loader
Dstv Habarileo Mobile
Picha

Kama hali ni hii, heri wangeacha tu

BAADA ya kukaa nje kwa takribani miaka mitatu, nilidhani mgombea urais wa chama kikuu cha upinzani nchini kwa sasa (Chadema), Tundu Lissu, amefanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya nafasi anayoamini kwamba anatosha.

Niliamini amekuwa akisoma vya kutosha, akiangalia sera za chama tawala na kulinganisha na hali ilivyo huko nje alikokuwa na kwamba pengine sasa anaweza akawa na kitu kipya.

Nilidhani atakuwa ameona pia mambo mazuri yaliyofanyika nchini ambayo kama Mtanzania angeyapongeza na kisha akatusaidia ni wapi, kwa mtazamo wake pamepelea. Nilijua amekuja akiwa ameangalia kila sekta kama vile kilimo, elimu, biashara, viwanda, nishati, madini, makusanyo ya serikali na kadhalika. 

Pamoja na Rais John Magufuli kuonesha uwezo mkubwa katika kupambana na mdudu aliyetutesa kwa miaka mingi yaani ufisadi, nilitegemea kumsikia yeye akigusia mikakati mikubwa zaidi aliyonayo kuliko iliyofanyika.

Katika makala yake kwa gazeti hili wiki iliyopita, David Kafulila alisema wagombea kuisusa ajenda ya ufisadi ni kujinyonga kisiasa kwenye dunia ya wazalendo hata kama kuiacha kwao kunaweza kuwanufaisha kupitia wafanyabiashara, taasisi, makampuni na hata mataifa waathirika wa operesheni ya JPM dhidi ya mafisadi ndani na nje ya nchi.

Kuna suala pia la umasikini ambalo Rais Magufuli amekuwa akijaribu kupambana nalo kwa mafanikio makubwa, suala ambalo marais waliopita liliwaumiza pia hadi kujitahidi pia kupambana nalo hadi kuanzisha vitu kama Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), mabilioni ya JK na kadhalika. Nilitegemea kumsikia yeye akiwa na mbinu bora zaidi katika kupambana na hilo, lakini hakuna kitu!

Baada ya kuwasili na kuanza kuhojiwa na vituo kadhaa vya televisheni na redio vya Kenya na kisha kufanya ziara kadhaa nchini, nimejaribu kufuatilia kusikia kama kuna hoja zenye mashiko zinazotolewa na Mtanzania mwenzetu huyu, lakini mpaka sasa nimeshindwa kuona kitu cha maana alichozungumza mintarafu kutupa sera mbadala.

Nikiulizwa kama kuna jambo la maana amezungumza, labda nitasema, tena kwa kusita sita pale alipodai kwamba endapo akichaguliwa kuwa rais hatolipiza kisasi. Nitasita sita kwa sababu pia sikumwelewa vyema anamaanisha kisasi cha aina gani hasa. Kwani nchi hii tunafanyiana visasi?

Kama anamaanisha tukio lake la kushambuliwa nimejiuliza sana analipiza kisasi kwa nini? Je, anawajua waliomshambulia? Kama ndivyo kwa nini asilisaidie Jeshi la Polisi?

Baadhi ya mambo ambayo nimesikia akiyataja ni kutaka Watanzania tujifungie ndani akimaanisha nchi yetu ina corona. Nimesikia pia akidai elimu yetu ni tegemezi na kwamba bila kutegemea misaada kutoa nje hatuwezi kuendesha elimu nchini, amekejeli pia vitambulisho vilivyotolewa kwa machinga na mengine hata siyakumbuki kwa sababu hayana uzito.

Katika msafara wake mmoja anatumia muda muhimu sana wa watu walioacha shughuli zao na kuishia kusema: “Sisi hatutembei na polisi kama Magufuli…Sisi hatufungulii watu kesi za uongo kama Magufuli. Sisi hatutafilisi wafanyabiashara kwa kutumia TRA, sisi tutafuatilia mbali vitambulisho vya machinga vilivyoletwa na Makonda pamoja na Magufuli. Sisi tutaongeza mishahara ya wafanyakazi kuanzia na hawa polisi…”

Yaani kimsingi, mgombea huyo hana kitu kipya. Bado ni aina ya wapinzani ambao wamekalia kutafuta hata kwa tochi upungufu wa serikali ya chama tawala na kufanya kuwa ndio ajenda zao badala ya kutupa sera mbadala. Kwa mfano, ukimuuliza ataongezaje mshahara wakati anapiga vita makusanyo naamini hana majibu.

Katika makala iliyopita nilizungumzia kidogo suala la corona, lakini hoja zake hizo nyepesi hata mwanangu wa kidato cha nne anaweza kuzijibu. Kwa mfano, hoja ya utegemezi kwenye elimu ambapo bila shaka analenga ule msaada tuliopewa na Benki ya Dunia katika kuboresha elimu, ina majibu lukuki. 

Kimsingi, hakuna nchi duniani isiyohitaji msaada. Hata taifa kubwa kama Marekani nalo hukopa. Hoja hapa ingekuwa sababu za mkopo, umuhimu wake na matumizi sahihi ya mkopo husika na si vinginevyo. Kwa nini Lissu hasemi pia kwamba serikali inatoa zaidi ya Sh billioni 20 kila mwezi ili kugharimia mpango wa elimu bure ambao umeleta manufaa makubwa katika elimu nchini? Je, hizo pia ni pesa tunazotegemea nje?

Wiki ijayo ikinipendeza nitajibu hoja zake nyingine nyepesi sana kama hiyo ya vitambulisho vya machinga na nyinginezo.

Kwa kifupi, heri huyu jamaa angebaki kimya na kuja kutoa hoja zake hizo nyepesi kwenye kampeni. Ametusaidia wengine kugundua kwamba kumbe ni mweupe sana kama karatasi. Ndio maana ninasema kama huyu ndiye mgombea wa Chadema wanayetaka apambane na ‘heavy weight’Magufuli, heri wangetafuta mwingine au wangeacha tu! 

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

5 Comments

 • avatar
  Martha
  26/08/2020

  UNATAFUTA HURUMA YA KUTEULIWA TENA HUNA LOLOTE.....!!HAKUNA LA MAANA LA KUMSAIDIA MWANANCHI WA KAWAIDA,LABDA KIDOGO KURUDI KWA HIZI SAFARI ZA TRENI....LKN HAYO MENGINE SISI MAKABWELA HAYATUSAIDII LOLOTE,DAWA TUNANUNUA KM KAWAIDA,MLO MMOJA KWA SIKU,ELIMU BURE CHANGA LA MACHO......MAANA HAO WADAU WA ELIMU WAMESAHAULIKA KABISA,NI KAZI TU BILA UHURU,KAZI TU BILA MAONI,WATU WAMENYAMANZISHWA HATA UHURU WA VYOMBA VYA HABARI HAUPO,TUNAISHI KINFIKI TU KUSIFIA SIFIA HATA PASIPOSTAILI ILI MRADI UENDELEE KUWA HAI...!!MAANA KUNA WATU WASIOJULIKANA.....!!!!!!!!WATZ TUMEROGWA NA MFU,HATA NYEUSI TUNAIONA NYEUPE.

 • avatar
  Philip julius
  27/08/2020

  Mi nadhani mwandishi umeandika mazuri tu yaani umeegamia upande wa mazuri yalofanywa kwa kifupi unaweza kueleza mapungufu ili hoja yako iweze kupimika maana yapo mengi tu hebu geuza upande wa pili wa shilingi tupime mazuri na mabaya

 • avatar
  Mussa
  27/08/2020

  Nakupongeza sana Mwandishi kwa nakala hii. Kwa kweli hoja za huyu mtu ni hafifu sana na zimejaa chembe chembe za tamaa ya madaraka, halufu ya chuki, ubinafsi na kukosa uzalendo. Watanzania tumpuuzeni.

 • avatar
  Kazumari
  27/08/2020

  Hivi kuna watu hawaelewi hakuna serikali inawagawia raia wake chakula au kuwaongezea kama wanakula mlo mmoja wawape Milo mitatu sijaona hiyo serikali inatakiwa kuangalia huduma muhimu kama maji usafiri umeme vinapatikana hivyo vinafingua fursa Kwa wananchi kuweza kutanua wigo wa kujitafutia rizki sasa weee mpe nchi huyo lissu halafu uone hiyo Milo mitatu utakapoitoa hivi vitu utakiwi kwenda chuo kikuu hiyo akili alokupa mungu ndio uitumie

 • avatar
  fahmy
  27/08/2020

  me naona mwandishi kaegemea upande mmoja .hasa chama tawala.ila hii ni demokrasia sio kama anayozunguza yote hayapo ila ni kama mtoto na mzazi wake hata kama mtoto kafanya vizuri mzazi akasema kibaya basi mzazi ndio mwenye nguvu..kwwli kuna mengine yanavuruga watu lakini mengine ni ya kweli .basi tumpe nafasi kama raiya anaekwenda kuqaakilisha nchi atoe pumba na mchele.hayo ndio maoni yangu..

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi