loader
Dstv Habarileo  Mobile
Serikali yahakikishia wakulima neema

Serikali yahakikishia wakulima neema

SERIKALI imeeleza inavyotambua mchango wa wakulima, wafugaji na wavuvi katika ujenzi wa taifa na ustawi wa Wanzania ikiahidi kuendelea kuwaunga mkono kwa kushughulikia changamoto zao ili kuongeza tija.

Msimamo huo ulitolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyekuwa mgeni rasmi katika sherehe za Wakulima Nanenane ambazo kitaifa zlifanyika mkoani Simiyu huku kauli mbiu ya sherehe hizo mwaka huu ikiwa ni: Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Chagua Viongozi Bora 2020.

Majaliwa alimwakilisha Rais John Magufuli ambako alisema nchi inahitaji viongozi watakaokuwa chachu ya kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kuinua ustawi wa maisha ya wakulima, wafugaji na wavuvi.

Katika hotuba yake, Waziri Mkuu alisema, kilimo ni mhimili muhimu katika maendeleo ya uchumi wa taifa na katika kipindi cha miaka mitano, Pato la Taifa linalotokana na kilimo, kwa kutumia bei za 2015 limeongezeka kwa asilimia 17 kutoka Sh trilioni 25.2 mwaka 2015 hadi Sh trilioni 29.5 mwaka 2019.

“Sote tunafahamu kuwa huu ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu. Sekta za kilimo, uvuvi na ufugaji ni miongoni mwa sekta za uzalishaji ambazo maendeleo yake yanategemea kwa kiasi kikubwa uongozi bora.

Nchi yetu inahitaji viongozi watakaokuwa chachu ya kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuinua ustawi wa maisha ya wakulima, wafugaji na wavuvi,” alisema Majaliwa.

Waziri Mkuu alisema viongozi bora ni muhimu katika kuhakikisha uwekezaji kwenye kilimo, ufugaji na uvuvi unakuwa na tija, unazingatia matumizi ya teknolojia za kisasa na kuongeza thamani ya mazao kwa kuzalisha bidhaa kupitia viwanda vidogo, vya kati na vikubwa. Alisema mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi ni malighafi muhimu kwenye viwanda na huchangia asilimia 65 ya malighafi zinazohitajika viwandani.

Sekta za kilimo, mifugo na uvuvi zimeendelea kutoa fursa nyingi za ajira kuliko sekta zote na asilimia 58 ya Watanzania wameajiriwa na kujiajiri katika sekta hizo. Alihakikishia umma kwamba nchi ina chakula cha kutosha ikijitosheleza kwa wastani wa asilimia 121 kutokana na uzalishaji wa mazao ya chakula kuendelea kuimarika.

Alisema serikali inao uhakika wa chakula cha kutosha na maeneo yote yanayohifadhi chakula yameihakikishia juu ya hilo. Alisema NFRA imehakikishia serikali kwamba nchi ina akiba ya kutosha ya chakula.

“Mazao ya chakula, uzalishaji unaendelea kuimarika hivyo kuwezesha nchi kujitosheleza kwa chakula kwa wastani wa asilimia 121. Bado nchi ina chakula cha kutosha,” alisema.

Wakati huo huo, majaliwa aliwataka wananchi wote kushiriki kwenye mikutano ya kampeni kusikiliza sera za wagombea na kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi kwa lengo la kuchagua viongozi bora kama kauli mbiu ya Nanenane mwaka huu inavyosema.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Magufuli itahakikisha kuwa wananchi wote wanaendelea kuwa salama kwa kusimamia kikamilifu amani, utulivu, umoja, undugu na ushirikiano wa Watanzania uliojengwa tangu kuanzishwa kwa taifa.

Kadhalika, Waziri Mkuu alitoa mwito kwa wanasiasa wote nchini wakati wa kufanya kampeni utakapofika wafanye kampeni za kistaarabu wa waepuke matumizi ya lugha za uchochezi ambazo zinaweza kuvuruga amani na utulivu wa nchi yetu.

Alisema mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi ni malighafi muhimu kwenye viwanda nchini na sekta hizo zimeendelea kutoa fursa za ajira kuliko sekta zote asilimia 58 wameajiriwa na kujiajiri katika sekta hizo.

Wakati huo huo alisema serikali imegundua kilimo cha bustani sasa kinaleta faida kubwa na uzalishaji umeongezeka.

Alihamasisha wanachi kujikita kwenye kilimo hicho akisisitiza kuwa kina faida na mkulima hatumii nguvu.

Naye Rais Magufuli kupitia ukurasa wake wa twitter alisema: “Nawatakia heri wakulima, wafugaji na wavuvi katika sikukuu hii ya Nanenane. Serikali inatambua mchango wenu mkubwa katika ujenzi wa taifa na ustawi wa Watanzania. Tunaahidi kuendelea kuwaunga mkono na kushughulikia changamoto zenu ili kuogeza tija katika kazi zenu”.

foto
Mwandishi: Ikunda Erick, Bariadi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi