loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Matukio ya moto kuunguza shule yachunguzwe haraka

TAIFA linaomboleza vifo vya watoto 10 wa Shule ya Msingi ya Byamungu Islamic ya wilayani Kyerwa mkoani Kagera, ambao wamefariki dunia baada ya moto kuteketeza bweni la shule hiyo usiku wa Septemba 14, mwaka huu na kujeruhi wengine kadhaa.

Tukio hilo limekuja siku chache baada ya matukio ya moto kuteketeza mali na kusababisha vifo. Shule ya Sekondari ya Ilala Islamic ya Dar es Salaam iliungua moto Julai na kusababisha vifo vya wanafunzi watatu.

Shule nyingine ni Kinondoni Muslim na Mivumoni pia za Dar es Salaam na Kaloleni mkoani Kilimanjaro.

Shule ya Mivumoni iliungua mara tatu katika kipindi cha miezi miwili kati ya Julai na Agosti mwaka huu.

Kwa hakika matukio haya yanaleta simanzi na huzuni kwa taifa, hasa ikizingatiwa kuwa wanafunzi hawa walitegemea kumaliza masomo yao na baadaye kuja kujitegemea na kutegemewa na familia zao na taifa kwa ujumla katika ngazi mbali mbali.

Lakini kubwa zaidi ni kwamba matukio haya yametokea katika muda mfupi na kwa mfululizo, hali inayotishia usalama wa wanafunzi katika shule hizo na shule nyingine nchini, lakini pia kuwaweka roho juu wanafunzi wenyewe, familia zao na taifa kwa ujumla.

Akihutubia jana mkutano wa kampeni mjini Bukoba, Rais John Magufuli ameziagiza Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na ile ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kuhakikisha shule zote zinazoanzishwa nchini, zinazingatia masuala ya usalama kabla na baada ya kuanzishwa kwake.

Rais Magufuli alisema shule zote nchini zinazoanzishwa, zinatakiwa kuwa na mifumo sahihi za kiusalama kwa watoto na watumishi katika shule hizo.

Amesema kumekuwepo na ajali katika baadhi ya shule zikihusisha masuala ya moto, huku vyanzo vyake vikiwa havieleweki, jambo ambalo linaacha majonzi kwa wazazi na kusitisha ndoto za watoto wengi.

Mbali ya Rais Magufuli, Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Nuhu Mruma ameziomba mamlaka za uchunguzi ikiwamo Polisi, kuharakisha kuchunguza matukio ya moto katika shule zao na kuwashirikisha kila hatua muhimu za uchunguzi ili kuondoa minong’ono kuhusu matukio hayo.

Ni kweli kabisa mamlaka zinazohusika katika kusimamia masuala haya, zinapaswa kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri katika shule ili kuepuka majanga zaidi, lakini kubwa mamlaka za uchunguzi zichunguze haraka na zitoe majibu ya yale ambayo yameonekana katika uchunguzi wao.

Hii itasaidia katika kurekebisha kasoro zitakazobainika lakini pia kuchukua hatua kwa wale watakaoonekana walifanya ama uzembe au hujuma katika matukio haya ya moto, ambayo kwa hakika yameanza kuwatia hofu Watanzania, hasa ikizingatiwa yanatokea katika maeneo ya shule.

HATIMAYE safari za ndege kati ya Tanzania na Kenya zimerejea ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi