loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Bima ya afya kwa wakulima itaongeza uzalishaji shambani

“WAKULIMA ni kundi lililosahaulika katika upatikanaji wa huduma za bima ya afya nchini, hivyo nashukuru na kuipongeza Benki ya TPB pamoja na NHIF (Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya) kwa kulikumbuka kundi hili,” anasema Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Philemon Sengati.

Anaongeza: “Napenda kutoa rai kwa taasisi nyingine za serikali kuiga mfano huu wa TPB na NHIF kwa kukumbuka makundi mbalimbali nchini ya kijamii.”

Mkuu huyo wa mkoa aliyasema hayo katika hafla ya uzinduzi wa huduma za bima ya afya kwa wakulima wa pamba kupitia Mpango wa Ushirika Afya unaotolewa na NHIF iliyofanyika hivi karibuni katika Kijiji cha Mwamashimba kilichopo Igunga mkoani Tabora.

Makubaliano ya kuanzisha huduma hizo kwa ushirikiano wa Benki ya TPB na NHIF yalihusisha pia vyama vya ushirika katika Kanda ya Ziwa.

Taarifa kutoka ndani ya taasisi hizo zinasema mpango huo umelenga kuongeza vyama vingine vya msingi vikiwamo vya Shinyanga Co-operative Union (Shirecu), Kahama Co-operative Union (Kacu) Simiyu Co-operative Union (SCU), Nyanza Co-operative Union (NCU) na vyama vingine vya Kanda ya Ziwa.

Vyama vya msingi vya ushirika kupitia Ofisi ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, vitaingia makubaliano na NHIF na Benki ya TPB kwa kusaini makubaliano ya awali ya ufanyaji kazi kwa Kanda ya Ziwa zitakapopatikana huduma hizi.

Kwa msingi huo, wakulima na wananchi kwa jumla, hawana budi kuuchangamkia na kuupokea mpango huu ili uwape uhakika wa matibabu na huduma nyingine za afya zitakazowawezesha kuwa na afya bora ya mwili na akili na hivyo, kuongeza ufanisi kwa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa wakiwa na uhakika wa matibabu wanapougua.

Katika gazeti hili, toleo la Septemba 13, 2020, mwandishi Ikunda Erick anaandika: “Kwa mkulima, siyo rahisi kila mara kuwa na akiba ya fedha ambayo inatengwa mahususi kwa ajili ya tiba, lakini ugonjwa hauna hodi, unakuja wakati wowote, iwe unazo fedha au hauna unaingia na hapo ndipo utajua umuhimu wa kuwa na bima kwa sababu hakuna hospitali utakayohudumiwa bure, vipimo navyo ni gharama sasa kwa hali ya kawaida si rahisi kuwa na fedha za kutosha kugharamia.”

Anasema ni vyema mfumo huu ulioanzishwa na Benki ya TPB na NHIF kwa wakulima wa kuunganishwa kwenye bima ya afya, ukapokewa kwa mikono miwili na wakulima na huduma zake zikatolewa kwa ubora na uhakika zaidi kwani una faida ni nyingi kwao na familia zao kiafya na kiuchumi kwao na kwa taifa.

Hivyo, wakulima wote wahakikishe wanajiunga na mfumo huo ili walinde na kuimarisha afya zao na nguvu kazi ya taifa kwani hapana siri kwamba, mtu asiye na uhakika wa matibabu, uzalishaji wake siyo wa uhakika na anachozalisha, huishia katika gharama za matibabu.

Kama anavyosema mwandishi Ikunda, changamoto za kiafya huja ghafla bila taarifa, hivyo huyumbisha uchumi wa familia kwa kuwa hutumia pesa nyingi zilizopo au familia kuingia katika madeni na umaskini zaidi ili kumudu matibabu hali ambayo ni hatari kwa ustawi wa jamii.

Jana wakati akizungumza katika mkutano wa kampeni akiwa mkoani Geita kuomba kuchaguliwa kwa kipindi kingine cha miaka mitano, Rais John Magufuli alisema serikali inataka huduma za bima ya afya zimfikie na kumhudumia kila Mtanzania.

“Hii ndiyo maana tuliamua kutumia makusanyo tunayoyapata kufanya uwekezaji wa kutosha katika huduma za afya,” anasema Rais Magufuli.

Katika moja ya mazungumzo na HabariLEO, Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Uhai (Prolife) Tanzania, Emil Hagamu aliwahi kusema: “Unapokuwa na bima, unakuwa na uhakika wa matibabu ikitokea umeugua, lakini usipougua kama wengine wanavyodhani, unakuwa na uhakika kuwa kama ungeugua, ungetibiwa bila tatizo na kubwa zaidi, usipougua lakini una bima, unawezesha wengine kutibiwa hivyo, unakuwa umechangia kulinda wazalishaji uchumi wa familia, ukoo na taifa kwa jumla.”

Hagamu anasema afya ni msingi mkuu wa uzalishaji mali wenye tija.

Ikumbukwe, taifa lenye wananchi wenye uhakika wa afya zao kupitia uhakika wa huduma za matibabu, ni taifa lenye watu wenye uwezo wa kushiriki uzalishaji mali kikamilifu na kujiletea maendeleo kupitia kazi mbalimbali ama za kujiajiri, au kuajiriwa viwandani, shambani, ofisini au katika biashara hivyo, kuzalisha kwa tija.

 

Ikumbukwe kuwa, Tanzania chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli, imefanikiwa kutoka katika nchi za ulimwengu wa tatu yaani nchi maskini na kuingia katika uchumi wa kati kabla ya kufikia kipindi kilichowekwa kufikia lengo hilo cha mwaka 2025.

Kimsingi matamanio ya serikali ya Tanzania, ni kuona huduma za bima ya afya zinawafikia watu wote.

Kimsingi, uhakika wa huduma bora za afya na matibabu, ni nyenzo muhimu kwa Watanzania kuibadili nchi yao kiuchumi na kuifanya ya uchumi unaotegemea zaidi uzalishaji wenye tija shambani na viwandani na ili kulitimiza hili, taifa linahitaji kuwa na wazalishaji mali wenye afya njema na uhakika wa matibabu sambamba na wategemezi wao.

Ndiyo maana Mkuu wa Mkoa wa Tabora (Dk Sengati) anasema katika hafla hiyo: “Utaratibu huu wa bima ya afya ni suluhu kubwa ya kila mkulima kuipatia kaya yake uhakika wa matibabu wakati wowote.”

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya TPB, Sabasaba Moshingi ananukuliwa akisema: “Mpango huu wa huduma za afya kwa wakulima, umeanza na mazao ya kimkakati hususani pamba ambalo ni zao linalolimwa zaidi Kanda ya Ziwa.”

Anasema: “Majaribio ya huduma hizi yanafanyika kwa kushirikiana na Chama cha Ushirika cha Igembensabo Co-operative Union kilichopo Igunga-Tabora na huduma hizo zitapatikana katika matawi ya Benki ya TPB Kanda ya Ziwa na ofisi za NHIF.”

Anasema wakulima wakiitumia fursa hiyo vizuri, itawapa ufanisi katika uzalishaji mali kwani wakati wote watafanya kazi zikiwamo za uzalishaji shambani wakiwa na amani na pia, mapato yao yatatumika kwa maendeleo na siyo kwa kulipia huduma za matibabu.

Kupitia mpango huu, Benki ya TPB inawakopesha bila riba wakulima hao fedha za mchango na watazilipa baada ya kuuza mazao yao.

Sengati anasema: “Kwa kuwa fedha zinazotolewa na TPB hazina makato wala riba, ni wazi hili ni jambo linalolenga kumkomboa mkulima na kumhakikishia uhakika wa matibabu wakati wowote.”

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga anasema: “Wakulima kupitia vyama vyao vya msingi watachangia Sh 76,800 kila mmoja, huku mwenza wa mkulima pia atachangia Sh76,800 na watoto chini ya miaka 18 watachangia Sh 50,400 kwa mwaka.”

Anafafanua kuwa, makato yatafanyika mkulima atakapokuwa analipwa fedha ya mazao yake kupitia chama chake cha ushirika.

“Mkulima akishapewa ‘Bima Afya Kadi’ yake, atanufaika na huduma mbalimbali zikiwamo za kumuona daktari, dawa, vipimo, upasuaji, afya ya kinywa na meno, tiba ya macho, miwani ya kusomea na mazoezi ya tiba ya viungo.

Meneja wa Tawi la TPB mkoani Tabora, Timon Massawe anasema: “Benki kupitia dira yake ya kuyafikia makundi yasiyopata huduma za kifedha kupitia mpango huu, itapanua wigo wa huduma zake nyingine za kibenki na itaungana na jitihada za Serikali chini ya Rais John Magufuli kuhakikisha wananchi wengi wanapata huduma ya bima ya afya hasa wakulima ili waongeze uzalishaji.”

 

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi