loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Takwimu zinavyombeba Mwinyi Pemba

KWA muda nrefu kisiwa cha Pemba kilikuwa mithili ya ‘koloni’ la Maalim Seif Sharrif Hamad, lakini ukisoma makala haya hadi mwisho, utaona sasa mambo yamebadilika sana.

Mapokezi makubwa aliyoyapata Dk Hussein Mwinyi hivi karibuni yameonesha taswira mpya ya hali ya Pemba kisiasa ilivyo sasa.

Twende kitakwimu

Kura za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kisiwani Pemba hazijawahi kuzidi 20,000 kati ya wastani wa kura 125,000 zilizopigwa miaka ya 2010 na 2015. Mwaka huu wa 2020 wamejiandikisha wapigakura wapya 23,000 na kufanya idadi ya wapiga kura kisiwani humo kufikia 148,000.

Umati wa Wapemba uliojitokeza katika Uwanja wa Gombani ya Kale ulioko Chakechake kuja kumsikiliza Dk Mwinyi ni zaidi ya watu 60,000. Hawa ni mbali na wale waliojipanga mabarabarani kumpokea wakati akitoka Uwanja wa Ndege.

Tabia za Wapemba

Wapemba sio wanafiki. Kwa wapemba, itikadi za kisiasa zinafanana kabisa na imani za kidini.

Mtu akishajidhihirisha katika dini yake anakuwa muumini wa kweli wa dini hiyo sawana kwenye siasa na Wapemba wamedhihirisha hivyo kwa muda mrefu na sasa wanaonekana ‘kuhamia’ itikadi nyingine ya kisiasa.

Kwa Pemba ukiwa CCM basi wewe ni CCM na hata rafiki zako, ndugu zako na washirika wako ni kama wanapaswa wawe pia CCM. Na ukiwa  chama cha ACT-Wazalendo au Chama cha Wananchi (CUF) ni hivyo hivyo mpaka watakaokuzika ni hao hao!

Wapemba wanapiga kura

Wakati ambapo takwimu za wapiga kura zimekuwa zikipungua Tanzania Bara, Pemba hazijawahi kupungua.  Wakati wote zaidi ya asilimia 95 ya waliojiandikisha wamekuwa wakijitokeza kupiga kura.

Mpemba aliyepo Uingereza, Italia, Dubai, Oman, Qatar, Kamachumu, Liwale, Kakonko na hata Ukara, atajiandikisha na kuhakikisha anasafiri umbali wowote aliopo kwenda kupiga kura.

Wafuasi Diaspora

Hali halisi inaonesha kwamba Wapemba ambao wamebaki kuwa wafuasi kindakindaki wa Maalimu Seif ni waishio nje ya nchi, yaani diaspora.

Pengine ndio maana hata mipango ya ushindi ya ACT Wazalendo imeenda kupangwa Dubai. Kwa hali ya Dunia kwa sasa ambapo kuna ugonjwa wa corona (Covid-19) na kufungiana (lockdown) katika nchi zenye wafuasi hao kama ilivyo Uingereza, Ulaya na Canada pamoja na nchi za Kiarabu ni wazi wengi watashindwa kushiriki kupiga kura mwaka huu.

Lakini hata kama watakuja bado wapiga kura wa ndani ambao wamebadilika sana ndio wengi.

Umri wa wapigakura

Ukweli ni kwamba idadi ya Wapemba wahafidhina, yaani wafuasi wa Maalim Seif imeendelea kupungua kwenye daftari la wapigakura.

Vijana wenye maono, elimu na matarajio mapya wamejiandikisha kwa wingi na wengi wao wameanza ‘kuasi’ misimamo ya wazazi wao.

Takwimu za umri na jinsia zinaonesha kwamba asilimia 40 ya wapiga kura wana umri chini ya miaka 35 na walio na umri wa chini ya miaka 50 ni asilimia 87 ya wapigakura wote.

Ikiwa Maalim Seif ana umri wa miaka takribani 80, watu wenye umri huo (miaka 75 - 85) kwenye daftari la wapigakura ni pungufu ya asilimia moja.

Hawa ndio waliokuwa pamoja na Maalim, kusoma pamoja na kuishi pamoja na ndio bado wanaamini kwamba Maalim Seif anapaswa kutawala Zanzibar kutokana na kumjua na kumfahamu kwa undani. Lakini idadi kubwa wanawaza tofauti.

CCM imejipanga Pemba

Ushuhuda wa kazi nzuri iliyofanywa na Rais anayemaliza muda wake, Dk Ali Mohamed Shein na mipango ya CCM kisiwani humo inaonesha chama hicho kimejiimarisha zaidi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Ni kipindi hiki ndipo Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, alifanya ziara Pemba na kujichimbia visiwani humo kwa zaidi ya siku 45.

Dk Bashiru pia alitembelea kisiwa hicho na kufunga mitambo ya ushindi ya chama hocho kikongwe ambayo inaonesha imezaa matunda.

Ikumbukwe pia ni katika kipindi hiki wabunge na wawakilishi kutoka vyama vilivyokuwa na wafuasi wngi Pemba walijiuzulu na kujiunga na CCM.

Kazi kubwa ya Magufuli

Kama ilivyo kwa Watanzania wengi, kazi ambayo imefanywa na Rais Magufuli katika kupindi cha miaka mitano imewagusa na kuwafurahisha watu wengi.

Kazi hizo ni pamoja na kupambana na ufisadi, kuboresha uwajibikaji katika sekta ya umma na kusimamia vyema raslimali za nchi.

Dk Mwinyi ambaye ni Waziri wa Ulinzi wa Jeshi la Kujenga Taifa katika serikali Rais John Magufuli inayomaliza muda wake, bila shaka kuna watu wanaomwangilia kwa taswira ya Magufuli.

Hata yeye mwenyewe wakati anapitishwa na Mkutano Mkuu wa CCM kugombea urais Zanzibar atafuta nyayo za Rais Magufuli katika kupambana na rushwa, uzembe na ubadhirifu.

“Wako waliosema mimi ni mpole sana, lakini nimejifunza kutoka kwako (Magufuli) mambo ya msingi, rushwa, uzembe na ubadhirifu yanataka uwe mkali na hilo ninawaahidi endapo nitachaguliwa kuwa rais nitakuja na satili ya Rais Magufuli katika maeneo hayo,” aliahidi Dk Mwinyi.

Ilani ya CCM

Mbali na ukweli kwamba CCM inayoongozwa na Mwenyekiti Rais John Magufuli imebadilika sana na kuwavutia watu wengi, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita imedhihirisha kwamba ina uwezo wa kutekeleza kwa vitendo ilani yake.

Hiyo imekuwa kete nyingine inayombeba Dk Mwinyi na kuleta matumaini mapya kwa Wapemba na Wazanzibari wote.

Wakati ilani ya chama hicho inayomalizika imetekelezwa kwa sehemu kubwa, ilani mpya imesheheni mambo mengi ambayo Wapemba wengi baada ya kuwa na imani na CCM, sasa wana uhakika kwamba itatakekelezwa pia.

Mpasuko CUF, ACT, ADC

Kwa miaka mitano iliyopita, migogoro mikubwa imeikumba kambi ya upinzani. Chama Wananchi (CUF) kilipasuka vipande na Maalim Seif akahamia ACT Wazalendo.

Mpasuko huo umeacha athari kubwa Pemba ambako CUF bado haijakata roho. Wakati huo huo Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) ambacho nacho kilitokana na mpasuko ndani ya CUF miaka ya nyuma kimeendelea kujiimarisha.

Ingawa ushawishi wa Maalim Seif umeiwezesha ACT kujipenyeza Pemba, lakini ukweli ni kuwa chama hicho hakina nguvu kama ilivyokuwa CUF katika chaguzi zilizopita.

Sifa binafsi za mgombea

Waswahili wanasema, Wema hauozi na chanda chema huvikwa Pete.

Maisha ya Dk Mwinyi tangu wakati wote wa uongozi wake yamekuwa ni ya kujishusha. Tabia njema imekuwa ndio sifa kuu inayomtambulisha. Hana kashfa wala makandokando.

Dk Mwinyio ni kiongozi anayekubalika na vijana, anapendwa na wazee na watu wazima. Mapokezi yake Pemba yameakisi taswira ya mapenzi ya watu kwa mgombea huyu.

Uchunguzi unaonesha kwamba hakuna mgombea wa CCM aliyewahi kupata mapokezi hayo tangu kuanza kwa vyama vingi. Hata Dk Shein ambae amezaliwa Pemba na kuwa na ndugu huko sambamba na kuwafanyia Wapemba mengi hakuwahi kupata mapokezi makubwa kama hayo.

Lakini ukirudi kwa Maalim Seif, ingawa bado wapo wanaoamini kwamba anaweza kutawala lakini umri wake mkubwa umeanza pia kuwa majadala, wengi wakiona kama ‘amechoka’.

Nyota njema asubuhi

Waswahili husema kwamba nyota njema huonekana asubuhi. Takwimu hazidanganyi kuwa Dk Mwinyi sasa ndiye anayekuna mioyo ya Wazanzibari.

Hii inaonesha pia kuwa kura za Dk Mwinyi Pemba mwaka huu zitakuwa zaidi ya 90,000.

Mwandishi wa makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili.

 

 

KATIKA kipindi cha miezi michache iliypopita, dunia ...

foto
Mwandishi: Bwanku M Bwanku

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi