loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mdomo sungura usipewe tena nafasi kumnyima mtoto furaha

MDOMO sungura ni aina ya ulemavu ambao mtoto huzaliwa nao. Ugonjwa huu husababishwa na sehemu ya uso na mdomo kushindwa kufunga wakati mtoto anapokuwa akijiunda tumboni wakati wa ujauzito wa mama yake.

Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa tatizo hili huzikumba zaidi nchi za Afrika, Amerika na Asia licha ya kuwa katika Afrika halijawa kubwa kama ilivyo kwa mabara hayo mengine. Hapa Tanzania inakadiriwa kuwa watoto 2,500 huzaliwa na tatizo hilo kila mwaka.

Kwa mujibu wa Daktari Bingwa wa Upasuaji katika Hospitali ya Rufaa kanda ya Mbeya (MZRH), Dk Omary Matola, anazidi kufafanua kwamba kwa mtoto mwenye mdomo sungura, mdomo wake wa juu au chini wakati anazliwa huwa una nafasi (cleft lip).

Anasema wakati mwingine mtoto anaweza kuzaliwa akiwa na uwazi ndani ya mdomo kwa juu, yaani cleft palate na kwamba wakati mwingine mtoto anaweza kuzaliwa akiwa na matatizo yote mawili.

Dk Matola anasema tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa chanzo cha tatizo la mdomo sungura ni vinasaba (genetics) vya wazai wake.

Kwa lugha nyepesi anasema linarithiwa kutoka kwa mama au baba, kama mmoja wao lipo kwenye ukoo wake, kuna uwezekano kupata mtoto mwenye tatizo hili.

Anasema pia kuna visababishi vingine ambavyo kama mama atakutana navyo wakati wa ujauzito, hasa miezi mitatu ya mwanzo, mtoto anaweza kuzaliwa akiwa na tatizo la mdomo sungura.

Vitu hivyo anavitaja kwamba ni pamoja na uvutaji sigara, unywaji pombe uliokithiri, matumizi ya baadhi ya dawa ikiwemo za degedege, lishe duni na hata uzito uliopitiliza unaweza kuchangia kwa kiasi fulani kupata mtoto mwenye tatizo hili.

 “Lishe duni kwa mama mjamzito inayoweza kumsababishia mtoto tatizo ni kukosa virutubisho muhimu kama vile madini ya folic acid. Pia kuna sababu za kimazingira ambazo hutokea wakati mama akiwa mjamzito ikiwa ni pamoja na mama kutopata hewa ya oksijeni ya kutosha wakati wa ujauzito (maternal hypoxia),” anafafanua Dk Matola.

Anaongeza: “Katika uumbaji wa uso unakuwa na hatua kama tatu ambazo ni sehemu ya juu ya uso, pembeni na sehemu ya chini ambazo zinakuja na kukutana katikati ili kutengeneza uso. Katika mchakato huo inaposhindikana kuungana katikati ndio husababisha ulemevu wa uso na mdomo au mdomo sungura. ”

Daktari bingwa wa upasuaji katika hospitali ya Tumbi mkoani Pwani, Dk Silas Msangi katika makala yake kuhusu mdomo sungura iliyochapishwa Juni 24 mwaka 2018 katika gazeti la Nipashe anasema uchunguzi unaonesha kuwa ugonjwa wa mdomo sungura umegawanyika katika sehemu kuu tatu.

Sehemu ya kwanza anasema mtoto anaweza kuzaliwa sehemu ya mdomo na pua vikiwa vimeathirika. Sababu ya pili anasema ni sehemu ya juu ndani ya mdomo inakuwa na uwazi na aina ya tatu mtoto anakuwa na vyote viwili sehemu ya nje ya mdomo, pua na ndani ya mdomo unakuwa na uwazi.

 Dk Msangi anasema sehemu ya nje ambayo inahusisha mdomo na pua mara nyingi watoto wa kiume ndiyo wanaathirika zaidi ikilinganishwa na wa kike.

Sababu za moja kwa moja anasema haijajulikana ni kwa nini wanaume wanapata tatizo hilo na kwamba takwimu zinaonyesha hivyo na kwenye sehemu ya ndani ya juu ya mdomo watoto wa kike ndiyo huathirika zaidi.

Kutokana na tatizo la mdomo sungura watoto waliozaliwa na ugonjwa huu hukabiliwa na changamoto za aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na kushindwa kunyonya hasa kwa wale walio na mdomo wazi wa ndani,

Matatizo mengine Dk Masangi anasema ni kupata maambukizi ya sikio na kupelekea usikivu finyu, matatizo ya kinywa na meno na kama atakosa matibabu ya mapema atakuwa na matatizo kwenye uzungumzaji.

Tatizo lingine la kisaikolojia anasema a unyanyapaa. Kwa mujibu wa Dk Matola ugonjwa huo unachukuliwa kwa namna tofauti tofauti na wanajamii.

Anasema licha ya jitihada zinazofanywa na Serikali nchini kwa kushirikiana na wadau mbalimba kutoa elimu bado wapo wazazi na walezi wanaoendelea kuamini kuwa katika familia au ukoo kuzaliwa kwa mtoto aliye na tatizo la mdomo sungura ni nuksi na hivyo baadhi yao kuwafungia ndani watoto hao.

 Anawaalika wakazi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na maeneo jirani kuitumia fursa ya utoaji bure Huduma ya Matibabu ya Mdomo Sungura inayofanyika katika Hospitali ya Rufaa, kanda ya Mbeya (MZRH) kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Kimarekani la Smiletrain kutibu watoto hao.

 Akizungumzia mradi wa utoaji wa huduma hiyo unaoendelea katika hospitali hiyo, Dk Matola anasema ni wakati kwa jamii kuachana na dhana hizo potofu na badala yake kuzitumia fursa za utoaji bure wa huduma za upasuaji katika hospitali mbalimbali nchini zinazotoa huduma hiyo ikiwemo MZRH.

 Anazitaja hospitali nyingine zinazotoa huduma hiyo bure kwa sasa hapa nchini kuwa ni KCMC ya mkoani Kilimanjaro, Bugando ya Mwanza, Siriani ya Arusha, Dodoma, Tumbi mkoani Pwani na CCBRT jijini Dar es Salaam.

 “Mdomo sungura ni tatizo la kuzaliwa kama matatizo mengine na linatibika. Tuachane na dhana kuwa ukizaa mtoto mwenye tatizo hili kuwa ni nuksi kwenye ukoo au familia. Ni jambo la kusikitisha mpaka leo hii pamoja na jitihada zinazofanywa na serikali na wadau wengine bado kuna watu wanawafungia ndani watoto wenye matatizo haya,” anasema Dk Omary.

 “Tuwafanye watoto wanaozaliwa na tatizo hiyo kuwa na furaha kama wenzao kwa kuwawahisha kuja kupata matibabu ili warejee kwenye hali zao za kawaida. Tuwape uhuru wa kushirikiana na wenzao katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya michezo, masomo na pia kwenye nyumba za ibada. Wataalamu tupo, wafadhili wapo kwa nini umfungie mtoto ndani?” Anahoji.

 Hata hivyo Dk Omary anasisitiza mambo yanayopaswa kuzingatiwa kabla ya mtoto kupelekwa Hospitalini kwaajini ya upasuaji wa mdomo sungura kuwa ni pamoja na mtoto awe ametimiza umri wa miezi mitatu,awe na uzito usiopungua kilogramu tano na uwingi wa damu usiwe chini ya 10.

 

Zipo shuhuda mbalimbali za watu waliozaliwa wakiwa na tatizo la mdomo sungura nchini lakini walifanyiwa upasuaji na kupona kabisa. Mfano mzuri ni wa binti  mtanzania Agnes aliyenukuliwa katika chapisho la Juni 12 mwaka 2018 katika mtandao (news.un.org/sw/story/2018/06/1018702) akizungumzia livyokutana na mtu aliyempa anuani ya Hospitali ya CCBRT alipokwenda jijini Dar es Salaam kutafuta kazi na akaenda kutibiwa na kurejesha furaha yake aliyoisubiri mpaka anafikisha umri wa miaka 14 mwaka 2009 alipofanyiwa upasuaji.

 Kwa shuhuda za watu kama binti Agnes hakuna haja ya jamii kuendelea kuona ugonjwa huu ni tatizo la kusumbua bali kufuata ushauri wa kufuata matibabu katika maeneo yanayotajwa.

Wazazi na walezi tusijitengenezee lawama zisizo za msingi kwa watoto watakaoendelea kubaki na tatizo hili kwa kutowapeleka hospitali.

 

INASIMULIWA kuwa miaka takribani 1000 iliyopita, eneo hili Ugogo ambalo ...

foto
Mwandishi: Joachim Nyambo

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi