loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Miradi ya kimkakati yapaisha maisha ya wananchi

MIRADI mbalimbali inayoendelea kutekelezwa na serikali imeonesha matokeo chanya kwa maisha ya watu na kuthibitisha kwamba si maendeleo ya vitu kama ambavyo baadhi ya wakosoaji wamekuwa wakiaminisha umma.

Miradi ambayo imedhihirisha kupaisha uchumi wa nchi na wananchi kwa kiwango kikubwa, ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya uchukuzi ikiwamo reli ya kisasa (SGR), barabara, madaraja, viwanja vya ndege; Mradi wa bwawa la kufua umeme wa maji la Julius Nyerere kwenye bonde la Mto Rufiji (JNHPP) na vituo vya mabasi.

Akizungumza na gazeti hili, aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, David Kafulila alieleza kushangazwa na wanaobeza miradi hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa na wananchi, wakiirejea kuwa ni maendeleo ya vitu.

“Kinachoitwa maendeleo ya vitu, wakosoaji wanarejea zaidi maamuzi ya ujenzi wa reli ya kisasa, kufufua shirika la ndege na mradi mkubwa kufua umeme wa bwawa la Nyerere,” alisema Kafulila.

Wanaobeza hawana msingi Kafulila ambaye amewahi kuwa mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kabla ya kuhamia NCCRMageuzi na kuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, alisema ujenzi wa miundombinu ya uchukuzi ilikuwa hoja ya upinzani miaka yote ukihoji sababu za nchi kukosa reli, meli za uhakika na shirika la ndege.

“Zaidi ya kuwa hoja ya upinzani miaka mingi, pia ripoti za Tafiti kama Poverty& Human Development ya mwaka 2008, ilionesha kwamba kwa nafasi ya Tanzania kijiografia, ikiwekeza sekta ya uchukuzi, sekta hiyo inachangia uchumi kuliko sekta yoyote kutokana na nafasi ya kimkakati kijiografia yaTanzania,” alisema.

Akipongeza serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli kwa mageuzi hayo, Kafulila alisema mgombea wa chama chenye mtazamo sahihi kuhusu maendeleo alipaswa aseme ni namna gani ataendeleza miradi hiyo lakini kinyume chake, wapo wagombea wanaobeza wakisema ni maendeleo ya vitu.

“Maendeleo ya watu huchagizwa na maendeleo ya vitu. Hivyo, katika uchaguzi huu Oktoba 28, 2020 ni vyema kuchagua watu makini, ambao tayari tumekwishaona utendaji kazi wao; katika kuwezesha watu kujiletea maendeleo yao na taifa kwa ujumla,” alisema mchangiaji wa makala katika gazeti hili, Gorwe Machage.

Mradi wa JNHPP Miongoni mwa miradi ambayo wananchi wanasema wameanza kuona matunda yake ni wa bwawa la RufijiJNHPP ambao Mhandisi Mkazi wa mradi , Mushubila Kamuhabwa alikaririwa hivi karibuni akisema wananchi wanaoishi kwenye vijiji vinavyouzunguka wamepata miundombinu wezeshi kama vile umeme unaotoka Morogoro.

Vile vile Watanzania wapatao 4,000 kutoka maeneo mbalimbali nchini, wameajiriwa na inatarajiwa ajira zitaongezeka kufikia watu 6,000 mradi utakapofika hatua ya juu zaidi.

Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Kisaki mkoani Morogoro, kilichopo kilometa 60 kutoka kwenye mradi, wanakiri kushuhudia ukuaji wa biashara na ajira miongoni mwao.

“Kisaki inakuja juu… Kwa sasa biashara inakua kwa kasi sana tofauti na hapo awali... Watu wameongezeka sana,” alisema Ali Matumbo na kukiri kufikiwa na umeme wenye uhakika.

Meli ziwa Victoria Ukarabati wa meli ya New Mv Victoria ‘Hapa Kazi Tu’ pamoja na Mv Butiama katika Ziwa Victoria zilizoanza safari wiki iliyopita, ni ukombozi mwingine kwa wananchi na taifa unaotokana na uwekezaji wa serikali katika miradi mbalimbali ya uchukuzi.

Wakati usafirishaji mizigo kati ya Mwanza na Bukoba kwa njia ya barabara inagharimu kati ya Sh 80,000 na Sh 100,000 kwa tani, upande wa meli ni Sh 27,000 kwa tani hatua ambayo imeleta nafuu kubwa kwa wafanyabiashara na walaji wa bidhaa mbalimbali katika miji hiyo.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Edmund Rutta wanatarajia watu wengi watatumia usafiri huo kutokana na unafuu siyo tu wa kusafirisha mizigo, bali pia nauli ambayo daraja la kwanza ni Sh 45,000; la pili Sh 30,000 na daraja la tatu ni Sh 16,000.

Barabara Dar, stendi MAPINDUZI makubwa ya kiuchumi yanatarajiwa kuonekana kwa wakazi wa maeneo inakotekelezwa miradi mikubwa ya maendeleo nchini ikiwamo jijini Dar es Salaam hatua inayodhihirisha dhamira ya dhati ya serikali kuwakomboa wananchi kutoka katika umasikini wa kipato.

Upanuzi wa barabara ya Morogoro kwa njia nane kutoka Kimara- Stopover, Dar es Salaam hadi Kibaha, mkoani Pwani na mradi wa ujenzi wa stendi kuu ya mabasi ya mkoani na nchi jirani cha Mbezi Luis, inasubiriwa kwa shauku na wananchi wakisema itafungua fursa nyingi za kiuchumi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi wa Serikali za Mitaa na wananchi wa maeneo hayo, wamepongeza serikali chini ya Rais John Magufuli huku wakijiandaa kutumia fursa ya miradi hiyo kukuza kipato chao na uchumi wa nchi.

Mkazi wa Mbezi, wilayani Ubungo, Michael Mallya alisema fursa za kiuchumi kutokana na ujenzi wa stendi mpya ya mabasi ya mikoani eneo la Mbezi Luis na upanuzi wa barabara ya njia nane ni nyingi.

Mallya ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mshikamano, Kata ya Mbezi kwa tiketi ya Chadema, alisema miradi hiyo itabadilisha hadhi ya Mbezi na kuleta ajira kwa vijana.

Alisema watu watakaowekeza biashara zao hawatawachukua watu kutoka mbali kupunguza gharama. Pia mama na baba lishe, hoteli na migahawa mikubwa itajengwa eneo hilo.

“Tuliomba watu tuliohamishwa hapo Mbezi kupisha miradi hiyo tupewe kipaumbele miradi ikikamilika. Kama ni kuweka vibanda au kutakuwa na fremu za biashara tufikiriwe kwanza na tunaamini itakuwa hivyo maana tuliandika barua Jiji la Dar es Salaam na wakasema watashughulikia hilo, tunasubiri majibu,” alisema Mallya.

Mkazi wa Kata ya Msigani, Erasmo Nziku ambaye ni mfanyabiashara, alisema wamejipanga kunufaika miradi hiyo itakapokamilika ikiwa ni pamoja na kuongeza maduka na kuajiri vijana wengi zaidi.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mshikamano, Kata ya Mbezi, wilayani Ubungo, Baraka Mwaijande, alisema amejipanga kuendelea kuhamasisha wakazi wa mtaa wake kuchangamkia fursa hizo zilizopo kwenye eneo lake kwani uwekezaji huo ni mkubwa na unafanywa na Serikali kwa dhamira ya kumkomboa Mtanzania wa chini.

“Nimehamasisha watumie fursa, biashara zitakuwa nyingi kwenye vizimba nje na ndani ya stendi, barabara inayopanuliwa ni fursa kubwa, Mbezi si ya zamani.

Jana (juzi) na leo (jana) ninaendelea na mikutano kwenye mashina kutoa elimu kuhusu vitambulisho vya ujasiriamali na kujiandaa kwa fursa hizo,” alisema Mwaijande.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Zipora Liana, stendi hiyo inatarajiwa kuanza kutumika Oktoba mwaka huu. Alisema hivi karibuni kwamba ujenzi wake unagharimu Sh bilioni 50.9 na ina uwezo wa kuchukua mabasi 108 kwa wakati mmoja, magari madogo zaidi ya 100.

Kitakuwa na huduma mbalimbali kama migahawa, benki, zahanati, kituo cha polisi, maduka na sehemu za kuosha magari Mradi wa Upanuzi wa Njia Nane unagharimu Sh bilioni 140.44 ambazo ni fedha za ndani.

Ujenzi ulianza Julai 21 mwaka 2018 na unatarajiwa kukamilika Januari mwakani ukilenga kupunguza msongamano uliolazimu magari kutumia saa tatu kuingia na kutoka katika jiji la Dar es Salaam. Habari hii imeandikwa na Stella Nyemenohi na Gloria Tesha.

MBUNGE  wa Mkuranga Abdallah Ulega anatarajiwa kufanya ziara ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi