loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mtanziko wa kusababishiwa na ulimwengu

Wiki iliyopita, tuliangalia mtanziko wa maadili wa kujisababishia mwenyewe (a self-imposed moral dilemma) ili vilevile tuweze kuielewa vizuri aina hii ya mtanziko, kuanzia kwenye maana yake, maelezo yake na mifano yake katika utumishi wa umma.

Katika toleo hili, tutauchambua Mtanziko wa kusababishiwa na mambo ya ulimwengu (A Worldimposed moral dilemma), ili vilevile tuweze kuielewa vizuri aina hii ya mtanziko, kuanzia kwenye maana yake, maelezo yake na mifano yake katika utumishi wa umma.

Kwa ujumla, mtanziko wa kusababishiwa na mambo ya ulimwengu (A World-imposed moral dilemma), unaweza kujitokeza pale ambapo kuna matukio yamejitokeza ulimwenguni na kumfanya mtumishi wa umma kupata mtanziko kwa maana ya mambo mawili au zaidi ya kuchagua na yote yakiwa na athari zake.

Kuna mifano mingi sana ambayo inaweza kuangaliwa kwa sababu kila mtu katika maisha yake anakutana na mtanziko unaosababishwa na matukio mbalimbali ulimwenguni na kwa wakati huo inakuwa vigumu sana kupata chaguo zuri kuliko lingine katika jitihada za kutatua tatizo.

Hapa nitajaribu kutumia mifano mitatu ya mazingira waliyokabiliana nayo viongozi wetu wakuu watatu kwa maana ya Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi na John Magufuli katika nyakati tofauti na namna walivyojinasua katika mitanziko inayotokana na mambo au matukio ya ulimwengu.

Kuanzia mwaka 1986 dunia ilikumbwa na mabadiliko makubwa ya kiasiasa na kiuchumi ambapo nchi nyingi ikiwa ni pamoja na Tanzania, zililazimika kwenda sambamba na mabadiliko hayo ya dunia.

Kabla ya mabadiliko hayo Tanzania ilikuwa chini ya mfumo wa chama kimoja cha siasa na kwa maana hiyo watanzania walitakiwa kupiga kura ya maoni ili kuona kwa kiasi gani watanzania walikuwa wanataka kuachana na mfumo wa chama kimoja na kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi.

Matokeo ya kura ya maoni yalionesha kuwa asilimia 80 ya watanzania walikuwa wanatamani kuona Tanzania inaendelea kuwa na mfumo wa chama kimoja, wakati asilimia 20 waliona ni vema Tanzania ikaingia katika mfumo wa vyama vingi.

Hali hii ilileta mkanganyiko mkubwa kwa vile kubaki katika mfumo wa chama kimoja ilikuwa ni kwenda kinyume na mabadiliko ya dunia na pia kuingia katika mfumo wa vyama vingi ilikuwa ni kwenda kinyume na mapenzi ya watanzania walio wengi.

Kutokana na ugumu wa mtanziko huu, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alilazimika kuingilia kati na kutumia ushawishi wake mkubwa sana kuwaelekeza watanzania kuingia katika mfumo wa vyama vingi kwa vile isingekuwa busara kwa watanzania kwenda kinyume na mabadiliko ya dunia na pia siyo vema kuwapuuzia wale ambao wangependa kushiriki siasa za Tanzania kupitia vyama vingine vya siasa tofauti na CCM.

Katika kipindi hicho hicho dunia ilikuwa ikikabiliwa na misimamo mikali ya kidini ikihusisha kwa kiasi kikubwa dini za kikristo na kiislamu.

Katika mazingira haya, kikundi cha watu kilichojitambulisha na uislamu kilivamia mabucha ya nyama za nguruwe na kusababisha uharibifu mkubwa na upotevu wa mali katika maduka hayo.

Hali hii kwa Rais wa Tanzania wakati huo, Ali Hassan Mwinyi ilikuwa ni mtanziko mkubwa sana kwa sababu alikuwa akiongoza watanzania wenye imani tofauti, ikizingatiwa kuwa wapo walioamini kuwa matumizi ya nyama ya nguruwe yalikuwa ni haramu na walitamani kuona nchi inaondokana kabisa na matumizi hayo.

Lakini vilevile wapo waliokuwa wanaona matumizi hayo ni sawa na kwa maana hiyo walipenda kuona matumizi yakiendelea. Rais Ali Hassan Mwinyi aliweza kuruka kiunzi hicho kigumu kwa kuwaambia watanzania kwamba kila mtu ana uhuru wa kula chochote anachotaka alimradi havunji sheria za nchi.

Jina la mzee Ruksa lilianza kipindi hiki pale aliposema kama kuna mtu anataka kula chura ni ruksa. Kama kawaida amani imeendelea kutamalaki licha ya tofauti katika anuai za jamii na watu wengi wanaweza kujifunza kwetu.

Kwa mfano, ukikuta watu wanafuturu pamoja usijidanganye kwamba wote ni waislamu na ukikuta watu wako harusini kanisani usije ukadhani kwamba wote ni wakristo humo.

Mfano mwingine na wa mwisho umetokea siku za karibuni chini ya Rais John Magufuli, ambapo nchi imekuwa katika tishio kubwa la ugonjwa wa mapafu unaotokana na virusi vya Corona (COVID19).

Katika mazingira haya magumu ambapo ugonjwa ni mpya na haujulikani sana na watu mbalimbali ikiwa ni pamoja na wataalamu, yalitokea makundi mawili makubwa.

Kundi la kwanza lilikuwa likisisitiza hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na watu wote kujifungia ndani na kundi la pili likiona kuwa kujifungia kungeweza kuleta madhara makubwa zaidi kiuchumi na pengine kusababisha vifo vingi zaidi.

Hali hii ilileta mtanziko mkubwa sana kwa sababu kujifungia kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kuleta madhara ikiwa ni pamoja na vifo na vilevile kutojifungia kulikuwa kunapelekea kuleta madhara.

Kutokana na busara zake na ushirikiano wake na wataalamu wetu, Rais Magufuli aliamua kufunga shule na vyuo na kusisitiza umuhimu wa kuchukua hatua zingine kama vile umbali wa mtu na mtu lakini alikataa kata kata kuamuru watu kujifungia ndani.

Baadaye mataifa mengi duniani yalianza kuona madhara ya watu kujifungia pengine ni makubwa sana kuliko madhara yanayotokana na kutojifungia mtazamo huu una maana kubwa zaidi kwa nchi zenye uchumi mdogo kama nchi zetu kusini mwa jangwa la Sahara.

MENO meupe na safi ni moja ya vitu vinavyoongeza mvuto ...

foto
Mwandishi: Dk Alfred Nchimbi - 0754658731

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi