loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wakulima parachichi Mafinga wanolewa

WAKULIMA wa parachichi katika mji wa Mafinga wilayani Mufindi mkoani Iringa, wamepatiwa elimu ya kilimo bora cha zao hilo ambalo hivi sasa lina soko kubwa ndani na nje ya nchi.

Elimu hiyo imetolewa na Kampuni ya Agrigrow Tanzania Ltd yenye makao makuu yake katika mji wa Morogoro ambayo wana lengo la kuleta mageuzi makubwa katika kilimo hapa nchini.

Akizungumza katika mafunzo hayo Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara, Wilson Mbwambo alisema kuwa lengo la kuendesha mafunzo hayo ni kuwapatia mbinu za kilimo hicho wakulima ili kuongeza uzalishaji ambao unakubalika katika soko la kimataifa.

Hata hivyo, aliwataka wakulima hao kuchagua mbegu bora hasa pale wanapotaka kuanzisha vitalu vya miche ya parachichi kwani hiyo ndiyo hatua muhimu itakayomfanya mkulima kupata faida kwa kile anachozalisha.

Katika hatua nyingine, aliongeza kuwa hivi sasa kampuni hiyo itahakikisha wanatoa elimu mara kwa mara sambamba na kuwapatia virutubishi asilia kutoka Agrigrow ambavyo vitawaongezea uzalishaji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mji wa Mafinga, Saada Mwaruka alisema kuwa katika kuunga mkono uzalishaji wa parachichi hivi sasa wana eneo lenye ukubwa ekari 50 ambazo zitatumika kama shamba darasa kwa wakazi wa mji huo.

Nao baadhi ya wakulima walisema kuwa hivi sasa wanakabiliwa na changamoto ya kupata miche bora ya zao hilo, ambalo linawaongezea kipato kikubwa kutokana na kuwa na soko la uhakika.

Hata hivyo, waliomba elimu hiyo itolewe mara kwa mara pamoja na wataalamu kufika katika mashamba ili kuangalia namna wanavyohudumia mashamba yao ya parachichi.

Akizungumzia suala la mbegu na miche bora ya parachichi, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya alisema kuwa hivi sasa vituo vya utafiti wa kilimo katika mikoa hiyo, vimeshaanza kuuza miche ambayo ni bora na yenye kuongeza uzalishaji.

Mafunzo hayo ya kilimo bora cha parachichi, yaliyoandaliwa na Kampuni ya Agrigrow Tanzania Limited yenye makao makuu yake katika mji wa Morogoro, yaliweza kuwajengea uwezo wakulima katika kukabiliana na magonjwa na wadudu wasumbufu katika zao hilo na mbinu za kujikinga nao.

Hata hivyo, waliahidi kuendelea kutoa elimu hiyo kwa wakulima wa mikoa hiyo ya Nyanda za Juu Kusini ili kuweza kuona faida ya kilimo cha parachichi ambacho kitaongeza kipato kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

KAMPUNI ya uchimbaji ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi