loader
Biden azindua  kampeni ya urais

Biden azindua kampeni ya urais

MGOMBEA urais kupitia Chama cha Democratic nchini Marekani, Joe Biden na mgombea mwenza wake, Kamala Harris, kwa pamoja wamezindua kampeni yao ya urais kuelekea Uchaguzi Mkuu Novemba, mwaka huu.

Hii imekuja siku moja baada ya Biden kumteua Harris kuwa mgombea wake mwenza na wawili hao wamemwelezea Rais Donald Trump kama kiongozi asiyejua uongozi na aliyeiharibu Marekani.

Harris alianza kumshambulia Trump, akisema amewaingiza hatarini Wamarekani kwa kushindwa kulichukulia kwa umakini janga la corona na kuitumbukiza nchi hiyo kwenye mzozo wa kiuchumi, ubaguzi wa rangi na masuala mengine ya kijamii.

Kwa upande wake, Biden alisema serikali yake na Harris itakuwa na mkakati thabiti wa kukabiliana na covid-19 utakaobadilisha hali ya mambo.

“Uvaaji wa barakoa, kuongeza upimaji na kuziwezesha serikali za majimbo ili kufungua shule na biashara kwa usalama tunaweza. Tunachohitaji ni Rais na makamu walio tayari kuongoza na kuwajibika," alisema Biden.

Naye Rais Trump alijibu mapigo na kumuelezea Harris kama mtu aliyeanguka mithili ya  jiwe baada ya kushindwa katika uteuzi wa kuwa mgombea urais wa chama chake cha Democratic.

Harris ni mwanamama Mmarekani mweusi mwenye asili ya India na Jamaica, aliwahi kuwa hasimu wa Biden katika mchuano wa kuwania urais.

Harris ni mwanasheria kitaaluma na Seneta wa Califonia na kwa muda mrefu amekuwa akichukuliwa kama mgombea wa nafasi ya pili baada ya Biden.

Mara kadhaa mwanasheria huyo amekuwa akitoa mwito wa kufanyika kwa mageuzi ndani ya idara ya Polisi nchini humo.

Marekani inatarajia kufanya uchaguzi wa Rais Novemba 3, mwaka huu, ambapo Rais Trump anawania tena muhula wa pili na atachuana na Biden katika kinyang’anyiro hicho.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/cb6068bbf522763140f9464b543974a0.jpg

UGANDA imekubali kuongeza maradufu idadi ya ...

foto
Mwandishi: DELAWARE, Marekani

Post your comments