loader
Waliokatwa ubunge CCM watoa ya moyoni

Waliokatwa ubunge CCM watoa ya moyoni

WATU wa kada tofauti wakiwamo waliogombea ubunge ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wameeleza kuguswa na uteuzi uliofanyika juzi wakipongeza mchakato mzima kuwa ni wa kimkakati unaodhihirisha ukomavu wa chama kisiasa na demokrasia.

Baadhi ya walioachwa katika uteuzi, wamesema wamepokea matokeo kwamikono miwili na kuahidi kuwa bega kwa bega katika kampeni kuhakikisha waliopitishwa kupeperusha bendera ya CCM wanashinda.

Miongoni mwa wagombea waliokatwa majina ambao wamesema wako bega kwa began a chama ni pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja na aliyekuwa Mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda na Enock Kiswaga aliyeongoza katika kura za maoni katika jimbo la Wanging’ombe.

Wengine waliosema watashiriki kampeni kikamilifu kuhakikisha walioteuliwa wanashinda, ni aliyekuwa mshindi wa kwanza wa kura za maoni katika Jimbo la Kawe, Furaha Domick na mwanasiasa maarufu aliyegombea Jimbo la Arusha Mjini, Samson Mwigamba. Waahidi ushirikiano

“Uteuzi wa chama nimeupokea kwa heshima kubwa. Nitashirikiana na chama chetu na wana Sengerema kwa ujumla kuhakikisha kwamba CCM inashinda kwa kishindo,” alisema Ngeleja kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Aliwashukuru wana Sengerema na CCM kwa kumuamini kutumikia jimbo hilo kwa miaka 15. Katika uteuzi wa juzi, chama kimempitisha Tabasamu Mwagao kugombea ubunge jimboni humo kwenye uchaguzi mkuu.

Aliyekuwa mbunge wa Mbinga Mjini, Mapunda pia alishukuru wananchi wa Mbinga kwa heshima waliyompatia kwa miaka mitano kuwaongoza.

Alimpongeza mgombea aliyeteuliwa na chama chake kuwania jimbo hilo. “…Mimi ni mwana CCM, nimekuwa mwana CCM na nitaendelea kuwa mwana CCM.

Twendeni sasa tukatafute kura kwa wananchi tupate ushindi wa kishindo kwa Rais, wabunge na madiwani,” aliandika pia kwenye ukurasa wake wa Instagram, Facebook na Twitter.

Kiswaga, aliyeongoza kura za maoni katika jimbo la Wanging’ombe, alieleza kuwa amepokea kwa moyo mkunjufu matokeo hayo ya uteuzi wa mgombea mwenzake Festo Dugange kuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo.

“Ni kweli niliongoza katika kura za maoni! Itoshe kusema ulikuwa mchakato tu.Niwashukuru wajumbe wote walioniunga mkono.

Nitamuunga mkono mgombea aliyepitishwa na Chama changu CCM,” alisisitiza. Akizungumza na waandishi wa habari, Dominick aliyeongoza kura za maoni katika jimbo la Kawe, alikishukuru chama na wajumbe kwa kumuamini na kumpatia ushindi huo wa kura za maoni.

“Mimi nimekubaliana na maamuzi ya chama na nitamuunga mkono aliyependekezwa na chama ndugu Askofu Josephat Gwajima, lengo ni kukipatia ushindi chama chetu,” alisema.

Alisema anaamini uteuzi umefanyika kwa umakini na kwamba chama hakijakosea na kimefanya uamuzi sahihi.

Aliyegombea Jimbo la Arusha Mjini, Mwigamba, alisema CCM ni taasisi kongwe na uteuzi umezingatia mambo yote ya kuwezesha wagombea kushinda.

“Siasa ni sayansi…Nakubaliana na gazeti lenu (HabariLeo) lilivyosema kwamba ni uteuzi wa kimkakati kwa sababu itakuwa haina maana kama utafanya uteuzi unaokwenda kutengeneza mpasuko ndani ya chama na kusababisha wapinzani washinde,” alisema.

Kwa mujibu wa Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM , Humphrey Polepole miongoni mwa sifa zilizozingatiwa ni utendaji kazi wa mgombea, nidhamu, mwenye mahusiano mazuri na wananchi na atakayekiweka chama pamoja.

Ukomavu CCM Mtaalamu wa Masuala ya Diplomasia na Uchumi, Profesa Wetengere Kitojo alisema CCM imeonesha ukomavu wa siasa kwa kiwango kikubwa.

“Kwanza niseme wazi mimi sio mwanachama wa chama chochote cha siasa, ila nimefuatilia mchakato mzima wa kupata wagombea wa CCM kwa sababu wameufanya kwa wazi na shirikishi,wameona makosa yaliyofanywa ngazi ya chini na huko juu wakayarekebisha, hili ni la kupongeza,” alisema Profesa Kitojo.

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Dk Charles Kitima alisema vyama vyote vya siasa vimeonesha ukomavu wa demokrasia.

“Tumeona kila chama kilijitahidi kufuata mifumo yao ya vyama, wameanzia ngazi ya chini kabisa hadi juu ambapo kila ngazi wajumbe wametoa maoni yao na na kufanya mchakato huo kuwa shirikishi kwa vigezo vyote, hii inadhihirisha demokrasia imo kwenye vyama hivyo,” alisema Dk Kitima.

 

Habari hii imeandikwa na Stella Nyemenohi, Ikunda Erick na Halima Mlacha

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/61379928063e872da284350a2b76871f.jpg

WAFANYABISHARA mbalimbali wa Temeke, ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi