loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Huduma za afya msingi zilivyoimarika maradufu

HUDUMA bora za afya ya msingi zinapunguza uhitaji, gharama na usumbufu kwa wananchi kufuata huduma za rufaa ngazi ya mkoa.

Kwa jiografia ya nchi yetu uboreshaji wa huduma za afya msingi siyo tu kwamba zinapunguza gharama za matibabu, bali pia zinawapa watu fursa ya kuelekeza rasilimali walizonazo katika shughuli zingine za kimaendeleo.

Katika kuimarisha usimamizi na uratibu wa utoaji huduma za afya ya msingi, Serikali iliamua kuboresha dawati la uratibu na ufuatiliaji wa shughuli za afya ya msingi katika Ofisi ya Waziri Mkuu kwa wakati huo kwa kuanzisha idara kamili ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe.

Uamuzi huu umeleta ufanisi na tija katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya afya na utoaji wa huduma za afya ya msingi kwenye mamlaka za serikali za mitaa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo, anasema uratibu na usimamizi wa utoaji huduma za afya ya msingi kwa wananchi katika mamlaka za serikali za mitaa ni nguzo muhimu katika kuchochea na kuimarisha uchumi wa kati.

Anasema uratibu na usimamizi huo kwa Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za MItaa (Tamisemi) unaongozwa na kauli mbiu ya “Afya ya Msingi ni Nguzo Muhimu katika Kuimarisha Uchumi wa Kati”.

Jafo anasema katika kuhakikisha huduma za afya ya msingi zinakuwa bora na kuimarika, Ofisi ya Rais Tamisemi kupitia Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe ilianisha vipaumbele tisa vya kimkakati ambavyo ni kujenga na kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma za afya, kuimarisha upatikanaji dawa na vifaa tiba, kuimarisha mifumo ya kielekitroniki, na kuratibu na kusimamia rasilimali watu.

Vipaumbele vingine ni kuimarisha uwezo wa vituo katika kuandaa mipango na bajeti, kuimarisha uwajibikaji wa Timu za Afya za Mikoa (RHMT) na za Halmashauri, kuimarisha huduma za ustawi wa jamii, kuratibu upatikanaji wa huduma za lishe na kuimarisha ushiriki na umiliki wa jamii katika huduma za afya ya msingi.

Jafo anasema katika kipindi cha miaka mitano, Ofisi ya Rais-Tamisemi imeweza kuratibu ushiriki wa wananchi katika kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya kwa kujenga na kukarabati zahanati 1,198, vituo vya afya 487 na hospitali 99 katika halmashauri ambazo hazikuwa na hospitali.

“Ushiriki huu wa moja kwa moja wa wananchi unakadiriwa kuwa na thamani ya Sh bilioni 3.8, sawa na asilimia moja ya gharama zote zilizotumika. Gharama hizi zinahusisha nguvu kazi, ukusanyaji wa malighafi za ujenzi, utoaji maeneo ya ujenzi, usimamizi na fedha tasilimu.

“ Haya ni mafanikio ya kihistoria ambayo yametokana na utashi na utendaji wa kiuwajibikaji wa waziri mwenye dhamana ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli.”

“Ni mafanikio yanayoakisi maono ya Rais Magufuli ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya ya msingi na dharura katika mazingira rafiki na rahisi.”

Akitoa mfano, Jafo anasema wajawazito waliopata huduma ya kujifungua kwenye majengo mapya yaliyojengwa ni 219,764, kati ya hao wajawazito 18,826 walipata huduma za upasuaji wakati wagonjwa wa kawaida waliohudumiwa na kufanyiwa upasuaji walikuwa 6,022.

“Pia wazee 128,108 walihudumiwa na wagonjwa waliolazwa walikuwa 420,784, wanaume 176,169 na wanawake 244,615.” Anasema pia Ofisi ya Rais –Tamisemi imeratibu upatikanaji wa vifaa muhimu vya upimaji, upasuaji, X-ray na ultrasound katika maabara kwenye vituo vya kutolea huduma za afya 487 ili kuvipa uwezo wa kutoa huduma za msingi za dharura.

Kuhusu rasilimali watu wenye ujuzi na weledi ambao ndio msingi mkuu katika kutoa huduma za afya, Jafo anasema Ofisi ya RaisTamisemi imeratibu na kusimamia ajira za watumishi wapya wa afya 12,865, hali ambayo imechangia ubora wa huduma na kupunguza rufaa.

Kwa upande wa huduma za ustawi wa jamii, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya RaisTamisemi (anayeshughulikia afya), Dk Doroth Gwajima, anasema katika miaka mitano huduma hizo zimeendelea kutolewa kwa kulenga familia/watoto, malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya watoto wadogo, marekebisho ya tabia na haki za mtoto kisheria, huduma kwa watu wenye elemavu na wazee.

“ Utoaji wa huduma za ustawi wa jamii umeimarishwa kwa kutumia mifumo ya utoaji wa taarifa ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, jambo ambalo limesaidia upatikanaji wa takwimu sahihi za watoto na kuwaunganisha na huduma za msingi,” anasema.

Anasema katika kipindi hicho, watoto 1,495,047 wamefikiwa, watoto wa kiume wakiwa 770,944 na wa kike 724,105 huku watoto 139,515, miongoni mwa hao, wa wakiume 116,036 na wa kike 23,479 waliokuwa wanatumia dawa za kulevya walihudumiwa pia.

“Halikadhalika, watu wenye ulemavu 405,426 wametambuliwa, wanawake wakiwa 191,116 na wanaume 214,220 na kamati za watu wenye ulemavu zimeundwa katika vijiji 6024, mitaa 2284 na halmashauri 140, wakati mabaraza ya wazee yalioundwa ni 6,844.” Dk Gwajima anaongeza:

“Mikopo isiyo na riba yenye thamani ya shilingi 2,102,654 imetolewa kwa vikundi 582 vya watu wenye ulemavu huku wazee 1,850,622 wakitambuliwa, kati ya hao wazee 898,753 wamepatiwa vitambulisho na wenye kadi za bima za afya NHIF/ CHF ni 684,383.

Kuhusu utekelezaji wa mfuko wa jamii ulioboreshwa-iCHF ulioanza Julai 2018, Dk Gwajima anasema wananchi milioni 9.2 wamenufaika hadi kufikia Juni, 2020.

Anasema Sh bilioni 22.5 zimekusanywa na kuwawezesha kupata matibabu kuanzia ngazi za zahanati hadi hospitali za halmashauri na za mikoa na hata vnje ya maeneo waliyojiandikisha kwa kufuata utaratibu wa rufaa.

Aidha, Dk Gwajima anasema mamlaka za serikali za mitaa kwa kushirikiana na wadau wa lishe zimeweza kupunguza udumavu kwa watoto walio chini ya miaka mitano kutoka asilimia 34.8 mwaka 2015 hadi asilimia 31.8 mwaka 2018.

“ Haya yamefanikiwa baada ya Serikali kuweka utaratibu unaowahusisha wakuu wa mikoa kuwajibika moja kwa maja kusimamia shughuli za lishe kwa kuwekeana mkataba kati ya waziri na wakuu wa mikoa.

Kumekuwa na ongezeko la bajeti ya lishe katika halmashauri kutoka shilingi bilioni 11 mwaka 2015 hadi shilingi billioni 16.7 mwaka 2019. Katibu Mkuu, Joseph Nyamhanga anasema katika kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa vituo vya kutolea huduma za afya, Ofisi ya Rais –Tamisemi imeanzisha, kusimamia na kuratibu mifumo ya kielektroniki inayolenga kuimarisha uandaaji wa mipango na bajeti, ukusanyaji wa mapato, takwimu na matumizi.

Baadhi ya mifumo hiyo ni Planrep iliyoboreshwa, FFARS, na GoTHOMIS. Katika kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinapatikana wakati wote katika vituo vya kutolea huduma za afya, Nyamhanga anasema umeanzishwa mfumo wa mshitiri katika mikoa yote 26 ambao umeviwezesha vituo kupata mahitaji ya vifaa, vifaa tiba, dawa na vitendanishi kutoka kwa wauzaji binafsi walioteuliwa katika mkoa husika pindi mahitaji yanapokosekana katika Bohari Kuu ya Dawa (MSD).

Hii ni sambamba na mpango wa uanzishwaji wa maduka ya dawa katika hospitali za halmashauri, na kwamba hadi kufikia Juni 30, 2020, halmashauri 88 zilikuwa zimeishafungua maduka ya dawa.

“ Usimamizi mahiri na utekelezaji wa mipango iliyowekwa imewezesha upatikanaji wa dawa muhimu katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa zaidi ya asilimia 90 na kuchochea uwajibikaji katika ununuzi na matumizi ya dawa kwa kuziba mianya ya udanganyifu, udokozi na wizi wa dawa,” anasema.

Nyamhanga anasema wameweza pia kugatua madaraka ya uendeshaji, kutoka halmashauri kwenda kwenye ngazi ya vituo vya kutolea huduma za afya kwa kuvifanya vituo kupanga mipango na bajeti na upelekeji wa fedha moja kwa moja kwenye vituo.

Anasema tangu kuanza kwa utaratibu huu mwaka 2017, zaidi ya Sh bilioni 599. 675 zimepelekwa moja kwa moja kwenye vituo vya kutolea huduma za afya msingi 5,538, kati ya hizo zaidi ya Sh bilioni 212.922 ni ruzuku ya uendeshaji na zaidi ya Sh bilioni 386.753 ni fedha za maendeleo.

“ Utaratibu huu umeongeza ufanisi, uwajibikaji, ushiriki wa wananchi katika kumiliki na kusimamia vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi kwa kushiriki katika uandaaji wa vipaumbele na mipango ya vituo, kusimamia huduma za afya katika maeneo yao kupitia Bodi na Kamati za usimamizi za vituo vya kutolea huduma za afya,” anasema.

UJENZI wa mfereji wa Suez nchini Misri ulioanza mwaka 1859 ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi