loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Serikali: Ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu UN haina uhalisia

SERIKALI imesema taarifa iliyotolewa na Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (UN) inayoitaka Tanzania kuepuka mazingira ya ukandamizaji, haina uhalisi juu ya hali ilivyo nchini.

Kwa mujibu wa Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi, taarifa hiyo imesheheni tuhuma ambazo zikifuatiliwa, itagundulika kuwa ni malalamiko yanayotokana na watu waliozoea kuvunja sheria au kupiga dili.

Akizungumza na gazeti dada la gazeti hili, Daily News, Dk Abbasi alieleza kuwa wasiwasi huo unaodaiwa kwenye taarifa hiyo ya UN, tayari kama nchi ilishaitolea majibu kwenye mikutano ya UN na kufafanua vyema jinsi Tanzania inavyolinda haki za binadamu, kwa maana ya haki na wajibu.

“Tunauahidi Umoja wa Mataifa kuwa sisi tutaendelea kuwa walinzi wa haki za binadamu na si watetezi wa wale wanaotaka kutumia haki za binadamu kuharibu uhuru wa wengine au kuchochea vurugu na kuharibu amani katika nchi yetu yenye amani,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje a Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Palamagamba Kabudi alipozungumza na Shirika la Habari la Uingereza (BBC), alisema serikali imeipokea ripoti hiyo kwa mshangao mkubwa.

Profesa Kabudi alisema endapo Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet aliyetoa taarifa hiyo angekuwa anaishi Tanzania, asingeandika maneno hayo au kutoa tathmini aliyoitoa.

''Kwanza tumechukua hatua leo (jana) kwamba Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Ofisi ya Geneva awasilishe majibu yetu rasmi kuhusu taarifa hiyo,'' alisema Profesa Kabudi.

Pia aliongeza kuwa hali halisi nchini Tanzania ni tofauti na yale aliyosema Kamishna Mkuu, Bachelet akiangazia hali ya siasa kipindi hiki cha uchaguzi.

''Sasa tuko katika Uchaguzi Mkuu tunao wagombea nafasi ya urais 15 na wote wanafanya mikutano yao nchi nzima kila sehemu na hakuna aliyezuiliwa kufanya mikutano. Kweli kwa wengine ni mshangao,” alisema.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Kamishna Bachelet, ilidai kuwa nchini Tanzania kumekuwepo na hali ya kuongezeka kwa ukandamizaji wa kidemokrasia na haki za raia, hali ambayo inazidi kufanya mazingira ya haki za binadamu kuwa duni.

Kamishna huyo alieleza hasa mabadiliko ya sheria mbali mbali hususani Sheria Namba 3 ya 2020, ambayo alidai kuwa inazuia uwajibikaji wa serikali kwa utekelezaji wa haki za binadamu nchini.

"Kuna sheria ambazo zimezuia haki ya raia mitandaoni na nje ya mtandao katika miaka ya hivi karibuni. Mfano Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 3 ya 2020 inaminya wigo wa kufungua kesi za ukandamizwaji wa haki za binadamu...kuminywa zaidi kwa haki za binadamu kunaweza kusababisha athari mbaya,” alidai Bechelet.

Alisema tume hiyo imekuwa ikipokea ripoti kuhusu ukamataji holela na kushikiliwa kwa wanaharakati, waandishi wa habari na wapinzani.

Kwa ukanda wa Afrika Mashariki, taarifa hiyo pia imegusia hali ya haki za binadamu katika mataifa ya Ethiopia, Somalia na Burundi.

Mataifa mengine yaliyoguswa kwenye ripoti hiyo ni Ethiopia, Mali, Marekani, Saudi Arabia, Ivory Coast, Iran, Iraq, Afghanistan, Colombia, Mexico na Brazil.

Wakati taarifa hiyo ikitoka Juni, mwaka huu, Tanzania iliongoza katika Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki (EAC) kwenye orodha ya nchi zenye amani, ikishika nafasi ya saba Afrika na nafasi ya 52 duniani, ikipanda kwa alama sita kidunia.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya mwaka huu ya Global Peace Index (GPI), inayotolewa na Taasisi ya Uchumi na Amani (IEP) yenye makao yake makuu mjini Sydney nchini Australia.

 

MGOMBEA wa nafasi ya ubunge katika jimbo la ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi