loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

AGNES SULEIMAN: Aliacha kazi ya Uhasibu, kageukia Bongo Muvi

“ NILIZALIWA miaka 29 iliyopita wilayani Temeke na kupata elimu ya msingi katika shule ya Wailes na baadaye nilihamia katika shule ya msingi Kibasila nilipohitimu elimu hiyo na baadaye kujiunga na Sekondari ya Dar es Salaam iliyopo Gerezani baada ya kufaulu,” ndivyo anavyoanza kusema Agnes Suleiman, mmoja wa wasanii wa sanaa ya uigizaji anayekuja juu kwa sasa kupitia fani hiyo.

Agnes hivi sasa anatamba katika tamthilia iitwayo PANGUSO inayooneshwa katika kituo cha televisheni cha Azam na anakiri kuwa kabla ya kufika hapo amepitia hatua mbalimbali hadi amefanikiwa ndani ya sanaa, jambo alililokuwa akilitamani na kulipenda tangu akiwa na umri mdogo.

Anasema akiwa mtoto wa miaka mitano, alikuwa na mazoea ya kujifunga vitenge kwa mitindo mbalimbali na kujitokeza mbele ya familia yake kujipitisha kama mshiriki fulani wa urembo ‘u miss’ jambo lililowafanya wazazi wake kumtabiria kuwa siku moja angejihusisha na sanaa ya urembo au sanaa ya mitindo.

Lakini pamoja na urembo pia alikuwa akipenda kuigiza vitu mbalimbali na hiyo ilitokana na familia yake kupenda kutazama filamu, huku akidai kuwa wakati mwingine alikuwa akiigiza vile vitu ambavyo wasanii walikuwa wakifanya kupitia filamu ama sinema anazoangalia, suala lililowafanya wazazi wake kumshangaa wakati wote kutokana na vipaji tofauti alivyokuwa navyo.

“Hata nilipowashirikisha kuwa nataka kuingia katika mashindano ya urembo, wazazi wangu waliniunga mkono na kuniamini, kuwa kitu ambacho nataka kukifanya kinatoka moyoni mwangu na si kama nataka kujiingiza kwa sababu nyingine, kikubwa waliniusia na kunitaka niwatunzie heshima kwa sababu kwa kipindi hicho sanaa ya urembo ilionekana kama ni uhuni,”anasema.

Agnes anasema wakati akisubiri matokeo ya kidato cha nne alishiriki mashindano ya ‘Miss Chang’ombe’ kwa kuwa ni kitu ambacho wakati wote alikuwa akitamani kufanya hivyo akidai kuwa hata alipokuwa mtoto wa miaka minne alikuwa na kipaji cha kupenda sana mitindo.

“Mama yangu alinisimulia kuwa hata pale ambapo nilikuwa nikiendelea kukua walikuwa wakishangazwa na vitendo vyangu vya uigizaji, nikiwaigiza wasanii mbalimbali vitu walivyokuwa wakifanya na kuigiza, wakati wote wazazi wangu walikuwa wakinitazama huku wakinitabiria kuwa ipo siku moja naweza kuwa mmoja wa wasanii wakubwa nchini,”anasema.

Kwa mujibu wa Agnes, wazazi wake walimuunga mkono aliposhiriki mashindano ya ulimbwende ya Miss Chang’ombe na baadaye Miss Temeke, bila kuchoka licha ya kwamba hakuweza kufanikiwa sana katika mashindano hayo, kwani alishika nafasi ya pili katika mashindano ya Miss Chang’ombe na nafasi ya nne katika mashindano ya Miss Temeke.

Agnes anasema wakati huo wote anafanya hayo, matokeo yake ya kidato cha nne yalikuwa hayajatoka na yalipotoka akawa amefaulu alikwenda kujiunga na Taasisi ya Biashara ijulikanayo kama Learnit Institute Of Business and Technology alikosoma na kuhitimu Shahada ya Biashara Mwaka 2015.

Huku akidai kuwa kipindi chote alichokuwa masomoni bado akili yake ilikuwa ikifikiria suala uigizaji na alikuwa akitumia muda wake mwingi kuangalia tamthilia mbalimbali kwa ajili ya kujijenga.

“Zaidi kipindi hicho nilikuwa nikifuatilia bongo muvi, nikiangalia wasanii kama Irene Uwoya, Johari Chagula ambaye nakiri kuwa katika filamu nyingi alizoigiza alikuwa akifanya vizuri na kunitamanisha sana nami niigize kama yeye… alimudu vyema uhusika wa huzuni, nilisema ipo siku lazima nitaingia katika uigizaji ili nitimize ndoto zangu,” anabainisha Agnes.

Anasema baada ya kuhitimu chuo na kurudi mtaani, aliajiriwa katika kampuni moja iliyopo jijini Dar es Salaam akifanya kazi ya Uhasibu huku akiendelea kufanya mazoezi mbalimbali ya uigizaji kwenye baadhi ya vikundi vya sanaa, mara nyingi alikuwa akienda baada ya muda wake wa kazi, kwani alikuwa na lengo lake kuu la kutimiza ndoto aliyokuwa nayo na hata kutabiriwa na wazazi wake tangu utotoni kuwa angeweza kufanikiwa katika sanaa hiyo ya uigizaji.

“Sikujiona kama nachoka licha ya kufanya vitu vingi kwa wakati mmoja kwa maana kazi na baadaye mazoezi ya uigizaji, hii ni kwa kuwa akili yangu yote muda mwingi ilikuwa ikiwaza kutimiza ndoto yangu.

Nilikuwa najisemea kuwa iwe leo au kesho lazima nitimize hii ndoto ya kufanya kitu kizuri katika jamii yangu,” anasisitiza Agnes.

Anasema mbali ya kutamani kuigiza pia wakati mwingine alitamani hata kuandika filamu na kuiigiza mwenyewe ili mradi afikie malengo yake na kutimiza kiu ya kutaka kuigiza.

Agnes anasema kadri siku zilivyokuwa zikienda ndiyo matamanio ya kuigiza yaliendelea na kudai kuwa wakati akiendelea na kazi yake alikutana na mtu mmoja kutoka kikundi cha sanaa kilichopo Bagamoyo ambaye alimshauri na kumtaka kwenda kujiunga nao ili aweze kujifunza zaidi, jambo ambalo binti huyo hakusita na kuamua kulifanyia kazi.

Anasema kutokana na mazingira ya jiografia ya umbali kati ya Bagamayo na Dar es Salaam alijiwekea ratiba ya kwenda huko kila ilipofika Ijumaa jioni na alikaa hadi Jumapili, akitumia muda mwingi kujifunza sanaa ya uigizaji na anadai kuwa kikubwa akichokuwa akifundishwa katika mazoezi hayo ni namna ya kuvuta hisia wakati wa kuigiza, kitu anachodai kuwa ni nadra kufanywa na wasanii wengi, yaani kulia kwa hisia na kisha kubadilika na kucheka ndani ya sekunde.

“Katika sanaa unatakiwa kujifunza vitu vingi, kucheka kwa furaha, kuonesha unyonge, kuchangamka na hata kuzungumza. Sanaa inabeba vitu vingi sana, namshukuru Mungu baada ya miezi kama mitatu hivi nilikuwa nimepata uzoefu wa kila kitu na hapo nikaona vyema kuacha kazi na kuamua kujikita rasmi katika sanaa ya uigizaji huku nikijishughulisha na ujasiriamali,” anasema Agnes.

Anasema baada ya hatua hiyo, kuna siku alikutana na Mustafa Faraji na yeye(Agnes) kujitambulisha kuwa yeye ni muigizaji na alimuomba kufanya kazi angalau katika filamu moja ili aweze kuonesha uwezo wake na alimkubalia na kumshirikisha katika filamu iitwayo Crazy Desire na baadaye Tamthilia ya Huba na sasa yupo katika tamthilia ya Panguso.

Agnes anasema kutokana na uwezo wake wa kubeba hisia ya kulia vizuri, muongozaji wa tathmilia hiyo Jimmy Mafufu aliamua kumpa kipengele kinachoendana na yale aliyojifunza Bagamoyo na kukiri kuwa hata bosi wake huyo anamsifu kwa kutendea haki uhusika wake tofauti na watu wengine.

Anasema hivi sasa sanaa ya uigizaji ndiyo kila kitu kwake kwa kuwa tayari imeshaanza kumpa mafanikio katika maeneo mbalimbali huku akiamini kuwa siku za usoni atakuja kuwa mmoja wa waigizaji wakubwa katika taifa hili na hata nje ya mipaka ya Tanzania kutokana na malengo aliyojiwekea lakini pia juhudi anazozifanya kufikia mahali hapo.

“Kwa urahisi huwezi elewa, mimi niliweka malengo, miaka saba iliyopita, niliweka kila kitu changu, nguvu, muda, rehani ya kazi yangu hadi nimefika hapa na naona mafanikio ya kile ambacho kwa muda mrefu nimekuwa nikikitafuta, najiona mbali sana…miaka miwili ijayo nitakuwa Agnes wa tofauti, nimepanga kuja kubadilisha tasnia nzima ya sanaa nchini,” anamaliza kusema Agnes.

Anasema anaamini mafanikio yake makubwa zaidi yatachangiwa pia na kujiendeleza, hivyo malengo yake baadaye ni kwenda kujiendeleza kimasomo katika masuala ya sanaa ili aweze kuchangia katika kuikuza sanaa ya uigizaji nchini na iweze kutoka na kutambulika kimataifa.

Agnes ambaye ni mtoto wa tatu kati ya watoto wanne wa Suleiman Kahamaba na Magreth Suleiman wenye makazi yao Mikocheni anasema anapenda kujifunza na kufanya vitu vipya vinavyoendana na masuala ya sanaa yake ili kufikisha ujumbe na kuleta mapinduzi ya kifikra katika jamii.

WANAWAKE wamekuwa ni chachu kubwa ya ...

foto
Mwandishi: Oscar Job

1 Comments

  • avatar
    Daud Jacob
    12/11/2020

    Hakika ni mwanamke jasiri na mwenye ndoto Kubwa, nimependa kwakweli. Mungu amjalie afanikiwe zaidi Kwenye UIGIZAJI. Amen

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi