loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mfahamu Khadija, mtoto wa Rungwe 'Mzee wa Ubwabwa'

Msomi aliyejikita kwenye biashara ya kuuza chakula

*Ana Shahada ya Uongozi kutoka Malaysia

*Ana ndoto ya kumiliki mgahawa wa kimataifa

NDOTO ya kila mhitimu ni kupata ajira ili aweze kufanyia kazi kile alichosomea. Hata hivyo  sio wote wanaotimiza ndoto hiyo kwani wapo wanaoamua kujiongeza na kuamua kujiajiri wenyewe badala ya kusubiri ajira.

Khadija Rungwe (32) ni mhitimu wa Shahada ya Uongozi wa Biashara, aliyekataa kazi ya kuajiriwa na kufanya biashara ya kuuza chakula inayomfanya kuendesha maisha yake.

Msomi huyu aliyezaliwa na kukulia jijini Dar es Salaam,  anakiri kuwa mmoja wa wadau wake wakubwa katika biashara yake ya chakula ni  baba yake Hashimu Rungwe ambaye ni miongoni mwa wagombea wa kiti cha Urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu kupitia Chama cha Chauma..

Rungwe anasifika kwa sera yake ya chakula kwa wanafunzi mashuleni, jambo ambalo Khadija anasema pengine baba yake amevutiwa na kuamua kutumia sera hiyo kutoka na kufurahishwa kwake na namna yeye (Khadija) anavyotoa huduma hiyo kwa makundi ya aina mbalimbali.

Khadija anasema amesoma hadi kuhitimu elimu ya kidato cha sita katika Shule ya Academy iliyopo Mikocheni na baadaye kwenda nchini Malaysia na kujiunga na Chuo Kikuu cha Binary, alipohitimu Shahada yake ya Uongozi wa Biashara katika nyanja ya ujasiriamali.

Anasema baada ya kuhitimu Chuo mwaka 2011, alirudi nchini na kufanya kazi katika mashirika tofauti lakini zaidi katika Shirika la Agakhan, upande wa Shule ya Sekondari ya Mzizima kama Katibu Muhtasi wa shule hiyo  alipofanya kazi kwa miaka miwili na nusu kuanzia Agosti mwaka 2011 hadi 2014.

Khadija anasema wakati wote akiwa kazini hapo akili yake wakati wote ilikuwa ikimtuma kufanya biashara ya chakula ambayo kwa msisitizo wake anasema alikuwa akiipenda kutoka  moyoni mwake tangu akiwa  mtoto.

Kwa mujibu wa Khadija baada ya kufanya kazi ya Ukatibu Muhtasi kwa kipindi hicho, aliamua kuacha kazi na kuingia rasmi katika biashara ya kupika na kuuza chakula na kusambaza maeneo mbalimbali ikiwemo katika ofisi tofauti na kujikuta akipata watu wengi waliokuwa wakimuunga mkono na kuwa wateja wake.

Msomi huyo ambaye ni mama wa watoto watatu, anasema hakujali kuhusu elimu ya Chuo Kikuu aliyokuwa nayo wala jambo jingine lolote ikiwemo maisha mazuri kiasi waliyokuwa nayo wazazi wake, kwake kuuza chakula ni jambo alililokuwa akilipenda wakati wote.

“Hii ni suala lililokuwa ndani ya moyo wangu, hata nilipokuwa Mzizima nilikuwa nafanya biashara kidogo kidogo kwa kuuza mishikaki, mihogo huku zikiendelea na kazi na kujipatia fedha zilizosaidia kuendesha maisha ya familia yangu,” anasema Hadija.

Khadija ambaye ni mtoto wa tano kati ya watoto saba wa Rungwe mzaliwa wa Kigoma Ujiji na mama Tunu Rungwe Mbondei mzaliwa wa Muheza, Tanga anasema kwa kiasi kikubwa mafanikio aliyoyapata katika biashara  ya chakula anayoifanya ni pamoja na kutiwa moyo na mume wake Amani Tesha kiasi cha kujiona mwenye bahati kubwa.

Anasema baadaye mumewe alimchukua na kumuajiri katika kampuni yake ya 'Catering' kwa lengo la kumuongezea juzi alipodumu kwa kipindi cha miaka miwili hadi mwaka jana alipoamua kuanzisha biashara yake mwenyewe baada ya kujiona kuwa amekomaa.

“Nikiwa chini ya uongozi wa kampuni ya mume wangu nilijifunza namna tofauti ya kufanya biashara ya chakula ikiwa ni pamoja na kutafuta zabuni za usambazaji vyakula katika kampuni na sherehe mbalimbali na kujikuta nikipata ujuzi mkubwa ulionifanya nifike hapa nilipo sasa,” anasema.

Anasema hakuna urahisi katika biashara ya  uuzaji chakula, inachotakiwa zaidi ni kujituma na anasisitiza kuwa kwake imekuwa kazi nyepesi kwa sababu anapenda kupikia watu na kufurahisha wateja na anaamini kila kitu kinawezekana kama kukiwa na nia.

Khadija ambaye kwa sasa anamiliki mgahawa wake unaoitwa All Season Kitchen uliopo mtaa wa Chole, Masaki jijini Dar es Salaam, anasema malengo yake ni kuwa na kampuni kubwa ikibidi hata kuja kumiliki mgahawa wa kimataifa utakatoa huduma kwa watu wa mataifa mbalimbali.

Anasema kupitia mgahawa wake huo mbali na kumuingizia kipato yeye binafsi pia umekuwa ukiwawezesha vijana wenzake anaofanya nao kazi mahali hapo kuendesha maisha yao kutokana na kipato wanachokiingiza.

Mbali na hatua hiyo, anasema atahakikisha elimu na ujuzi alionao katika mapishi na biashara ya chakula kwa ujumla anaipekeleka kwa wanawake wenzie na wale wote wanaohitaji ili waweze kunufaika nayo kama ambavyo ananufaika yeye sasa.

Anasema ili kuyafikia makundi hayo, atakuwa akitoa elimu  kupitia njia ya televisheni na mitandao ya kijamii ili kutimiza dhamira yake hiyo na kuongeza kuwa anaamini kwa kupitia hatua hiyo anaweza kuwanufaisha watu wengi na kujikwamua umasikini.

 

Khadija anatoa wito kwa wahitimu na vijana wenzake kutosubiri  ajira zaidi na badala yake watengeneze mazingira ya kujiajiri ili kuendesha maisha yao na kujiingizia kipato badala ya kusubiri kuajiriwa.

Aidha Khadija anasema sera ya chakula bure mashuleni  inayotumiwa na  mzazi wake Rungwe inamaana kubwa kwa kuwa imelenga kuhakikisha afya za watoto zinakuwa imara wakati wote na kuwawezesha kutimiza ipasavyo majukumu yao shuleni.

Anasema anamuunga mkono Rungwe kwa asilimia mia moja katika harakati zake za kisiasa na kuwaomba wananchi kumchagua ili aweze kutekeleza yale yote aliyoyakusudia kuyafanya kipindi atakapochaguliwa.

“Sikuwahi kushiriki kampeni zote za mzee miaka yote ya nyuma kwa sababu nilikuwa nje ya nchi, namshukuru Mungu kampeni za mwaka huu zimenikuta nikiwa hapa nchini hivyo nitashiriki kikamilifu,” anasema Khadija ambaye alikuwepo katika ufunguzi wa kampeni za Rungwe zilizofanyika Manzese, Jumamosi ya wiki iliyopita.

Anasema anaamini baba yake atafanya vizuri akiwa na chama hicho alichokianzisha mwenyewe baada ya kujiengua kutoka Chama cha NCCR-Mageuzi kwa kuwa kinazidi kujengeka siku hadi siku.

Mwanadada huyo anasema ipo siku chama cha Chauma kitakuja kuwa chama kikubwa cha upinzani hasa kutokana  na mwenendo wake wa sasa unakiwezesha kupata mashabiki kila uchao hususani katika kipindi hiki cha uchaguzi.

Khadija akiwa hayupo katika shughuli zake za ujasiriamali hupenda kusoma vitabu vya mapishi, kuangalia televisheni hususani tamthilia mbalimbali, kucheza mpira na kuogelea.

 

 

 

 

 

 

 

WANAWAKE wamekuwa ni chachu kubwa ya ...

foto
Mwandishi: Oscar Job

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi