loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ongezeko la wataalamu wa jiolojia litakavyonyanyua uchumi

RASILIMALI zinazotokana na jiolojia zimekuwa na umuhimu mkubwa kwa wanadamu na viwanda. Rasilimali hizi mara nyingi hupatikana kupitia utafiti na kisha kuchimbwa baada ya kugundulika kwamba zinapatikana mahala fulani.

Hakuna shaka kwamba, viwanda vya ufuaji chuma, shaba, dhahabu, uchongaji wa vito na mawe, utengenezaji wa vyombo vya udongo, mbolea na uzalishaji wa saruji vinategemea mazao ya moja kwa moja ya kazi za wanajiosayansi.

Hali kadhalika, mitambo ya viwanda duniani kote inaendeshwa kwa kutumia nishati inayozalishwa kutokana na kazi wa wanajiosayansi kama vile umeme wa mafuta, gesi asilia, makaa ya mawe, joto ardhi na madini ya urani.

Tunaposema wanajiosayansi tunamaanisha wataalamu waliosomea fani za jiolojia, jiofizikia, jiokemia, jioteknolojia, jiolojia ya mazingira na nyinginezo. Wataalamu hawa wanapata maarifa ya elimu ya masomo hayo yanayohusu jiolojia kutoka vyuo vikuu nchini kama vile Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu Dodoma (UDOM).

Miezi michache iliyopita wanafunzi 28 kutoka UDSM na UDOM, walifanya ziara ya kimasomo kwa lengo la kujifunza kwa vitendo juu ya jiolojia na madini yaliyopo nchini Tanzania.

Ziara hiyo ilianzia Dar es Salaam Machi 12 mwaka huu kupitia Morogoro, Dodoma, Kituo cha Madini (GST), machimbo madogo ya dhahabu ya Sekenke mkoani Singida, mgodi wa almasi wa Williamson Mwadui, Shinyanga, migodi ya dhahabu Bulyanhulu, Kahama, Geita na North Mara.

Wanafunzi hao pia walitembelea mbuga ya wanyama Serengeti pamoja na hifadhi ya Ngorongoro na kuishia milima ya Upare mkoani Kilimanjaro.

Lengo lilikuwa ni kujifunza kwa vitendo kuhusu jiolojia na madini yaliyopo katika migodi mbalimbali nchini.

Kutokana na ziara hiyo, Rais wa chama cha wanajiolojia nchini (TGS), upande wa wanafunzi, Lutangilo Sakafu anaipongeza serikali na makampuni binafsi katika sekta za madini na nishati kutokana na mchango wao wa kuendeleza sekta ya madini na jiolojia kiujumla.

Sakafu anasema kwa kufanya hivyo serikali na wadau wake wamewekeza mtaji mkubwa wa rasilimali watu katika fani hiyo, ikiwa ni pamoja na kuwatayarisha wasomi hao kuajiriwa kama wanataaluma wajao au kuajiri.

Anasema kwa kutumia elimu waliyoipata wakiwa chuoni na katika ziara hiyo, wanafunzi hao wangependa kuisaidia serikali kuendeleza sekta ya uchimbaji mdogo wa madini kwani kuna matumizi madogo ya elimu ya jiolojia katika sekta hiyo.

“Endapo utaalamu wa kijiolojia utatumika vizuri na zaidi, upatikanaji wa madini utaongezeka, hali ambayo itaongeza mapato kwa serikali yetu ya Tanzania,” anasema.

Anasema kuwa wanafunzi wanatambua jitihada zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano katika kuendeleza jiolojia. “Tunaomba serikali na wadau wengine katika sekta za madini na nishati kuendelea kusaidia wanafunzi wa jiolojia kuwa na ziara za kivitendo mara kwa mara ili kuongeza ujuzi wa vitendo kwa wanafunzi hao,” anasema.

Naye Katibu Mkuu wa chama hicho upande wanafunzi, Sharon Athumani, anasema ziara hiyo ilikuwa ni fursa ya kipekee na imewawezesha kujifunza juu ya utajiri wa madini wa Tanzania.

“Kama wanafunzi tumejifunza jinsi tunaweza kuchanganua akili zetu pamoja na kuangalia fursa za sisi kuweza kujiajiri,” anasema.

Anasisitiza kuwa endapo sekta ya uchimbaji mdogo wa madini itazingatia elimu ya jiolojia badala ya ile ya mtaani, itasaidia katika kuongeza pato la nchi.

Anasema kama wanafunzi watakapohitimu wapo tayari kutumia elimu yao ya kijiolojia kuhakikisha upatikanaji wa madini katika maeneo ya wachimbaji wadogo yanaongezeka.

Anasema kwa niaba ya chama na wanafunzi wote anawashukuru wale wote waliofanikisha ziara yao hiyo ambao ni ni Pamoja na kampuni ya mafuta na gesi ya Pan African Limited na chama cha wanajiolojia Tanzania.

Wengine waliofanikisha ziara hiyo ni mgodi wa almasi wa Williamson, Mwadui, migodi ya dhahabu ya Bulyanhulu, Kahama na North Mara, kituo cha madini GST na wadau wengine wa serikali.

Mwaka juzi, Katibu Mkuu wa chama cha wanajiolojia, Dk Elisante Mshiu ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Jiolojia UDSM, aliwasilisha maombi kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ya kuwepo na utaratibu maalumu wa wahitimu wanaomaliza chuo, kuchukuliwa na makampuni kwa muda maalumu kwa ajili ya mafunzo kwa njia ya vitendo ili kuongeza ujuzi wao.

Dk Mshiu alisema kwa kufanya hivyo watakuwa sio tu kwamba wanawekeza mtaji katika rasilimali watu katika fani hiyo bali wanawatayarisha wasomi hao kuwekeza kujiajiri na kuajiri wataaluma wajao.

Alisema jambo hilo lingeweza kuratibiwa vizuri na kwa ufanisi mkubwa zaidi endapo patakuwa na chombo bora cha kuwatambua na kuwaandikisha wana jiosayansi nchini, yaani Bodi ya Usajili ya Wajiosayansi.

Chombo hicho alisema kinapaswa kuwa mdau muhimu kupitia kamati zake katika kuisaidia serikali kuwaendeleza wachimbaji wadogo kwa kupitia na kufanya upembuzi yakinifu wa miradi pendekezwa ili kurahisisha na kusaidia upatikanaji wa mikopo itakayowaendeleza wachimbaji hawa.

Tanzania kupata wachimbaji wadogo wenye elimu ni muhimu katika kuboresha sekta hii hasa kwa kuzingatia kwaba asilimia 67 ya dhahabu duniani kote huzalishwa na wachimbaji hao.

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi