loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Yajue yasiyotakiwa wakati wa kampeni

KAMPENI kwa ajili ya uchaguzi utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu zinaendelea baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kupuliza kipyenga.

Kwa mujibu wa kifungu cha 46 (1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha 53 (1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 kipindi cha kampeni huanza siku moja baada ya Siku ya Uteuzi na kumalizika siku moja kabla ya siku ya Uchaguzi.

Kwa kuzingatia kanuni ya 40 ya kanuni za uchaguzi wa rais na wabunge za mwaka 2020 na kanuni ya 35 ya kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa (Uchaguzi wa Madiwani) za mwaka 2020 zikisomwa pamoja na kipengele cha 2.1(c) cha maadili ya uchaguzi ya mwaka 2020 muda wa kuanza kampeni utakuwa saa mbili kamili (2:00) asubuhi na kumalizika saa kumi na mbili kamili (12:00) jioni Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeandaa Maadili ya Uchaguzi kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Maadili ya uchaguzi ni makubaliano ya pamoja baina ya vyama vya siasa, serikali na NEC yanayoeleza mambo yanayotakiwa kufanywa au kuzingatiwa na yasiyotakiwa kufanywa katika mchakato wa uchaguzi wakati wa kampeni za uchaguzi, upigaji kura na kutangaza matokeo ya uchaguzi.

Vifuatavyo hapa ni miongoni mwa vitendo ambavyo vimetajwa katika maadili ya uchaguzi ambavyo vyama vya siasa havitakiwi kufanya na mtu akivifanya ni ukiukwaji wa maadili ya uchaguzi.

Mosi ni lugha za kashfa na matusi kwa wagombea na viongozi wa vyama vya siasa wakati wa kampeni. Ni marufuku kwa mgombea au viongozi wa chama kimoja cha siasa kutoa lugha za kashfa na matusi dhidi ya mgombea au viongozi wa chama kingine cha siasa wakati wa kampeni.

Kosa lingine ni kuzidisha muda wa kampeni; Muda wa kampeni ulioelekezwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi yaani kuanzia saa mbili kamili asubuhi hadi saa kumi na mbili kamili jioni. Mgombea au chama cha siasa hakitakiwi kufanya kampeni zaidi ya muda ulioelekezwa na Tume.

Halikadhalika ukiukwaji wa ratiba ya kampeni ni kosa. Uratibu wa kampeni za uchaguzi unafanywa chini ya uenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa makubaliano na vyama vya siasa.

Hivyo mabadiliko yoyote ya ratiba ya kampeni hayana budi kufanywa na Tume kwa kushirikisha vyama vyote vinavyoshiriki katika kampeni. Maandamano ya wafuasi wa vyama vya siasa yasiyokuwa na kibali kabla na baada ya kampeni ni ukiukwaji pia wa maadili ya uchaguzi.

Wafuasi wa vyama vya siasa wanaokwenda au kutoka kwenye mikutano ya kampeni hawapaswi kufanya maandamano wakati wa kwenda wala kutoka katika mikutano husika.

Kwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria. Ukiukwaji mwingine ni wafuasi wa vyama kuharibu mabango ya wagombea wa vyama vingine; baadhi ya watendaji wa serikali kuingilia shughuli za vyama vya siasa; vurugu dhidi ya vyama na wagombea katika baadhi ya maeneo; kubandika picha za wagombea juu ya picha za wagombea wa vyama vingine; wafuasi wa vyama na wagombea kuingilia mikutano ya wagombea wa vyama vingine na mgombea au chama kimoja kutoa kauli zisizoweza kuthibitishwa dhidi ya mgombea au chama kingine.

Kwa ujumla maadili ya uchaguzi yanahusu kuheshimiana, kuzingatia ratiba za kampeni na kuelimisha wanachama wa vyama katika misingi ya kuelewa sera za vyama husika.

Aidha vyama vinahimizwa kutohamasisha wanachama au wafuasi wao kujenga chuki na pia wanachama na wafuasi hawatakiwi kubeba silaha za aina yoyote katika mikutano ya kampeni.

Kila chama kilichosaini maadili ya uchaguzi na kuweka mgombea, mgombea mwenyewe, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Serikali vina haki ya kuwasilisha kwa maandishi malalamiko ya ukiukwaji wa maadili ya uchaguzi.

Malalamiko juu ya ukiukaji wa maadili ya uchaguzi yanapaswa kuwasilishwa kwenye Kamati husika ndani ya muda wa saa 72 tangu ukiukwaji ulipofanyika.

Sehemu ya 5 ya maadili ya uchaguzi ya mwaka 2020, imezitaja kamati za maadili ya uchaguzi ambazo zitashughulikia malalamiko ya ukiukwaji wa maadili wakati wa kampeni.

Kamati hizo ni kama ifuatavyo: Kamati ya maadili ngazi ya kata ambayo mwenyekiti wake ni Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Kata. Wajumbe wa Kamati hii ni mwanachama mmoja kutoka kwenye kila chama cha siasa chenye mgombea wa udiwani na mwakilishi wa serikali aliyeteuliwa na katibu tawala wa wilaya.

Kamati ya maadili ngazi ya jimbo ambayo mwenyekiti wake ni msimamizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo. Wajumbe wa kamati hii ni mwanachama mmoja kutoka kwenye kila chama cha siasa chenye mgombea wa ubunge na mwakilishi wa serikali aliyeteuliwa na katibu tawala wa wilaya.

Kamati ya maadili ngazi ya taifa. Mwenyekiti wa kamati hii ni mjumbe yeyote wa tume atakayeteuliwa na Tume.

Wajumbe wa kamati hii ni mwanachama mmoja kutoka kwenye kila chama cha siasa chenye mgombea wa kiti cha rais na mwakilishi wa serikali aliyeteuliwa na katibu mkuu ofisi ya waziri mkuu.

Kamati ya maadili ya rufaa mwenyekiti wake ni Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Wajumbe wa kamati hii ni mwanachama mmoja kutoka kwenye kila chama cha siasa chenye mgombea wa kiti cha rais na mwakilishi wa serikali aliyeteuliwa na katibu mkuu ofisi ya waziri mkuu.

Ikumbukwe kuwa kosa lolote la ukiukaji wa maadili ya uchaguzi linaambatana na adhabu kulingana na ukubwa au uzito wa kosa husika.

Adhabu zinazotokana na ukiukaji wa maadili ya uchaguzi ni pamoja na wahusika kutakiwa kusahihisha kosa au kuomba radhi, kupewa onyo kwa njia ya maandishi, kutangazwa kwenye vyombo vya habari na pia kuzuiwa kufanya kampeni kwa muda ambao Kamati husika itaona unafaa na pia kupigwa faini.

Hivyo ni vema wahusika wa maadili ya uchaguzi hususan wagombea na vyama vya siasa wakajikita katika kueleza sera za vyama na kuepuka kujiingiza katika mtego huo wa mambo yasiyotakiwa kufanywa wakati wa kampeni ili kuvuka salama katika kipindi hiki cha kampeni na hivyo kushiriki katika uchaguzi huu ujao wa Oktoba 28, mwaka 2020.

Mwandishi wa makala haya ni Ofisa Habari wa NEC

foto
Mwandishi: Margareth Chambiri

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi