loader
Dstv Habarileo  Mobile
Majaliwa acharuka Majaliwa acharuka bima za wanafunzi

Majaliwa acharuka Majaliwa acharuka bima za wanafunzi

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wiki moja kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kukutana na wakuu wa vyuo vikuu kubaini vyuo ambavyo vimeshindwa kuwasilisha michango ya wanafunzi katika Mfuko wa Taifa Bima ya Afya (NHIF) licha ya wanafunzi kulipa fedha hizo.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Kwanza kwa mwaka 2019/2020 wa Jumuiya ya Wanafunzi Taasisi ya Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO).

“Katibu Mkuu Wizara ya Elimu kashughulikie jambo hili tujue mifumo wanayotumia, pia nataka kujua ni wanafunzi wangapi ambao wamelipa na hawajapewa vitambulisho na kwa nini na nani amesababisha haya na hatua alizochukuliwa.

"Taarifa hiyo nataka niipate tarehe 16 mwezi huu, wiki moja inakutosha,”alisema Majaliwa.

Alitoa agizo hilo baada ya Mwenyekiti TAHLISO, Peter Niboye kumwomba asaidie kutatua tatizo hilo kwa kuruhusu wanafunzi hao kulipa moja kwa moja fedha NHIF badala ya kupitisha vyuoni ambako zimekuwa zikicheleweshwa kufikishwa kwenye mfuko huo.

Majaliwa alimuagiza Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Anamaria Semakafu aliyemwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako kufikisha taarifa hiyo.

Alihoji kama mwanafunzi analipa ada na fedha za kulipa bima Sh 50,400 zipo ndani yake, inakuwaje fedha hizo hazifiki kwa wakati NHIF ili kupata vitambulisho kwa ajili ya kupata huduma ya afya.

Aliiagiza Wizara ya Elimu isimamie suala hilo kwa kufanya kikao na wakuu wa vyuo vinavyolalamikiwa.

Alisema katika taarifa atakayopelekewa na Wizara inatakiwa kuonesha ni vyuo gani, wanafunzi wangapi hawana kadi za bima na kiasi gani cha fedha hakijafika NHIF.

Katika mkutano Majaliwa pia alitoa takwimu za mafanikio yaliyofikiwa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi cha miaka mitano na akawaomba TAHLISO waende kuwaeleza wananchi mafanikio hayo.

Miongoni mwa mafanikio hayo ni kurudisha nidhamu serikali kwa watumishi wa umma ambako kuligusa watumishi zaidi ya 32,555 wakiwamo 15,308 walioachishwa kazi na 19,708 walikuwa watumishi hewa ambapo serikali iliokoa Sh bilioni 19.8 kutoka na udhibiti huo.

Pia ilipambana na wala rushwa na mafisadi kwa kuanzisha mahakama ya mafisadi mwaka 2016 ambapo fedha zilizopatikana kutokana kuwabana mafisadi zinatumika katika kujenga miradi mbalimbali nchini.

Pia serikali imepambana na biashara ya dawa za kulevya ambapo imedhibiti uingizaji dawa za kulevya kwa asilimia zaidi ya 90 na sasa inadhibiti wazalishaji, wasafirishaji, wauzaji na watumiaji.

Serikali imebadilisha sheria mbalimbali kwa ajili ya kulinda raslimali na maliasili za taifa hasa madini ambapo imeanzisha masoko 28 na vituo 13 vya kuuza madini nchini pamoja na kujenga ukuta kudhibiti tanzanite ambayo mauzo yake yameongezeka kutoka Sh bilioni 194 mwaka 2014/15 hadi Sh bilioni 346 mwaka 2019/2020.

Waziri Mkuu alisema katika mwaka huu wa fedha Serikali ilipanga kukusanya mapato yatokanayo na madini kuwa Sh bilioni 470 lakini hadi Juni 30, mwaka huu imeshakusanya Sh bilioni 528 sawa na ongezeko la asilimia 58.

Alisema pia imepata mafanikio makubwa kwa kuongezeka mapato ya ndani ambapo mwaka 2014/15 serikali ilipata Sh trilioni 11 lakini hadi mwaka 2018/19 imepata Sh trilioni 18.5 sawa na ongezeko la asilimia 69.1 Ukusanyaji wa kodi nao umeongezeka kutoa Sh bilioni 825 katika mwaka huo na kuongezeka hadi Sh trilioni 1.3 katika mwaka 2018/19.

Alisema uchumi wa Tanzania umekua kutoka wastani wa asilimia 6.2 katika mwaka 2014/15 hadi wastani wa asilimia 6.9 na kuifanya Tanzania kuingia katika uchumi wa kati kabla ya miaka mitano iliyopangwa 2025.

Pia imepunguza umasikini na kuongeza ajira katika sekta mbalimbali za viwanda, kilimo, biashara, madini na utalii pamoja na sekta nyingine kutokana na serikali kuanzisha miradi mingi nchini vikiwamo viwanda vipya vilivyozalisha ajira 486,601.

Serikali pia imejenga na kukarabati miundombinu mbalimbali ya sekta ya afya katika maeneo ya huduma ya afya 1,769 kati yake zahanati 1,198, vituo vya afya 487, hospitali za wilaya 71 na hospitali za mikoa 10 pamoja na rufaa tatu.

Pia imeanzisha miradi ya kusambaza umeme vijijini katika nchi nzima ambapo kati ya vijiji 12,268 umefika katika vijiji 9,112 na bado takribani vijiji 3,000 na kazi hiyo imefikia asilimia 80 na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza Afrika kusambaza umeme katika maeneo mengi vijijini.

Serikali imejenga na kukarabati reli ya uhuru ambapo reli ya kati imekarabatiwa na ya kwenda kaskazini Tanga hadi Moshi ambapo tayari treni inafika na Arusha itakamlika karibuni.

Ujenzi wa reli ya kisasa kipande cha Dar hadi Morogoro umefikia asilimia 78 na kipande cha Morogoro hadi Makutupora umefikia asilimia 30 mradi huo utakamilika Julai mwakani na utagharimu Sh trilioni 7.062.

Aidha alisema ujenzi wa meli unaendelea katika maziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa na lengo ni kufungua mianya ya biashara ambayo wasoni hao wataitumia mara wakihitimu.

Pia imefanikiwa kuboresha kilimo, mifugo na uvuvi ambazo Watanzania asilimia 75 wapo katika sekta hizo na kwamba Tanzania ina uhakika wa chakula na ziada ya tani 3.4.

Aliwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano ya kampeni ili wachague sera za chama gani zinafaa na wakipigie kura katika uchaguzi.

Alisema wajitokeze kwa wingi kwenye mikutano ya kampeni itakayoanza Agosti 26, mwaka huu wasikilize sera na kuchambua na kisha wakipigie chama chenye kuleta maendeleo nchini.

Akitangaza Azimio au Tamko la Tahliso Mwenyekiti wake, Niboye alisema wanachama takribani 150 nchini wanaahidi kwamba wanaungana na Watanzania wengine kumuunga mkono Rais John Magufuli katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 28, 2020.

Majaliwa alisema atafikisha salamu hizo kwa Rais Magufuli na akaahidi kwamba atawapa nafasi wasomi 10 au 100 kwenda kwenye kampeni kueleza mafanikio ya Serikali kwa wananchi, wajipange fursa hiyo inakuja. Tahliso pia ilitoa Tuzo za Heshima kwa Rais John Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa kazi nzuri wanazofanya.

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi