loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mtanzania anayeng’ara kwa utafiti wa aina yake China

‘MTANZANIA ashinda tuzo ya mtafi ti bora nchini China’. Ni kichwa cha habari kilichobeba taarifa kumhusu Hamenya Mpemba iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii.

Habari hiyo ikamtaja kwamba anasoma Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Uhifadhi wa Wanyamapori katika chuo cha Northeast Forest, mjini Harbin, China na kwamba tuzo ilikuwa ikishindaniwa na watafiti kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Ushindi unatokana na kufanikiwa kugundua uwapo wa mbwa mwitu (wolf) kwa mara ya kwanza katika eneo la pori la Hifadhi ya Taifa ya Hanma katika jimbo la Inner Mongolia. Ugunduzi ulifanyika baada ya kufunga zaidi ya kamera 200 katika eneo hilo.

Utafiti umechapishwa kwenye jarida la kimataifa la Zuolojia la nchini Pakistan tangu mwaka jana. Taarifa hizi zinanipa shauku ya kumtafuta Mtanzania huyu nipate undani zaidi wa maisha yake, alivyojitosa na siri ya mafanikio kwenye utafiti huo wa aina yake uliopaisha siyo tu jina lake pekee kimataifa, bali pia la Tanzania.

Nafanikiwa kufanya mahojiano naye. Ananithibitishia kwamba ameibuka mshindi wa Tuzo ya Mtafiti Bora wa Kimataifa ambayo ilishindaniwa na watafiti hasa wa kuanzia miaka ya 2015 kutoka mataifa mbalimbali.

Nabaini Mpemba alizaliwa miaka 36 iliyopita wilayani Kibondo Mkoa wa Kigoma. Ni mtoto wa pili kati ya watoto wanne wa familia ya Mwalimu Michael Runaku (sasa marehemu) na Victoria Fulela.

Baba yake alifariki akiwa mdogo hivyo akalelewa na mama yake. Alipoanza shule, yeye na ndugu zake waliishi na baba yao mdogo, mzee Martin Mpemba Runaku.

Alimsimamia masomo katika shule za msingi nne tofauti alizosoma wilayani Kibondo ambazo ni Nyamtukuza (sasa ipo wilayani Kakonko); Mkarazi iliyopo Mabamba na shule ya msingi Kibondo.

Kadri baba mdogo alivyokuwa akihamishwa, ndivyo alivyohama shule na hatimaye akahitimu darasa la saba mwaka 1999 katika shule ya Kanyamahela wilayan Kibondo.

Alichaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari Malagarasi iliyopo Kibondo Mjini mwaka 2000. Akiwa kidato cha pili, alihamia shule ya sekondari Kigoma hadi alipohitimu mwaka 2003 na kufaulu kwa daraja la kwanza.

Alijiunga na kidato cha tano katika shule ya Kwiro, iliyopo Mahenge Ulanga Morogoro akichukua masomo ya Kemia, Baolojia na Jiografia (CBG). Baadaye alihamia Shule ya Sekondari Milambo, mjini Tabora na kuhitimu kidato cha sita kwa daraja la pili.

Alivyokosa ada Safari yake kitaaluma iliendelea hadi mwaka 2006 alipojiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kusoma Shahada ya Sayansi ya Mazingira ya Majini.

Hata hivyo, kabla ya muhula wa kwanza kuisha, yeye na baadhi ya wanafunzi walisimamishwa masomo kwa sababu za kutolipa ada. “Kama utakumbuka vizuri mwaka huo mambo ya mikopo ya Elimu ya Juu yalisumbua sana na Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia wa wakati huo Profesa Peter Msolla alitangaza kwamba wavulana wenye ufaulu wa daraja la pili wasingepewa mikopo,” anasema.

Anasema, “jambo hilo liliniumiza sana katika maisha yangu. Tulitakiwa kurudi nyumbani kwa ahadi kwamba mwaka unaofuata tutapewa mikopo na kuendelea na shule.

Tulitakiwa kuahirisha masomo.” Mwaka 2007 alirudi chuoni kuendelea na masomo. Ingawa alipenda kuendelea na shahada aliyokuwa akisoma, alishauriana na wanafunzi wenzake wakaona ili kuhakikisha mwaka unaofuata wanaendelea na chuo, waombe pia shahada ambazo upo uhakika wa kupata mkopo. Aliamua kuomba Shahada ya Sayansi ya Ualimu.

“Niliumia sana, niliambiwa kama nataka kusoma ile shahada basi niahirishe tena mwaka mwingine hadi mwaka unaofuata na sikuwa tayari basi nikalazimika kuendelea na shahada ya sayansi na elimu.”

Alihitimu chuoni hapo mwaka 2010 kwa ufaulu wa daraja ya pili la juu. Aliingia mtaani na kufanya kazi kadhaa kabla ya kupata udhamini wa Serikali ya China kwenda kusoma Shahada ya Pili mwaka 2011.

Lakini kutokana na sababu mbalimbali, hakwenda mwaka huo. Mwaka uliofuata, aliomba udhamini sehemu mbalimbali, akafanikiwa kupata sehemu tatu tofauti; mbili zikiwa nje ya nchi na moja ya nchini.

Baada ya kujadiliana na familia, aliamua kwenda China katika chuo cha Northeast Normal kilichopo mjini Changchun Jimbo la Jilin ambako alisoma Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika ikolojia.

“Nilimaliza digrii yangu na kufanya vizuri sana kiasi ambacho kilimfanya mwalimu wangu kuandika barua rasmi kwa chombo kinachohusika na kutoa udhamini wa serikali ya China yaani Chinese Government Scholarship Council wa kuendelea na shahada yangu ya Uzamivu (PhD).” Shahada ya Uzamivu Mwaka 2015 alianza masomo ya PhD katika Chuo cha Northeast Forestry kilichopo mjini Harbin katika jimbo la Heilongjiang.

Ilikuwa ahitimu mwaka huu lakini kutokana na sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (Covid-19), atahitimu mwakani.

“Naipenda kazi hii ya utafiti. Ni ngumu lakini penye nia pana njia,” Mpemba ndivyo anaeleza safari yake ya taaluma na hata jina lake kuchomoza kimataifa kupitia utafiti wa aina yake uliompatia tuzo mwaka huu.

Anajieleza zaidi akisema: Utafiti uliompatia tuzo Utafiti ulionifanya nishinde ni sehemu ndogo ya utafiti wangu jimboni Inner Mongolia. Kwa lugha rahisi, utafiti ulikuwa unaangalia athari za uwapo wa viashiria; mfano picha, sauti, harufu za wanyama wakubwa wapatikanao au waliowahi kupatikana maeneo hayo.

Wanyama hao ni kama vile chui milia na dubu kwenye eneo au pori kwa mtawanyiko na tabia za wanyama wengine wakiwamo wakubwa wenzao, wa kati na wadogo wa aina zote. Mfano, wanaokula wenzao na wanaoliwa katika eneo husika.

Utafiti huu huweza kufanyika kwa njia mbalimbali. Mimi na wenzangu tumekuwa tukitumia zaidi kamera maalumu za kusomea wanyamapori. Kamera hizi hufungwa sehemu ya mti ambayo itawezesha kumpiga picha mnyama yeyote atakayepita eneo husika.

Kamera zipo za aina nyingi ila sisi tunatumia kamera zinazotumia infrared kupiga picha. Kitu chochote, wakiwamo binadamu, kikipita mbele ya kamera kinapigwa picha automatically.

Hivyo baada ya muda, tunaenda kuchukua kamera na kuangalia wanyama waliomo, tunarekodi na kuendelea na hatua nyingine za kisayansi. Wakati naendelea na utafiti huo mkubwa, ndipo nilifanikiwa kumpata mnyama huyo kwenye moja ya kamera tulizosambaza porini.

Eneo ambalo lipo mbali sana katikati mwa hifadhi hiyo ambayo ni moja ya hifadhi ambazo ni ngumu kufanya utafiti kutokana na mazingira ya milima na mabonde makubwa.

Hapo ndipo niliamua kuandika chapisho la kisayansi kuripoti juu ya kuonekana kwa mnyama huyo mahali hapo na kufanikiwa kuchapisha utafiti huo katika jarida la kimataifa la Zuolojia la Pakistan.

Chapisho lilionesha uwapo wa mbwa mwitu katika eneo la milima ya Khingan, katika hifadhi ya Hanma iliyopo mji mdogo wa Jinhe jimboni Inner Mongolia. Katika utafiti huu pia nilishirikiana na watafiti wenzangu wa kichina.

Ila napenda kumtambua kwa karibu mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Pensylvania State cha Marekani, Dk Asia Murphy kwa ushirikiano wake mkubwa wakati tukiandika kazi hii.

Taarifa za ushindi nilizipokea kupitia kwa rafiki yangu Mchina anayeishi jimbo la Inner Mongolia. Nilitumiwa tangazo na rafiki zangu wa kichina wakinieleza juu ya suala hilo.

Nilijua nina vigezo vyote na tangu siku ya kwanza nilihisi ningeweza kushinda. Tunashukuru Mungu tumeshinda. Walioratibu shindano ni taasisi ya hifadhi za asili jimboni humo na hivyo tuzo ilitolewa na viongozi kutoka taasisi hiyo.

Kwa sasa nasubiri kuipokea ana kwa ana kwa sababu hivi sasa nipo Tanzania. Pamoja na chapisho hilo lililonipa ushindi, nimechapisha zaidi ya machapisho manane na yote nikiwa kama mchapishaji wa kwanza na yote yanahusu tabia, uhusiano, uwapo, mazingira na maisha ya wanyamapori kwa jumla. Siri ya mafanikio Tuzo niliyoshinda ilikuwa ikishindaniwa na watafiti kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Wala sikuwa na woga wowote. Imani yangu siku zote huwa ni kwamba kama unajiamini unaweza jambo fulani, ingia. Siku zote hakuna kushindwa bali kuna kushinda au kujifunza.

Siyo kwamba kila nikishiriki nashinda. La hasha! Nimeshiriki pia tuzo mbalimbali na kukosa. Huwa nikikosa, kuna kitu najifunza na kinanisaidia mbele ya safari. Mfano, mwaka juzi tulishiriki na mtafiti mwenzangu wa Marekani kwa pamoja kwenye kuomba fedha inayotolewa na shirika maarufu la mambo ya wanyamapori duniani na hatukubahatika kushinda lakini tulijifunza mengi sana.

Mwaka jana tulishiriki kupitia shindano lingine tukashinda japo haikuwa na ufadhili mzuri. Kilichonifanya kujiamini zaidi mara hii nadhani ni namna watu wa China walivyopokea taarifa za uwapo wa mnyama huyo eneo hilo.

Ziliwafurahisha sana na taarifa kurushwa na televisheni ya CCTV ya nchini humo. Ilinipa imani sana. Siri kubwa ya mafanikio ni kupenda unachofanya na kumtanguliza Mungu.

Siyo kwamba mimi ni bora zaidi kuliko wale wenzangu. Kuna mambo mengi unatakiwa kufanya ili utafiti wako uweze kuwa na matunda mazuri ikiwamo jinsi unavyopangilia utafiti wako vizuri Lazima usome maandiko mbalimbali na kwa uzuri ujue ni eneo gani, saa ngapi, muda gani wa mwaka ukiweka kamera zako unaweza kupata picha/ video za wanyama fulani kama wapo.

Hapo hasa ndipo unapotakiwa kuchanga karata zako vizuri na nafikiri hapo ndipo nilipokuwa tofauti na wengine na hatimaye kufanikiwa kumnasa mnyama huyo ambaye hakukuwa na ushahidi usiona shaka wa uwapo wake tangu mwaka 1972 kwa mujibu wa maandiko ya wenyeji wa maeneo hayo.

Utafiti wangu una maana kubwa kwa ikolojia ya wanyama mahali hapo ukizingatia wolf ni mmoja wa wanyama wa juu kabisa kwa walao wenzao eneo hilo. Hivyo ana mdhara makubwa kwa mfumo mzima wa maisha mahali hapo.

Kubwa zaidi, kiutalii, utafiti huu ni jambo kubwa sana. Utasaidia sana kutengeneza fedha kwa watalii wengi kwenda kwa lengo la kuona mbwa mwitu (wolf) siku zijazo na hivyo kukuza uchumi wa jimbo kwa jumla.

Ameipaisha Tanzania Utafiti kama huu niliofanya una manufaa makubwa sana kwenye sekta ya uchumi wa nchi. Mathalani, chukulia leo hii Tanzania tukatangaza uwapo wa chui milia (tiger) kwenye moja ya mbuga zetu! Watalii wengi watamiminika kutalii Tanzania.

Lakini pia unaposomwa ukiwa umebebwa na jina la Mtanzania, unafanya nchi yetu kujukulikana zaidi. Pia nimekuwa nikishiriki makongamano mbalimbali ya kimataifa katika mataifa mbalimbali. Kote huko najitangaza kama Mtanzania.

Vile vile, mmoja wa watafiti tuliyeandika naye kazi hii ni mtafiti mzuri wa Marekani na amekuwa akiuwasilisha kwenye makongamano anayoshiriki. Vyote hivyo vinaitangaza Tanzania moja kwa moja. Nashauri tusifanye mzaha na utafiti.

Tuelekeze fedha zaidi za bajeti ya taifa kwenye utafiti na tuhakikishe zinafikia walengwa. Utafiti huleta uelewa na fikra mpya na kutangaza taifa. Aidha, mwaka jana nilishinda tuzo ya mwanafunzi bora wa kimataifa upande wa utafiti chuoni kwetu.

Tulishinda watu watatu. Wengine ni kutoka Pakistan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Mimi nilikuwa mshindi wa kwanza. Lakini pia nilishinda tuzo ya mwanafunzi bora wa kimataifa katika michezo na utamaduni.

Hakuna siri zaidi ya kujituma na kupenda ninachokifanya. Ndoto zake Ndoto yangu ni kupata nafasi katika moja ya taasisi kubwa za wanyamapori hapa nchini kwetu niweze kushirikiana na wenzangu na serikali kwa jumla kwenye vitengo vya utafiti wa wanyamapori.

Hii itanisaidia kuendelea kufanya utafiti mwingi kadri ya uwezo ambao Mungu atanijalia. Naamini Tanzania bado kuna viumbe wengi ambao sisi wenyewe hatuwafahamu na dunia kwa ujumla.

Hizi ni ‘Tanzanite’ nyingine ziko porini zimetulia. Ndoto yangu nyingine ni kuwa na taasisi yangu binafsi itakayofundisha masuala ya utafiti wa wanyamapori ikishirikiana kwa karibu na taasisi za serikali.

Lakini pia furaha yangu itakuwa ni kuona Tanzania tunakuwa ndani ya nafasi tano za juu kwa watafiti wa wanyamapori duniani. Maisha ughaibuni Nimekaa China kwa takribani miaka saba na nusu hadi sasa.

Nilikwenda kwa mara ya kwanza mwaka 2012. Chuoni kwetu sasa tupo Watanzania watatu. Ni wachache kwa sababu nadhani hakuna mwamko wa kusoma masuala haya ya wanyamapori kwani chuo chetu kimejikita kwenye misitu na wanyamapori.

Nashukuru sana serikali ya China. Nitaipenda na kuitangaza vizuri popote niendapo duniani. Ni watu wazuri na wamekuwa wema sana kwangu. Changamoto zipo ila zinamezwa na mazuri.

Nimewahi kuajiriwa sehemu mbalimbali kwa ajira rasmi na zisizo rasmi nchini China. Miongoni mwa kazi hizo ni kuwa mtafiti mshiriki, mtafiti msaidizi kwenye vyuo tofauti . Nimefanya kazi zisizo rasmi kwa maana ya kuajiriwa katika hifadhi mbalimbali nchini China ikiwa ni sehemu ya masomo yangu.

Nazo ni hifadhi ya Hanma; Xilin Gol Steppe; Chuimilia; Hunchun; Mlima Changbai ; Shuanghe na Xiaobeihu. Tanzania inavyozungumziwa Tanzania inajulikana sana baina ya watu wenye umri mkubwa walau kuanzia miaka 48 kwenda juu.

Hii ni kwa sababu ya urafiki uliokuwapo kati ya Mwalimu Julius Nyerere na Mwenyekiti Mao Zedong. Ukitaja Tanzania kwa kundi hilo, watamtaja Nyerere, watataja reli ya Tazara na wanamalizia na nchi ya Zambia kwamba ni majirani zetu.

Pia hifadhi ya Serengeti inafahamika kiasi fulani hasa miongoni mwa wasomi. Vile vile Rais John Magufuli anatajwa zaidi na wasomi na wafanyabiashara. Kwa vijana, siyo wengi wanaofahamu Tanzania isipokuwa wale ambao ndugu zao wamebahatika kuja huku.

Nampongeza Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki. Anafanya kazi nzuri ya kuiwakilisha nchi yetu. Ni mnyenyekevu na mwelewa, anapokea kero muda wote. Matarajio yake Matarajio yangu ni mengi.

Kwanza ni kumalizia PhD yangu. Pili, ni kuhakikisha naendelea kufanya vizuri zaidi katika utafiti na kushirikiana na watafiti wengi wakubwa wa kimataifa kuendelea kuitangaza Tanzania kimataifa na kusaidia kutunza wanyamapori ambao ni zawadi kubwa kwa taifa letu.

Pia napenda sana siku moja nifanye kazi kwenye Shirika letu la Hifadhi za Taifa (Tanapa) niweze kutoa mchango wangu na uzoefu wangu wa nje ya nchi kwenye sekta ya uhifadhi na utalii.

Hili ni moja ya matarajio yangu makubwa. Nashauri viongozi wa Wizara ya Mali Asili na Utalii wawe karibu sana na Watanzania wanaoishi nje ya nchi. Watawapa taarifa za kutosha za namna ya kusaidia kutangaza nchi kupitia vivutio vya utalii.

Ombi langu lingine kwa serikali ni kwamba wafuatilie sana nje ya nchi tupo vijana wengi wazuri na wazalendo. Kijana wenu nina nguvu za kutosha kutumikia taifa letu hasa kwenye eneo la wanyamapori.

Nitumieni muda wowote niko tayari kufanya makubwa kwa taifa langu. Watu asiowasahau Watu walioniwezesha kufika hapa nilipo ni wengi. Lakini kwa uchache, mtu wa kwanza ni mama yangu.

Alisimama na sisi wanae hata pale baba yetu alipofariki akiwa na umri mdogo wa miaka 35. Bila mama kusimama nisingekuwa hapa nilipo. Mwingine ni baba yangu mdogo, Mzee Martin Mpemba.

Bila huyu kuchukua majukumu yake ya mzazi, nisingefika popote. Maana kwa mazingira ya kijijini wakati huo, elimu haikuwa kipaumbele sana. Alihakikisha analipia ada zetu bila kuchoka hadi nilipomaliza elimu ya sekondari. Mwingine ni kaka yangu , Dk Danford Mahwera ambaye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Yeye ndiye alinipa motisha nipende kupata matokeo ya juu chuo kikuu kwani naye alikuwa amefanya vizuri. Mwingine ni Dk Christine Noe wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliyenifanya nijikite kusoma wanyamapori.

Alivyogundua uwezo wangu akanipenda pia kwa kunipa ushirikiano mkubwa. Kuna kipindi nilimtembelea ofisini kwake kuomba ushauri kuhusu kusoma Shahada ya Uzamivu; akaniambia ‘chukua karatasi andika mwenyewe ni jambo gani unalipenda toka utotoni.

’ Nikakumbuka nilikuwa mwindaji mzuri utotoni na nilipenda sana wanyama. Nikamwandikia kisha akasema basi nafikiri ukisoma chochote kinachohusu masuala haya utafanya vizuri.

Bila kuwasahau ndugu zangu wote na familia yangu, akiwamo mdogo wangu Columbas, kwa ujumla kila mara wamekuwa wakinitia nguvu. Anachopenda, asichopenda Katika mahojiano na Hamenya ambaye sasa anaishi Arusha akisubiri kurudi China kumalizia masomo yake ya PhD, nabaini mambo anayopenda na asiyopenda.

Zamani alipendelea muziki. Ndiyo maana aliibuka kuwa mchezaji wa ngoma mzuri wakati akiwa sekondari hata akapewa tuzo katika Umoja wa Michezo kwa Shule za Sekondari (Umisseta).

Lakini sasa anapendelea kuangalia mpira wa miguu akisema hicho ndicho kilevi chake kikubwa. “Kwa maana sinywi pombe…Sijawahi kunywa pombe. Mpira naupenda sana na ndicho kitu kinachoniburudisha zaidi.”

Anataja timu anazoshabikia kwa Tanzania ni Yanga. Timu za nje ni Liverpool ya Uingereza ambayo ikifungwa, huhisi kuugua. Kitu kingine anachopenda ni siasa. Anasema siasa ni mfumo wa maisha ya watu.

“Wengine huniambia kwamba mimi ni mtaalamu mzuri hivyo niachane na mambo ya siasa nisaidie taifa. Jibu langu huwa ni hili, ukiona msomi anaingia kwenye siasa na anashindwa kusaidia taifa basi hiyo ni shida yake binafsi na siyo shida ya wasomi wote.”

“Mimi binafsi nina malengo makubwa na taifa hili, siku nikipata nafasi yoyote ya uongozi serikalini nina hakika nitaonesha mfano mzuri sana,” anasema

Hamenya akisisitiza kuwa ana ndoto kubwa kwa taifa taifa lake na kwamba ndiyo maana anafanya kila awezalo kuitangaza Tanzania kimataifa.

Hamenya anapenda pia kujenga urafiki na watu wengi zaidi duniani jambo analosema kuwa amefanikiwa kwani ana marafiki wa karibu anaoshirikiana nao mambo mbalimbali hasa kwenye sayansi na utafiti takribani katika mabara yote duniani.

Kuhusu mambo asiyopenda, Hamenya anasema “Kwa ujumla sipendi watu wavivu na wasiopenda maendeleo ya wenzao... Lakini pia sipendi watu na hasa viongozi wasiotimiza ahadi zao.”

“ NILIZALIWA miaka 29 iliyopita wilayani Temeke na kupata elimu ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi