loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Profesa Chijoriga: Sera ya ‘Kilimo Kwanza’ bado muhimu

KILIMO ni sekta muhimu kutokana na mchango wake katika maendeleo ya taifa. Kinategemewa kutoa chakula kwa Watanzania, kuingiza fedha za kigeni na kutoa malighafi kwa ajili ya viwanda.

Mtazamo huo unaungwa mkono na msomi na mtaalamu mstaafu aliyebobea katika masuala ya Fedha na Usimamizi wa Biashara ambaye sasa anajishughulisha na kilimo cha korosho, Profesa Marcellina Chijoriga.

Profesa Chijoriga pia ni mkufunzi na mwezeshaji kwa msimu katika masuala ya fedha, utawala wa biashara, programu na miradi, ufuatiliaji wa masuala ya menejimenti, tathmini, ujasiriamali na utawala.

Hivi karibuni alifanya mahojiano maalumu na gazeti hili kuhusu  masuala mbalimbali akiwa kama mama, msomi na mtaalamu aliyebobea katika masuala ya uchumi, fedha na biashara. Miongoni mwa mengi aliyozungumza ni masuala ya kilimo.

Huku akiamini kilimo ndicho kitainua taifa hili, Profesa anasema kampeni kama ya chakula ni uhai ni muhimu sana kwa watanzania kwa kuwa kilimo ni sekta shirikishi ama jumuishi, akifafanua kwamba inashirikisha watu wengi na kumgusa kila Mtanzania.

“Watu wa kada mbalimbali wanashiriki na hata ukitaka kugusa uchumi wa mtu mmoja mmoja kwa mazingira ya sasa na Rais John Magufuli amesema tunakwenda uchumi wa viwanda, ambao kimsingi utafanikishwa kwa kaisi kikubwa na kilimo,” anasema.

Anasema unapozungumzia suala la viwanda lazima utambue unazungumzia viwanda vya aina gani au vya kuzalisha nini?

“Sio siri, hatuwezi kushindana na viwanda vya wenzetu nje lakini tunaweza kushindana na viwanda ambavyo malighafi zake tunazo hapa hapa nchini, malighafi hizo zinapatikana mashambani mwetu watanzania.

“Angalia kipindi cha janga la ugonjwa wa covid-19 (corona), tungekuwa na viwanda (vingi) vinavyotegemea malighafi kutoka nje, leo tungekuwa wapi… Mungu ametuonesha kwamba sisi kufanya kilimo ndio uti wa mgongo ni jambo jema, ingawa wengine wanasema uti wa mgongo umetafsiriwa vibaya, tunachosema ni kwamba kilimo ndio kitatuletea maendeleo,” anasema.

Profesa Chijoriga anasema ukiangalia kilimo, mnyonyoro wake wa thamani ni mzuri kwani kila mtu anashiriki na kinashirikisha  sekta nyingine lukuki.

Anatoa mfano kwamba katika kilimo sekta ya elimu inaguswa kwa sababu lazima wataalamu wawepo, sekta ya afya imo pia kwani kama huna afya huwezi kwenda kulima, usafirishaji vile vile, huwezi kufanya kilimo bila usafirishaji kwa sababu ili kupeleka mazao sokoni ni lazima uwe na barabara nzuri, kwa hiyo kilimo kinahusiana na sekta karibu zote.

Msomi huyo anasema janga la ugonjwa corona limeleta mafunzo mawili; kwanza kuna sekta zinahitajika sana na kuna sekta ambazo zisipofanywa vizuri zitakwamisha maendeleo.

Anataja sekta ya afya akisema kila mtanzania ameelewa faida ya afya maana mtu asipokuwa mzima hawezi kufanya jambo lolote.

Jambo la pili anasema ni sekta za huduma muhimu/huduma msaada (supporting services) moja ikiwa ni elimu. Anafafanua kwamba mtu akielimika hata akiambiwa masuala ya afya ataelewa kwa sababu ni vigumu kumwelewesha mtu ambaye hajaelimika.

Anasema unapozungumzia masuala ya kilimo, bila afya nzuri huwezi kulima, ukienda hata vijijini utakuta kuna vikundi vya afya lakini ukiangalia historia ya wanaounda vikundi hivyo ni wakulima, yaani chanzo cha mapato kijijini ni kulima na ukizungumzia watoto kwenda shule huyo mzazi ni mkulima na hata iwe vyama vya kuweka na kukopa (saccos) wahusika ni wakulima.

Anasema ile sera iliyoanzishwa na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ya ‘Kilimo Kwanza’ ilikuwa na umuhimu wa pekee na kwamba hata sasa bado ina umuhimu huo na inapaswa kuhuishwa.

Anaamini kama ingeendelezwa vyema Tanzania kwa sasa ingekuwa imefika mbali katika kilimo.

Anasema kila zao la kilimo linawagusa watu wengi kwani ukianza na mbegu bora utakuta kuna mtengenezaji wa mbegu, kuna mtafiti wa mbegu husika, kisha kuna mkulima na kwenye kulima kuna pembejeo, matrekta na kadhalika.

“Ukishalima lazima uwe na maghala, hiyo ni nafasi nyingine inatokea hapo, lakini ili uweze kuwa na soko lazima uwe na barabara, ili kusindika mazao yako lazima uwe na umeme, kulima kote huko kuna hitaji fedha na hapa utahitaji benki,” anasema.

Anasema kingine kinachotakiwa ni elimu sahihi ya kilimo na sio elimu ya taaluma nyingine.

Anasema Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ulikuwa mzuri pia lakini tatizo kulikuwa na ushindani baina ya sekta na sekta ambao haukuwa na tija sana.

“Watu wanapenda kushindana wenyewe kwa wenyewe na kimsingi sekta zote zinahitajiana lakini tulikosa kujua lengo letu lilikuwa ni nini hasa,” anasema. 

Anasema Watanzania wanatakiwa kuwa makini kwa kila jambo, kama ni mifugo ni lazima uifuge vizuri, upate mbegu nzuri itakayozalisha vizuri na kupata maziwa mengi na kama ni nyama upate ng’ombe bora watakaokupa nyama nzuri itakayovutia soko.

“Uzuri wa mifugo na kilimo, utahitaji maji na hiki kilimo cha kusubiri mvua mpaka inyeshe ndio shida sasa, kama miye shambani kwangu nalima nasubiri mvua nilime, lakini niko na harakati ya kutafuta namna ya kuhifadhi maji ili niweze kumwagilia kama mvua hakuna mwaka mzima,” anasema.

Anasema kama watu watakuwa na namna ya kuhifadhi maji na kumwagilia itasaidia kulima mwaka mzima badala ya kulima kilimo cha kusubiri mvua zinazonyesha msimu kwa msimu.

“Kuna wakati hapa nyanya hakuna, lakini kuna ardhi nzuri ya kulima nyanya wakati wote, kuna wakati mboga zinapotea lakini ukiangalia tuna maji mengi katika taifa letu kuliko maeneo mengi tu duniani. Je, haya maji tunafanya nayo nini?” Anahoji Profesa Chijoriga.

Anahoji utajiri wa misitu uliopo nchini kwamba ni nini kinafanyika? Anasema kama unaelekea Songea, utaona ukanda wote wa Mbeya, Njombe, Rukwa ni ardhi ambayo haijaguswa lakini anaamini kama itasimamiwa vizuri, Tanzania inaweza kufanyika kilimo kikubwa kitakachoinua nchi na kuchangia vyema katika Tanzania ya viwanda.

Anasema aliwahi kwenda nchini Misri, nchi ambayo iko jangwani na kugundua kwamba ardhi yao ni mchanga mtupu na siyo ardhi nzuri kama Tanzania lakini Wamisri wametumia maarifa wakatengeneza ardhi nzuri ya kulima.

Anasema hata Israel wameweza kubadilisha ardhi yenye mawe mengi kuwa ardhi nzuri ya kilimo, jambo ambalo Tanzania tayari ardhi ipo nzuri.

Anasema kwa taifa kama Tanzania elimu ya kilimo ni muhimu kuanzia ngazi ya elimu msingi na ngazi za juu kwani wataalamu wa kilimo wanaoendana na hali halisi ya mazingira yetu wanahitajika sana.

Profesa Chijoriga ambaye amekuwa akijihusisha na kilimo kwa miaka mitatu sasa amekuwa pia kiongozi wa Timu ya Uwekezaji kwenye Kilimo Tanzania (TAN-AIM).

Ameshiriki pia katika kuanzisha taasisi inayojulikana kama Agricultural Delivery Division (ADD), ameshiriki uwezeshaji na kusaidia Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Kilimo (ASDPII) uliokuwa chini ya Wizara ya Kilimo na Blue Print katika kuleta maendeleo ya viwanda.

“Nimeshiriki kutengeneza programu ya ASDP. Nilipomaliza Ukuu wa Kitivo UDSM niliombwa kushiriki katika programu hii. Programu hii nilishiriki kikamilifu kuitayarisha na ilikuwa chini ya Wizara ya Kilimo. Ilianza kutekelezwa mwaka juzi kwa ufadhili wa Bill and Belinda Gates Foundation baada ya kusuasua,” anasema.

Anasema serikali ilikuwa na wadau wengi kwenye kilimo, lakini ilikuwa haijulikani wadau wa maendeleo ni nani na anafanya nini kwenye kilimo na hivyo programu hiyo ilisaidia jambo hilo.

Profesa anasema baada ya kuandaa hiyo programu, walimwambia amefanya kazi nzuri akaombwa asaidiea kuanzisha kitu kinachojulikana kama Agricultural Delivering Division.

“Ukisikia Ethiopia imeendelea katika kilimo ni kwa sababu wana kitu kinaitwa Agricultural Transformation Agency (ATN) na walisaidiwa na taasisi ya Bill and Belinda Gates,” anasema.

Profesa Chijoriga anasema kupitia programu hizo alipata mawasiliano na taasisi ya Bill and Belinda Gates na mpaka sasa anaendelea kushirikiana nao katika masuala ya kilimo na kwamba tangu mwaka 2017 taasisi hiyo imekuwa ikisaidia maendeleo ya kilimo Tanzania.

Profesa Chijoriga  ambaye anaendelea kufanya kazi na taasisi ya Bill na Belinda Gates kama mshauri (consultant), anasisitiza kwamba kilimo ni kizuri sana na ndio sekta itakayoendelea kuwa juu katika kuinua maendeleo ya taifa na watanzania kwa ujumla, hivyo anatoa wito kwa watanzania kundelea kuithamini, kuheshimu na kukipenda kilimo.

 

foto
Mwandishi: Angela Semaya

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi