loader
Dstv Habarileo  Mobile
Serikali yavuna bil 80/- mauzo ya dhahabu

Serikali yavuna bil 80/- mauzo ya dhahabu

MKOA wa Geita umepata mafanikio kupitia madini ya dhahabu na katika miaka mitano kuanzia 2016/ 2020 umepata kilo 13,052 zenye thamani ya shilingi trilioni 1.169.

Katika kipindi hicho tozo ya Serikali ilikuwa sh bilioni 79. 55 hivyo kuonesha kuwa sekta hiyo ya madini imeendelea kuimarika.

Mkuu wa Mkoa wa Geita,  Robert Gabriel  aliyasema hayo wakati akizungumza  katika ofisi za Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) inayochapisha magazeti ya Daily News, Sunday News, HabariLeo, HabariLeo Afrika Mashariki, Spoti Leo, habari kupitia tovuti, chaneli ya Youtube na kurasa za mitandao ya kijamii.

Gabriel alisema jijini Dar es Salaam, mafanikio katika sekta ya madini yamepatikana kutokana na juhudi za kuiimarisha zilizofanywa na uongozi wa Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli.

“Yamekuwepo mageuzi makubwa kwenye sekta ya madini, kuanzia kikao cha wadau wa madini kilipokutana kwa ajili ya kuondoa baadhi ya kero, urasimu na malalamiko mbalimbali yamesaidia kwa kiwango kikubwa kuimarisha sekta hiyo,” alisema Gabriel.

Alisema katika mwaka 2016 waliweza kupata kilo za dhahabu 337.4 zenye thamani ya sh bilioni 28.8 huku tozo ya Serikali ikiwa sh bilioni 1.15, mwaka 2017 zilipatikana kilo 832.5 zenye thamani ya sh bilioni 62.9 na tozo yaSserikali ilikuwa sh bilioni 3.4.

Gabriel alisema, mwaka 2018 zilipatikana kilo 1634 za madini hayo zenye thamani ya sh bilioni 125.4 na tozo ya Serikali ikiwa sh bilioni 8.7, mwaka 2019 lilipoanzishwa soko la kwanza la madini zilipatikana kilo 4656 zenye thamani ya sh bilioni 375.5 na tozo ya Serikali ilikuwa sh bilioni 26.

Alisema mwaka 2020 pamoja na kuwepo kwa maambukizi ya virusi vya corona zilipatikana kilo 5,591 za dhahabu zenye thamani ya sh bilioni 576.5 na tozo ya Serikali ilikuwa sh bilioni 40.3.

Kuhusu maduhuli yaliyokusanywa na Serikali katika kipindi hicho cha miaka mitano, alisema katika mwaka 2015/16 ilikuwa na lengo la kukusanya sh bilioni 50 utekelezaji ukawa ni sh bilioni 53.6, mwaka 2016/17 ililenga kukusanya sh bilioni 55.2 na kufikia sh bilioni 56.89 na mwaka 2017/18 ililenga sh bilioni 50.5 na kufikia sh bilioni 114.74.

Alisema katika mwaka 2018/19 ililenga kufikia sh bilioni 85 na kufikia sh bilioni 128 na mwaka 2019/20 walilenga kufikia sh bilioni 156.34 na kufikia sh bilioni 207.7 na hiyo yote inatokana na sekta ya madini kuwa na mapinduzi makubwa kwa nchi.

Gabriel alisema, biashara ya dhahabu ni nzuri hasa baada ya kuanzishwa masoko ya madini na hadi sasa kuna mawakala 34.

Alisema, kutokana na mafanikio katika sekta hiyo mkoa umeweza kujenga soko kubwa lenye vizimba zaidi ya 230.

“Tumeboresha soko hilo, tutaweka mfumo wa kuchajia simu ili mwananchi asihangaike, kutakuwa na bucha 13 za nyama, maeneo maalumu ya kuhifadhi na kuuza samaki na kuku lengo kubwa ni kumuondoa barabarani,” alisema Gabriel.

foto
Mwandishi: Lucy Lyatuu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi