza Tanzania inavyoendelea kuaminika kimataifa na kufunguka kiuchumi. 

MGOMBEA Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi