loader
Dstv Habarileo Mobile
Picha

JPM afafanua mishahara ya watumishi wa umma

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli ameeleza serikali yake ilivyojali maslahi ya wafanyakazi kwa kipindi chote cha miaka mitano bila kutangaza huku akisisitiza kuwa hata watumishi wenyewe wanajua.

Alisema serikali yake haikutaka kudanganya wafanyakazi kuwa imewapandisha mishahara na kuwaacha wateseke kwa kupandishiwa bei ya bidhaa muhimu kama mafuta, nauli, vyakula na vitu vingine muhimu.

Akizungumza katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Mkendo Musoma Mjini, mkoani Mara, Magufuli alisema katika kipindi cha miaka mitano serikali yake imefanya mambo makubwa kuhakikisha wafanyakazi wanaboreshewa maslahi yao na kunufaika.

“Katika kipindi cha miaka mitano tumeajiri watumishi zaidi ya 61,000 wakiwemo walimu na madaktari. Leo hii wote wanaoitwa majalala. Tumejitahidi kusimamia wafanyakazi. Wakati tunaingia hata pensheni za wafanyakazi zilikuwa hazijalipwa tumelipa zaidi ya shilingi trilioni moja,” alisema. 

Alisema serikali pia imepunguza utitiri wa mifuko ya hifadhi ya jamii kutoka sita hadi kuwa miwili iwahudumie vizuri wafanyakazi. 

“Tumerekebisha kodi inayolipwa kutokana na mapato ya Pay as You Earn (Paye) kutoka asilimia 11 hadi tisa. Tumelipa malikimbizo ya wafanyakazi zaidi ya Sh bilioni 500 lengo kuhakikisha wafanyakazi wote wa zamani na wapya wafaidike na kazi zao,” alisema.

Aliongeza kuwa “Mtu anakuja anasema mbona hamjapandishwa mishahara, ukishampandisha mtu kutoka daraja fulani kwenda daraja fulani mshahara wake haubadiliki? Ukilipa malimbikizo zaidi ya bilioni ( Shilingi) 500  hiyo si fedha? Ukimpunguzia Paye hujamuongezea mshahara?”

Alisema suala la kuwadanganya wafanyakazi kuwa wanaongezewa mshahara halafu kesho yake mafuta yanapanda, unga unapanda, nauli zinapanda kila kitu kinapanda kwa CCM limepitwa na wakati.

“Lakini nilishawaahidi wafanyakazi kwamba kabla sijamaliza muda wangu nitawapandishia mishahara. Unapopandisha mishahara lazima uangalie vigezo muhimu vya uchumi wa nchi. Huwezi ukaacha kujenga reli kwa gharama ya trilioni saba itakayoleta uchumi mkubwa lakini pia hata wafanyakazi wataipanda, ukasema unaenda kupandisha wafanyakazi mishahara,” alieleza.

Alisema pia haiwezekani kuacha kujenga vituo vya afya, kulipia elimu bure ambayo watoto watakaosoma ni wa watanzania wote kwa ajili ya kuongeza mshahara.

“Tumejenga nchi nzima vituo vya afya 887 wanaotibiwa si wakulima na wafanyabiashara bali hata wafanyakazi. Tuliamua hiyo fedha iende kujenga vituo vya afya, zahanati zaidi ya 1,000 na hospitali 99 zimejengwa. Hospitali za rufaa zaidi ya tatu hizi zinatibu pia wafanyakazi na watoto wao,” alifafanua.

Alisema serikali iliamua kutoa elimu bure kwa watoto kuanzia  darasa la kwanza hadi sekondari na mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu imeongezeka hadi kufikia Sh bilioni 450 ili mtoto wa maskini apate mkopo na fedha zilizotumika ni Sh trilioni 1.06.

“Kupanga ni kuchagua tuliamua watoto wasome bure kwanza, na wanaosoma bure na ni wa wakulima, wafanyakazi, wafugaji na wakulima,” alisema.

Bila kutaja jina, Rais Magufuli alisema anashangazwa na mtu anayedai kuwa anawapenda wafanyakazi na kwamba atawaongezea maslahi, lakini baadaye anawaita majalala. 

“Wafanyakazi mmeyaona wenyewe kabla jua halijazama, jipangeni jiulizeni mlikotoka na mnakoenda mpaka uchaguzi unakwisha mtapewa majina ya kutosha. Uchaguzi si mwisho wa maisha ni process (mchakato)tusijenge chuki ya kudhalilisha watanzania wengine ambao baadaye tutahitaji kura zao,” alisema.

Kumuenzi Nyerere

Aliahidi katika utawala wake endapo atachaguliwa kuendelea kuwa rais wa Tanzania awamu yake pili, atahakikisha yale aliyoyapanga baba wa taifa (Mwalimu Nyerere) kuyatimiza anayatimiza kwa kasi kubwa ikiwemo kuuenzi mkoa aliotoka baba wa taifa.

Alitaja maendeleo yaliyofanyika mkoani Mara ikiwemo kujengwa kwa Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ambayo ujenzi wake ulianza tangu mwaka 1975. Alisema chini ya serikali yake, Agosti, mwaka huu ilianza kufanya kazi na mtoto mmoja amezaliwa anaitwa Julius.

“Yale yaliyobaki kwenye hospitali hiyo tutayamaliza shilingi bilioni 15 zilitolewa kumalizia ujenzi huo uliokwama takribani miaka 30. Najua kuna kifaa cha AVR hakipo kitakuja ili figo ziwe zinasafishiwa Musoma badala ya watu kupelekwa Dar es Salaam,” alisema.

Alitaja mipango mingi iliyopo kwenye ilani ya CCM ya mwaka 2020/25 kwa mkoa wa Mara ikiwamo ujenzi wa barabara, hospitali saba, vituo nane vya afya, zahanati 27 ambavyo vyote vimegharimu Sh bilioni 25.1. wamejenga shule za  Sekondari 35, Msingi 102, maboma ya madarasa 646, nyumba za walimu 158 na kukarabati vyuo viwili vya ualimu Tarime na Bunda.

“Tumekarabati meli tano na kutengeneza moja mpya Mwanza. Tunataka turudishe utaratibu wa baba wa taifa, meli ilikuwa inakuja mpaka Musoma. Bilioni 152 tumekarabati meli. Meli Victoria na MV Mwanza ziwe zinatoka Kisumu-Musoma-Kemondo-Uganda-Kisumu.,” alisema.

MGOMBEA wa nafasi ya ubunge katika jimbo la ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

2 Comments

 • avatar
  Nyakalo
  06/09/2020

  Mapunjo Mzee hujalipa, mwalimu aliepanda drj 2013 Aprli hatjalupwa Na utawala wako tunambiwa sio wa kulipa madeni ukipanda drj shukuru lkn Deni la mapunjo halilipiki

 • avatar
  Bahati Onesmo
  07/09/2020

  Big up President Magufuli for all you have done to us as Tanzanians. Don't give up because God is with and we will all stand with you.

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi