loader
Majaliwa: Takukuru endeleeni kung’ata

Majaliwa: Takukuru endeleeni kung’ata

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), iendelee kukaza uzi kwa wagombea wanaojihusisha na vitendo vya rushwa wakati huu wa uchaguzi.

Aidha, ameitaka Takukuru ihakikishe Watanzania hawarubuniwi ili watumie vizuri utashi wao wa kisiasa kuchagua viongozi bora. Alitoa agizo hilo jana alipofungua jengo la Intelijensia Takukuru Makao Makuu Dodoma.

“Tayari tumeshuhudia mking’ata baadhi ya wagombea waliojihusisha na vitendo vya rushwa kwenye hatua za awali za uteuzi wa wagombea kupitia vyama vyao. Msiache; endeleeni kukaza uzi na kuwadhibiti wote wenye kujihusisha na vitendo hivyo,” alisisitiza.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa vyombo vya habari, Majaliwa aliwasihi Takukuru watumie vizuri ofisi hiyo, kukusanya taarifa za kiintelijensia zinazowahusu wagombea, vyama au wananchi watakaojihusisha na vitendo vya rushwa kwenye Uchaguzi Mkuu.

“Sote tunatambua kuwa Oktoba mwaka huu taifa letu litaendesha Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani…mna jukumu zito la kuhakikisha Watanzania hawarubuniwi na msimuonee au kumpendelea yeyote kwa maslahi yenu binafsi,” alisema.

Majaliwa alisema kuwa wananchi wanatakiwa kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura Oktoba 28, mwaka huu, na kwamba wana wajibu wa kuchagua serikali bora na kiongozi bora atakayewaletea maendeleo.

“Chagueni kiongozi mwenye maono aliyetenda na atakayetenda... niungane pia na Rais Dk John Magufuli kuwasihi wanasiasa na wagombea wenzangu wa nafasi mbalimbali za uongozi kwenye Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba mwaka huu tuache kutumia rushwa kwa lengo la kununua uongozi,” alisema.

Majaliwa alisema kuwa wakati huu nchi inapojiandaa kwa Uchaguzi Mkuu, Watanzania wakiwemo viongozi wanapaswa kuzingatia nasaha za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere katika moja ya hotuba zake alipowataka wajiulize kwamba mgombea anayetumia rushwa kununua kura amepata wapi fedha hizo na je akipata uongozi, fedha hizo atazirudishaje.

“Kwa hivyo, nasi ifike mahala tuwahoji hawa wanaotutia doa. Je, wewe mwenzetu unayetumia rushwa kununua uongozi umepata wapi fedha hizo? Na je? tukikuchagua, utarejesha vipi fedha hizo? Nitoe wito kwa Watanzania wote, msikubali kuwachagua wagombea wanaotumia rushwa ili kupata nafasi za uongozi.”alisema.

Aliwapongeza viongozi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na watendaji wa Takukuru kwa kusimamia mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi ndani na nje ya serikali.

Pia, alisema kuwa ni lazima wafanye uchunguzi wa kutosha kuhusu matumizi ya fedha zote za umma na kujua kama matumizi hayo yanaenda sambamba na matakwa ya kisheria.

“Rais Dk. Magufuli amemudu kurejesha imani ya Watanzania kwa watumishi wa umma na zaidi ya yote amerejesha uwajibikaji. Ni ukweli usiopingika kwamba tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa kulikabili tatizo la rushwa na ufisadi ndani ya taifa letu,” alisema Majaliwa.

Waziri Mkuu alisema amefurahishwa na kitendo cha Takukuru kurejesha fedha na mali za wanyonge waliodhulumiwa mauzo ya mazao yao na kutozwa riba za kubambikiziwa.

“Hatua hiyo imeudhihirishia umma kuwa Takukuru sasa inang’ata kwelikweli… operesheni ya urejeshaji wa fedha za wakulima zilizotokana na mauzo ya korosho na ufuta ilianzia mkoani Lindi na baadaye kuhamia katika mikoa ya Mtwara, Pwani, Simiyu na hatimaye nchi nzima,” alisema.

Majaliwa alisema kuwa Takukuru imewafuta machozi Watanzania wengi hususan wastaafu ambao kwa kutotambua haki zao, walikopa fedha kidogo kutoka kwa watu wenye dhuluma.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/d775800d395ee2f34d7e63778b10eb25.jpg

RAIS Samia Suluhu Hassan amehutubia taifa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi