loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mimba, uzazi salama ni haki ya wanawake wenye ulemavu

“WATU wengine wakiona mwanamke mwenye ulemavu ana mimba, wanashangaa na kubeza huku wengine wakiwalaumu wanaume kuwa hawana huruma; utamsikia mtu anasema yani hata huyu nani alimpa mimba wanaume hawa jamani! Kudhani au kusema hivyo siyo sahihi.”

“Watu wenye ulemevu wakiwamo wanawake ni watu wenye mahitaji na haki zote kama walivyo wengine hivyo, nao wana haki ya kuingia katika mahusiano, kupata mimba na hata kuzaa na kuwa na familia; sijui kwanini watu wanashangaa kumwona mwanamke mwenye ulemavu ana mimba.”

Mtetezi na Mshawishi kutoka taasisi ya ADD INTERNATIONAL, Asteria Gwajima anasema hayo katika ufunguzi wa mafunzo kwa wanawake wenye ulemavu yaliyoandaliwa na Sauti ya Wanawake wenye Ulemavu Tanzania (Swauta) na kufanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa juma.

Mafunzo hayo ya siku moja yalihusisha wanawake wa Swauta wenye ulemavu wa kutokuona, viziwi, wenye ulemavu wa viungo na albino huku watafsiri wa lugha za alama kwa ajili ya viziwi wakiwa ni Olwin Mbangwa na Elisha Kulangwa.

Hatimaye Asteria anasema: “Mwanamke mwenye ulemavu ukiona mtu anakunyanyapaa hasa kutokana na hali hiyo, una haki ya kumshitaki…” Kimsingi, mazingira kama hayo yanaonesha wazi kuwa watu wenye ulemavu miongoni mwa jamii wanapoishi, wanakumbana na changamoto za kunyimwa au kupunjwa haki zao zikiwamo haki ya kuanzisha na kuwa katika mahusiano.

Katika semina hiyo, Asteria anasema mazingira mengi ya kijamii na kiuchumi waliyo nayo wanawake wenye ulemavu ukiwamo utegemezi wa kiuchumi, yanawaweka katika kipindi kigumu kwa kuwa pia husababisha kufanyiwa ukatili na ndugu (wanafamilia), lakini wakashindwa au kuogopa kutafuta haki mbele ya sheria kwa kuwa wanaweza kupoteza uhusiano wa kifamilia na wanaoishi nao na hivyo, kupata ugumu kumudu maisha.

Mshauri na Mtetezi huyo wa ADD INTERNATIONAL, anasema, hata katika kipindi cha mlipuko wa maambukizi ya virusi vya Corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu (Covid- 19), kiwango cha unyanyasaji na unyanyapaa dhidi ya wanawake wenye ulemavu kiliongezeka, lakini wengi hawakusema.

Akiwasilisha mada mintarafu Haki ya ya Uzazi kwa Wanawake na Wasichana Wenye Ulemavu, Mratibu wa Shirika la People’s Health Movement Tanzania, Godfrey Philimon, anasema kutokana na ujinga na mitazamo duni ya baadhi ya wanajamii nchini wakiwamo baadhi ya watoa huduma za afya, kumekuwa na vizuizi vingi vya wanawake wenye ulemavu kupata huduma sahihi na kwa kiwango stahiki za afya ya uzazi.

Anasema huduma za afya zilizopo siyo rafiki wa watu wenye ulemavu wakiwamo wanawake kwani mahitaji yao ya msingi katika kupata huduma hizo yamekuwa yakipuuzwa.

“Wako katika hatari kubwa ya kunyimwa haki kuanzisha mahusiano na kuamua watu wa kuanzisha nao familia na pia, wengine wanalazimishwa kuondolewa uzazi, kutoa mimba au kuingia katika ndoa wasizotaka ili wakawe walinzi wa nyumba na kutumiwa kama vyombo na siyo kuwa kama wanafamilia,” anasema.

Kwa mujibu wa mratibu huyo, ukatili dhidi ya wenye ulemavu unaongezewa na ukweli kwamba waathirika wanaweza kuwa wategemezi wa mwili au fedha kwa wale wanaowadhulumu.

Mratibu huyo wa People’s Health Movement anatoa mfano akisema, katika baadhi ya nchi zipo imani potofu kuwa kama mtu ana virusi vya ukimwi (HIV) akifanya ngono na bikira, virusi vile vitamtoka na kuhamia kwa bikira.

“Kwa kuwa wenye ulemavu wanaaminiwa kimakosa kuwa hawana nguvu au tamaa za kimwili hivyo ni bikira, mara nyingi wamekuwa hatarini kubakwa na wako hatarini mara tatu zaidi ya wasio na ulemavu kwa kuwa waathirika wa ukatili wa kijinsia ukiwamo ubakaji hasahasa wenye matatizo ya afya ya akili,” anasema Philimon.

Aprili 11, 2018 Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Stella Ikupa,alisema katika Kikao cha Saba cha Mkutano wa 11 wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma, alisema yeyote atakayebainika kufanya ubakaji kwa watu wenye ulemavu atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Katika hali kama hiyo, Philimon anasema Serikali inapaswa kuhakikisha watu wenye ulemavu wanashirikishwa katika mchakato wa uanzishwaji wa sheria ya afya kwa wote na kwa usawa nchini. Anasema:

“Hakuna chochote juu yetu bila sisi ni kanuni muhimu kwa watu wenye ulemavu. Makubaliano ya Haki za Watu wenye Ulemavu yanaonesha kanuni hii inayosisitiza umuhimu wa kushirikiana na watu wenye ulemavu katika hatua zote za maendeleo ya sera, upangaji wa mipango, na utekelezaji.”

Anasema watu wenye ulemavu hawahitaji huduma maalumu za walemavu, badala yake watafaidika kwa kuingizwa katika juhudi za afya ya kijinsia na uzazi iliyoundwa kufikia jamii kwa jumla na kwamba, popote yanapojadiliwa masuala ya afya na uzazi, ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu utaongeza ufahamu haraka.

Hata hivyo anasema, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita hadi sasa kuna maendeleo yanayopaswa kuungwa mkono na kuendelezwa kwani Tanzania inaendelea kuhakikisha uongozi wa kisiasa unatilia mkazo huduma bora za afya, utunzaji bora wa huduma , na kusisitiza ‘Wekeza zaidi, wekeza malengo bora’ hususan katika niundombinu ya afya na ugavi wa matibabu sambamba na wafanyakazi katika sekta ya afya.

“Kulingana na data kutoka kwa serikalini, tangu mwaka wa 2015 hadi 2020, zahanati 1198, vituo vya afya 884, hospitali za wilaya 71, mikoa 10 na hospitali za rufaa za kanda 3 zimejengwa.,” anasema.

Philimo anaongeza: “Wanaojifungua hospitalini wameongezeka kutoka asilimia 64 mwaka 2015 hadi asilimia 83 mwaka 2020 na ya wahamishia matibabu nje ya nchi imepungua kwa asilimia 95 wakati idadi ya wagonjwa wanaokuja Tanzania kwa wataalam wa matibabu maalumu kama ya moyo na ubongo ikioongezeka.”

Mshiriki mmoja wa mafunzo aliyefahamika kwa jina moja la Flora, anapendekeza kuwa na sera inayoruhusa mjamzito mwenye ulemavu anayekwenda kujifungua katika chumba cha kujifungulia hususan kiziwi au asiyeona, awe na mtu anayemwamini ili kumsaidia kwa mawasiliano na utambuzi wa mambo mbalimbali.

Anasema haya ni pamoja na kuona na kumtambua mtoto anayezaliwa ili kuepuka malalamiko ambayo yamekuwa yakisikika kutoka kwa baadhi ya wanawake wenye ulemavu hasa wasioona kuwa, wanaibiwa au kubakwa.

TANZANIA imeridhia mikataba na matamko mbalimbali ya kimataifa yanayotoa haki ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi