loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ubora wa barabara unaboresha kilimo, biashara Shinyanga

"WAKALA huu tunaouzindua leo utakuwa na manufaa makubwa kwa ustawi wa nchi yetu kwa kuongeza chachu ya uzalishaji mali mashambani kutokana na urahisi wa kufika sokoni, utashusha bei ya vyakula mijini na bidhaa za viwandani vijijini kutokana na gharama za usafirishaji wa mazao kutoka mashambani na bidhaa za viwandani kutoka mijini kupungua,” hayo ni maneno aliyoyasema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akizindua Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Oktoba 12, 2017 mjini Dodoma.

Miaka takribani mitatu tangu Waziri Mkuu aseme hayo, maneno yake yanatimia na hilo linaweza kuthibitishwa na wakazi wa mkoa wa Shinyanga kwa namna ambavyo mambo mengi yamefanywa na Tarura katika kipindi kifupi, mintarafu suala zima la uboreshaji wa barabara za mijini na vijijini.

Akizungumzia hilo, Baraka Mina, ameandika kwenye mtandao wa Jamii Forum kwamba barabara nyingi za mkoa wao zimebadilika katika kipindi kifupi na maeneo mengi ambayo yalikuwa hayapatiki vyema sasa yanapitika.

“Katika Manispaa ya Shinyanga barabara nyingi zimeboreshwa kwa kiwango cha lami safi na imara. Unasafiri bila shida huku ukikumbuka idadi ya ng’ombe ulizo nazo,” anaandika Mina.

Shughuli za kiuchumi

Wakazi wa mkoa wa Shinyanga wanajishughulisha zaidi na kilimo pamoja na ufugaji. Kwa upande wa kilimo cha biashara, zao kuu wanalolima ni pamba na mazao ya chakula ambayo wakati mwingine pia hutumika kama mazao ya biashara ni mhogo, mpunga, karanga na mahindi.

Kama ilivyo kwa mikoa mingi ya Kanda ya Ziwa, wakazi wa Shinyanga ambao wengi wao ni wa kabila la Kisukuma wanafuga ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku.

Mkoa huo pia umebarikiwa kuwa na madini ya aina mbalimbali, hususani dhahabu na almasi ambayo yanachimbwa zaidi katika mgodi wa Mwadui.

Maeneo mengi yafunguka

Kuanzishwa kwa Tarura, kumesababisha maeneo mengi ya mijini na vijijini mkoani Shinyanga kuendelea kufunguka na hivyo kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mazo ya wakulima.

Mratibu wa Tarura mkoani Shinyanga, Dastan Kishaka anasema wakala unafanya shughuli zake katika halmashauri sita, zenye jumla ya mtandao wa barabara uliohakikiwa wa kilomita 5,207.32.

Anasema barabara za kiwango cha lami zilizo chini ya Tarura ni kilomita 36.28, za changarawe kilomita 1,392.30 na barabara za udongo ni kilomita 3,778.75.

Anasema nguvu kubwa imekuwa ikielekezwa kwenye matengenezo ya barabara za udongo ili kufikia kiwango cha changarawe na zile za changarawe kuzifanya za lami kadiri ya fedha inavyoruhusu.

Mratibu huyo anasema kwa mwaka wa fedha 2019/2020 mkoa ulipanga kufanya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilometa 603.75 kwa gharama za Sh milioni 9,438.64.

Anasema kilometa 3.35 za barabara zinajengwa kwa kiwango cha lami kwa maana ya halmashauri za Kishapu (km 1), Ushetu (km 1) na Msalala (km 0.85km) kwa fedha zinazotokana na mfuko wa ahadi za Rais John Magufuli na km 0.5 zinajengwa Kishapu kwa fedha za mfuko wa barabara.

“Mpaka sasa jumla ya km 368.52 za barabara zimetengenezwa kwa thamani ya Sh milioni 3,992.40 ambazo zimeshalipwa,” anasema.

Kishaka anasema hadi kufikia Juni 2020, Mkoa wa Shinyanga uliingia mikataba mitatu ya matengenezo ya dharura yaliyogharimu Sh milioni 307.21 katika Mji wa Kahama, Kishapu na Ushetu. Anasema utekelezaji wa mradi hiyo umekamilika kwa asilimia 100.

Barabara zilizohusika na ukarabati katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu na kugharimu Sh miloni 29.96 ni Mhunze-Lubaga-Tuta, Mhunze-Lubaga-Ukuta/Retaining na Mhunze-Lubaga.

Anasema barabara zilizoshughulikiwa katika halmashauri ya Mji wa Kahama ni za Inyanga – Nyashimbi, Chansi 1 & 2 na barabara ya Kanu yenye urefu kilometa mbili. Gharama zilizotumika kwa mujibu wa mratibu huyo ni Sh milioni 200.45. Barabara iliyotengenezwa anasema ni ya Uyogo - Ulowa – Ihata katika Halmashauri ya Ushetu iliyogharimu Sh milioni 76.8.

Anasema kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Tarura Shinyanga imefanya matengenezo ya kawaida kwa kuchonga barabara zilizoharibiwa na mvua zilizonyesha wakati wa masika.

“Barabara ziliweza kupitika kwa kuzirudisha katika hali yake ya kawaida kwa njia ya nguvu kazi (force account) katika Halmashauri za Manispaa ya Shinyanga na Wilaya ya Ushetu,” anasema.

Anafafanua kwamba jumla ya kilometa 36 zimejengwa katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Shinyanga na kilometa nyingine 20.5 zimefanyiwa kazi katika halmashauri ya Ushetu kwa gharama ya Sh milioni 95.00.

“Juni 2020 tulipokea Sh 7,182.63, sawa na asilimia 92.10 ya bajeti yetu ya 2019/2020 kutoka Mfuko wa Barabara kwa matengenezo ya kawaida, sehemu korofi, muda maalumu, madaraja na makaravati pamoja na fedha za usimamizi wa miradi.

Anasema kwa mwaka 2020/2021 Mkoa wa Shinyanga umepitishiwa bajeti ya Sh milioni 7,764.78l na kwamba kati ya fedha hizo, Sh milioni 7,628.78 ni fedha za mfuko wa barabara na shilingi milioni 136.00 ni fedha ya maendeleo kwa ajili ya halmashauri ya Ushetu.

“Jumla ya kilometa 673.68 zitakarabatiwa katika mkoa wetu wa Shinyanga, makaravati 226, mitaro ya maji ya mvua yenye urefu wa mita 4,500, madaraja manne pamoja na daraja moja la chini (solid drift) yatajengwa,” anasema.

Ongezeko la magari mazito

Anasema ukuaji wa haraka wa miji, biashara na migodi wilaya ya Kahama na Manispaa ya Shinyanga zimesababisha kuongezeka kwa watu na magari ya uzito tofauti na uwezo wa barabara zilizojengwa miaka ya nyuma.

Anasema barabara za pembezoni zinazoelekea migodini ndizo huathirika mara kwa mara kutokana na kupitwa na magari yenye uzito mkubwa yakiwa yamebeba mchanga wa madini na hivyo kuchangia kuharibu barabara.

Changamoto

Uelewa mdogo wa sheria ya barabara kwa wananchi na hivyo kuingilia maeneo ya hifadhi ya barabara kwa kujenga majengo mbalimbali anasema ni moja ya changamoto zinazowakabili.

hangamoto nyingine anasema ni ulimaji wa mpunga katika majaluba hadi kwenye hifadhi ya barabara.

Ushetu na ongezeko la barabara

Manyongo Nchambi, Meneja wa Tarura katika Halmashauri ya Ushetu anasema kabla ya uanzishwaji wa Tarura halmashauri hiyo ilikuwa na mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 794 za udongo na Changarawe.

Lakini kupitia Tarura mtandao wa barabara umeongezeka na kufikia kilometa 1029.93, lami km 1, Changarawe km 274.52 na zinazobaki ni barabara za udongo.

“Takwimu hizi zinatuonesha kuwa tumeweza kuwafikia wananchi wengi kwa kiwango kikubwa ndani ya miaka mitatu ya Tarura,” anasema.

Wengi wafikiwa Kahama

Joab Mutagwaba, Meneja wa Tarura Halmashauri ya Mji Kahama anasema wao wana mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 911.3 huku lami ikiwa kilometa 11.7, changarawe km 73.9 na barabara za udongo zina urefu wa kilometa 825.6.

“Kwa kiwango kikubwa tumewafikia wananchi wa Kahama ndani ya hii miaka mitatu tangu kuanzishwa Tarura. Hii imerahisisha usafiri na usafirishaji wa wananchi wa Kahama. Wengi wao ni wazalishaji wa mpunga na wengine wanajihusisha na uchimbaji madini aina ya dhahabu. Miundombinu bora na rafiki huwa chachu ya kuendelea kuzalisha kwa wingi zaidi,” anasema.

Barabara zaidi kuboreshwa

Kwa upande wake, meneja wa Tarura Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Salvatory Yambi, anasema wao wana mtandao wa kilomita zaidi ya 700 za barabara, nyingi zikihitaji kufunguliwa na kuwekewa changarawe ili ziweze kupitika kwa muda wa mwaka mzima.

Moja ya mradi mkubwa tulioutekeleza ni ujenzi wa daraja la Kituli ambalo litakuwa linaunganisha kata mbili, hivyo kuwasaidia wananchi wa eneo hilo kuweza kuvuka upande wa pili ili kuweza kupata huduma za kijamii, ikiwa ni pamoja na kupata elimu na huduma za kiafya.

Mapinduzi makubwa Kishapu

Naye Samsoni Gechamet ambaye ni Meneja wa Tarura katika Halmashauri ya wilaya ya Kishapu anasema kuanzishwa kwa Tarura katika halmashauri hiyo kumeleta mapinduzi makubwa ya kimiundombinu.

Anasema wamekuwa wakifanya miradi ya kufungua barabara na kufanya ukarabati wa dharura wa barabara zinazopita vijijini.

Anasema tangu kuanzishwa kwa wilaya ya Kishapu hapajawahi kuwa na barabara yenye kiwango cha lami lakini sasa wameanza kujenga barabara ambayo ni ahadi ya Rais kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita moja.

“Lengo letu ni tuwe na angalau kilomita tano kwa kuanzia katika makao makuu ya wilaya. Lakini ninachoweza kusema mapinduzi makubwa ya barabara yamepatikana katika wilaya yetu,” anasema.

Awali barabara ambazo ziko chini ya Tarura sasa zilikuwa chini ya wakurugenzi wa halmashauri. Wakati huo ufanisi wa maboresho ya barabara ulikuwa mdogo, kutokana na usimamizi kutokuwa wa uhakika sambamba na  mvutano wa mara kwa mara kutoka kwa madiwani wakibishana ni kata gani ipewe fungu kwanza katika utengenezaji au ukarabati wa barabara.

 

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi