loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Mlipuko wa watoto kuhara unabaki hisroria nchini’

MIAKA ya nyuma katika maeneo mengi ya nchi yetu, mlipuko wa ugonjwa wa kuhara kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano ulikuwa ya kawaida.

Kuhara kuliwafanya watoto kupoteza maji na hivyo kuishiwa nguvu. Baadhi yao walipona kwa kuwahishwa hospitali kupata tiba na kuongezewa maji lakini wengi walipoteza maisha.

Kilichokuwa kinawapata watoto hawa ni maambukizo ya virusi vya rota, vilivyosababisha waharishe sana na hivyo kuwa katika hatari ya kupoteza maisha yao

Lakini sasa, wakazi wa wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, bila shaka na maeneo mengi ya Tanzania, ni mashahidi kwamba sasa ugonjwa huo unaendelea kubaki historia.

Agnes Mahala na Hassan Henga, wakazi wa Kishapu ni miongoni mwa wazazi wanaothibitisha kwamba hawajasikia tena kwa muda mrefu mlipuko wa ugonjwa wa watoto kuhara kutokana na virusi vya rota.

 

Virusi vya rota ni nini?

Rota ni virusi vilivyo katika familia ya virusi aina ya Reoviridae. Virusi vya rota ndivyo kwa kiasi kikubwa husababisha ugonjwa wa kuhara miongoni mwa vichanga na watoto ambao hawajafikisha umri wa miaka mitano.

Inaelezwa kwamba karibu kila mtoto duniani alishawahi kuambukizwa virusi hivyo angalau mara moja katika kipindi cha tangu kuzliwa hadi kufikia umri wa miaka mitano.

Kinga za mwili huwa zinaimarika kadri mtu anavyoambukizwa na kuugua ugonjwa huo na ndio maana ugonjwa huo ni nadra kuleta madhara kwa watu wazima hata kama wataambukizwa virusi hivyo.

Virusi hivi mara nyingi huambukizwa kwa njia ya mdomo kwa maana ya kula au kunywa kitu chenye virusi hivyo. Mtoto anayeambukizwa virusi hivi bila ya kuwa na chanjo, hushambulia kuta za utumbo wake mwembamba na kusababisha kile kinachoitwa ‘mafua ya tumbo’ (gastroenteritis).

Ingawa ugonjwa huu ambao pia wanyama huupata uligunduliwa mwaka 1973, bado unaelezwa kuwa wa tatu katika kusababisha watoto wengi kulazwa hospitalini katika nchi nyingi za Afrika.

 

Kilichopunguza ugonjwa wa rota?

Agnes Mahala anasema chanjo ya rota ndio imesaidia sana kuwafanya watoto wasiharishe mpaka kuishiwa nguvu na kuwa katika hatari ya kupoteza maisha.

Agnes aliwahi kupoteza mtoto wake kwa ugonjwa huo wa kuharisha kutokana na kutochanjwa na anasema kwamba miaka ya nyuma ilikuwa ni nadra sana mtoto akishashambuliwa na virusi hivyo kupona.

“Tunaishukuru sana serikali kuleta chanjo hii ya rota na hivyo kudhibiti ugonjwa wa kuharisha kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano. Hapa Kishapu kwa sasa huu ugonjwa umebaki historia,” anasema.

Samoda Kilumba, mkazi wa Kishapu kutoka kabila la Wataturu anasema zamani katika kabila lao mtoto akiugua ugonjwa wa kuhara walikuwa wakimpa mkojo wa ng’ombe kama tiba lakini anakiri kwamba ulikuwa hausaidii sana kwani watoto wengi walipoteza maisha.

Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba anasema kuwa jamii imeanza kuelimika vyema kuhusu kuwapeleka watoto wao kupata chanjo hiyo ya rota na zinginezo.

Anasema inafurahisha kuona Wataturu wakifikia hatua ya kujenga zahanati na kwamba kwa sasa akina mama wengi wanahudhuria kliniki hatua inayosaidia sana kuokoa maisha ya watoto wao.

Mratibu wa chanjo katika halmashauri ya wilaya ya Kishapu, Jamila Mawazo, anasema ugonjwa wa kuharisha kwa watoto umebaki historia tofauti na miaka ya nyuma.

“Ukiona mtoto ameletwa hospitalini kwa tatizo la kuharisha ujue ni la kawaida katika mabadiliko ya mwili wake huenda anaota meno au kala kitu kichafu wakati wa kucheza kwake.

“Hakuna mtoto anayeletwa sasa akiwa mahututi kwa ajili ya tatizo la kuharisha kwani tangu kuanza kwa chanjo ya rota na wananchi wengi kuitikia tatizo limeisha,” anasema.

Anasema kuna vituo vya chanjo 53 kati ya 59 wilayani Kishapu vilivyoidhinishwa kutoa chanjo. Anasema pia wanazo friji 20 zinazoweza kutumia umemejua (sola) kwa maeneo yasiyo na umeme ambazo husaidia kuhifadhi dawa ili zisipoteze ubora wake.

Jamila anasema wanajitahidi kuhakikisha kwamba hakuna mtoto ambaye hapati chanjo na ndio maana mlipuko wa ugonjwa huo wa kuhara umetoweka.

Anasema mama mjazito anaanza kupata chanjo ya kumkinga mtoto na anapozaliwa mtoto anapata jumla ya chanjo tisa ikiwemo hiyo ya rota ili kuzuia magonjwa mbalimbali ya mlipuko.

Mratibu huyo wa chanjo anasema chanjo ya rota ya kwanza kwa mwaka 2019 wilayani humo ilifanikiwa kwa asilimia 129 na rota ya pili kwa asilimia 121.

Kwa mwaka 2020 anasema chanjo ya rota ya kwanza imefanikiwa kwa asilimia 114 na rota ya pili hadi mwezi Agosti ilikuwa imefikia mafanikio ya asilimia 108.

Jamila anasema kuwa wamekuwa wakitoa chanjo hiyo mara kwa mara ili kuwafikia watoto wote kwani wapo wazazi au walezi ambao hufanya uzembe kuwapeleka watoto kupata chanjo.

Marwa Ngutunyi, daktari bingwa wa magonjwa ya watoto   katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga anasema kuwa tatizo la kuharisha kwa watoto limepungua sana na kwamba kati ya watoto 10, mmoja ndiye anabainika kuwa na tatizo hilo.

Anasema chanjo ya rota imesaidia sana kupunguza ugonjwa wa kuhara kwa watoto ingawa bado wanakuja watoto wachache wakiwa na tatizo la kuharisha na nimonia au homa ya matumbo.

Dk Onesmo Mwegoha anayeshughulikia magonjwa ya mlipuko katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga anasema kuna asilimia 78 ya magonjwa ambayo hutoka kwa wanyama na kuingia kwa binadamu ukiwemo huo wa rota.

“Wataalamu walivumbua chanjo ya kukabiliana nayo, ndio maana hivi sasa baadhi ya magonjwa ya mlipuko yamebaki kuwa historia,” anasema akitaja magonjwa hayo kuwa ni pamoja na kuharisha, kifua kikuu na pepopunda.

Anasema mkakati wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ni kuondoa magonjwa ya mlipuko katika kipindi cha kuanzia mwaka 2017 hadi 2022.

Mratibu wa chanjo mkoa wa Shinyanga, Timothy Sosoma, anasema Sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009 inaeleza kwamba wazazi na walezi wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha kwamba watoto wanapelekwa kwenye chanjo, wanapatiwa huduma za afya na kupewa miongozo na matunzo.

Kwa upande wake, Meneja wa Mpango wa Taifa wa Chanjo, Dk Dafrosa Lyimo, anasema kuna magonjwa 13 yanayotibiwa au kuzuiliwa kwa chanjo.

Dk Lyimo anahimizwa wazazi na walezi kuhakikisha wanatimiza chanjo zote kwa ajili ya afya ya watoto wao.

Mkurugenzi wa chanjo nchini, Dk Leonard Subi anasema uwekezaji unaofanywa kwenye chanjo unaendana na mafanikio kwani kiwango cha upataji chanjo kimefikia asilimia 94 hadi 96.

Kuhusu ugonjwa wa rota anasema kutokana na chanjo hakuna hosipitali hapa nchini iliyotenga wodi kwa ajili ya watoto wenye ugonjwa wa kuharisha kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Dk Subi anasema wizara imetoa kipaumbele katika chanjo ambapo bajeti yake kwa sasa kwa kila mwaka ni shilingi bilion 50.

Anasema mpango wa taifa wa chanjo ulianza rasmi mwaka 1975 na zilikuwa zikitolewa chanjo tatu lakini sasa chanjo zinazotolewa ni tisa ikiwemo ya rota.

Anasema chanjo hizo zenye kuzuia magonjwa ya mlipuko  takribani 13 kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano zinatunzwa kwenye friji 1,385 zilizogharimu shilingi bilioni 13.

Anasema hatua ya kuwa na friji hizo inawezesha kusambazwa kwa chanjo kwenye hospitali na vituo vya afya katika halmashauri zote nchini.

INASIMULIWA kuwa miaka takribani 1000 iliyopita, eneo hili Ugogo ambalo ...

foto
Mwandishi: Kareny Masasy, Shinyanga

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi