loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Serikali inavyotekeleza miradi kuhifadhi mazingira

SIKU ya Kimataifa ya Kuhifadhi Tabaka la hewa ya Ozoni huadhimishwa duniani kote Septemba 16 ambapo kwa mwaka huu maadhimisho hayo yanafanyika jijini Dodoma, Jumatano kesho kutwa.

Ozoni ni tabaka la hewa lililopo kwenye angahewa ya juu, takribani kilometa 15 hadi 30 juu ya ardhi na kazi yake kubwa kuchuja kiwango kikubwa cha mionzi ya jua isifike kwenye uso wa dunia.

Maadhimisho haya yanachagizwa na kaulimbiu ya ‘Miaka 35 ya Kuhifadhi Tabaka la Ozoni kwa Manufaa ya Afya ya Binadamu na Mazingira’. Kimsingi kaulimbiu hii inatukumbusha umuhimu wa kulinda na kuhifadhi tabaka hilo kwa kupunguza uzalishaji na matumizi ya kemikali zinazomong’onyoa tabaka hili.

Baadhi ya kemikali zinazomong’onyoa tabaka la ozoni pia huchangia katika kuongezeka kwa joto duniani, hivyo kupunguza matumizi ya kemikali hizi kunachangia kwa kiasi kikubwa katika kukabiliana na ongezeko la joto duniani na mabadiliko ya tabianchi Zipo juhudi mbalimbali zinazofanywa na Ofisi ya Makamu wa Rais za kuhifadhi mazingira zikiwemo utekelezaji wa miradi ya kitaifa ya kimkakati inayochangia katika hifadhi ya mazingira.

Ofisi imechukua hatua mbalimbali kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zikiwemo ujenzi wa ukuta wa Pangani (Tanga) wa urefu wa mita 950 na katika ufukwe wa Ocean Road na Kigamboni za urefu wa mita 1,335 (Jijini Dar es Salaam).

Pia imepandwa mikoko katika Manispaa ya Kinondoni-Mbweni (hekta 1), Manispaa ya Kigamboni (hekta 40), wilaya ya Kibiti/Rufiji Delta (hekta 1,000), wilaya ya Pangani (hekta 10), eneo la Kisakasaka (Unguja) hekta 8, eneo la Kilimani (Unguja) hekta 4 na eneo la Kisiwa Panza (Pemba) hekta 200.

Katika eneo la hifadhi ya Misitu na upandaji Miti, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kupitia kampeni ya Kijanisha Dodoma, jumla ya miti 1,402,812 ilipandwa kati ya mwaka 2018 hadi 2020 na kati ya hiyo miti 1,146,098 sawa na asilimia 81.7 imepona.

Wadau walioshiriki kufanikisha zoezi hili ni pamoja na Mfuko wa Dunia wa Hifadhi ya Wanyamapori Tanzania (WWF), Vodacom Foundation Tanzania, Halmashauri ya Jiji la Dodoma (CCD), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), shule za msingi na sekondari, vyuo vya elimu ya juu, Jeshi la Magereza Tanzania na Jeshi la Polisi Tanzania.

Aidha, katika utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Upandaji Miti ambapo kila halmashauri inatakiwa kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka, upandaji miti umeongezeka katika baadhi ya maeneo nchini kutokana na msukumo wa viongozi katika maeneo husika. Kwa mfano katika Mkoa wa Tabora jumla ya miti 5,858,453 ilipandwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2016 hadi 2020.

Kati ya hiyo miti 4,452,424 imestawi ambayo ni asilimia 76. Kwa kipindi cha mwaka 2018/19 Serikali iliweka malengo ya kupanda miti 313,196,500 katika mikoa yote nchini ambapo miti iliyopandwa ni 209,767,815 sawa na asilimia 72.6 ya lengo zima.

Kati ya hiyo, miti 153,288,845 sawa na asilimia 73.1 ya miti yote iliyopandwa imestawi. Hatua nyingine ni uchimbaji wa visima 10 katika wilaya ya Bagamoyo, ujenzi wa makinga bahari (groynes) matano katika eneo la Kilimani (Unguja) na ujenzi wa kuta mbili za bahari katika eneo la Kisiwa Panza kisiwani Pemba.

Ofisi ya Makamu wa Rais imeratibu Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na kuongeza usalama wa chakula katika maeneo kame ya Tanzania unalenga kurejesha ardhi iliyoharibika na kuongeza usalama wa chakula katika maeneo kame ambapo unatekelezwa katika Wilaya za Magu, Nzega, Mkalama, Kondoa na Micheweni kwa upande wa Zanzibar na unawanufaisha wakazi takribani 70,000.

Pia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia mifumo ikolojia kutoka Mfuko wa Mazingia wa Dunia (Global Environmental Facility- GEF) wenye lengo la kuongeza uwezo wa wananchi kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi kwa njia za mifumo ikolojia na kuwezesha njia mbadala za kujiongezea kipato.

Aidha, kwa kipindi cha mwaka 2018/19 serikali iliweka malengo ya kupanda miti 313,196,500 katika mikoa yote nchini. Miti iliyopandwa ni 209,767,815 sawa na asilimia 72.6 ya lengo zima. Kati ya hiyo, miti 153,288,845 sawa na asilimia 73.1 ya miti yote iliyopandwa imestawi.

Serikali iliandaa na kutekeleza Programu ya Taifa ya kuondosha matumizi ya kemikali hizo nchini ambapo shughuli mbalimbali zimefanyika zikiwemo kuandaa Kanuni za Usimamizi wa Kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni za Mwaka 2007.

Pia iliratibu mafunzo kwa mafundi mchundo wanaohudumia viyoyozi na majokofu zaidi ya 500 kuhusu njia bora za kuhudumia vifaa hivyo bila kuathiri tabaka hilo pamoja na kutoa mafunzo kwa wakufunzi wa vyuo vya ufundi zaidi ya 100 kuhusu njia bora za kuhudumia vifaa hivyo bila kuathiri tabaka la ozoni.

Aidha, vitambuzi 18 (refrigerant identifiers) vya kemikali zinazomong’onyoa tabaka la ozoni vilisambazwa katika vituo vya forodha vilivyo mipakani kwa ajili ya kusadia kutambua kemikali zinazodhibitiwa chini ya Itifaki Montreal wakati zinapoingizwa nchini.

Jitihada nyingine iliyofanywa ni kununua na kusimika mashine 25 za kunasa na kurejeleza gesi chakavu za majokofu na viyoyozi katika karakana 20 na vituo vitano vya kikanda katika vyuo vya VETA vya Mwanza, Chang’ombe jijini Dar es Salaam, Kigoma, Mbeya na Mkokotoni visiwani Zanzibar.

Serikali ilitoa mafunzo kwa maofisa takriban 172 kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (ZEMA), Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuhusu udhibiti wa kemikali zinazomong’onyoa tabaka la ozoni.

Aidha, vyuo vya VETA, Chuo Kikuu cha Mbeya cha Sayansi na Teknolojia (MUST) na Chuo cha Kodi viliwezeshwa kupitia mitaala ya kufundishia kwa kozi zinazohusiana na uhudumiaji wa majokofu, viyoyozi na mitambo ya kupoozea pamoja na udhibiti wa kemikali zinazodhibitiwa chini ya Itifaki ya Montreal.

Miradi ya kimkakati Serikali ya Awamu ya Tano imewekeza katika miradi mikubwa ya umeme ikiwemo ujenzi wa Bwawa la kuzalisha Umeme la Julius Nyerere Hydropower Station lenye uwezo wa kuzalisha Megawati (MW) za umeme zaidi ya 2,115.

Umeme huu utapatikana kwa bei nafuu na hivyo kuwezesha wananchi wa kawaida na taasisi kutumia umeme kama nishati ya kupikia na shughuli nyingine. Usambazaji wa umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umefikia vijiji zaidi ya 9,000 sawa na asilimia 80 ya lengo la kufikia vijiji 12,268 vya Tanzania Bara.

Pamoja na yote yaliyofanyika, kama sehemu ya Jumuiya ya Kimataifa, hadi sasa Tanzania imeweza kupunguza zaidi ya tani 216 sawa na asilimia 86 ya kiasi cha matumizi ya kemikali zinazomong’onyoa tabaka la ozoni.

Lengo letu ni kuondosha kabisha matumizi ya kemikali hizi nchini kufikia mwaka 2030. Hadi sasa jitihada za utekelezaji wa mikataba ya kulinda tabaka la Ozoni zimechangia kupunguza kiasi cha asilimia 98 (takribani tani milioni 1.8) ya uzalishaji na matumizi ya kemikali zinazomong’onyoa Tabaka hili.

Hivyo, matokeo ya tafiti mbalimbali yamethibitisha kuwa utekelezaji wa mikataba hii umechangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa uzalishaji na matumizi kemikali zinazoharibu tabaka la ozoni angani.

Inakadiriwa kuwa, iwapo jitihada hizi zitaendelea kama ilivyo sasa, litarudi katika hali ya kawaida ifikapo katikati ya karne hii. Ikumbukwe kuwa Novemba 2019 Tanzania iliridhia Marekebisho ya Kigali yenye lengo la kupunguza na baadae kuondosha uzalishaji na matumizi ya kemikali ambazo hapo awali zilikuwa ni mbadala wa kemikali zinamong’onyoa tabaka hilo na baadae kugundulika kuchangia katika ongezeko la joto duniani na mabadiliko ya tabianchi.

Marekebisho haya yalipitishwa na nchi wanachama wa itifaki ya Montreal mwaka 2016, mjini Kigali Rwanda na kupitishwa kwa marekebisho haya kutachangia katika jitihada za kukabiliana na kuhimili mabadiliko ya tabianchi.

 

Mwandishi wa makala haya ni ofisa habari wa Ofisi ya Makamu wa Rais.

foto
Mwandishi: Robert Hokororo

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi