loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tunduma kuwa kitovu biashara Afrika, Asia

SERIKALI imesema mipango imekamilika kubadili mji wa Tunduma kuwa kitovu cha biashara na eneo muhimu la kiuchumi kwa Bara la Afrika na Asia.

Hatua hii inalenga pia kutengeneza ajira na kuwa miongoni mwa miji mikubwa kimaendeleo nchini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Viwanda, Profesa Riziki Shemdoe, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam alipozungumza na ujumbe wa Mkoa wa Songwe uliofika jijini humo kwa ziara ya mafunzo katika eneo la Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA).

"Jiji la Tunduma liko katikati ya masoko ya kikanda ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika; linaunganisha Soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Soko la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Sasa ni wakati wa kutekeleza mpango huu utakaomnufaisha Mtanzania kwa kuongeza fursa," alisema.

Shemdoe alisema tayari mipango ya kuufanya mji huo kuwa kitovu cha biashara kwa Bara la Afrika na Asia imekamilika na hivyo, kuwa eneo muhimu la uchumi na ajira nchini.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, Dk Seif Shekhalage, alimwambia Katibu Mkuu kuwa, Mkoa wa Songwe umetenga ardhi hekta 400 kwa ajili ya Ukanda Maalumu wa Uchumi (SEZ) utakaovutia ujenzi wa miradi ya kimkakati ya maendeleo ya uchumi.

"Ardhi iliyotengwa kwa SEZ itatumiwa kuvutia wawekezaji kwa ujenzi wa viwanda na bandari kavu kwani takwimu zinaonesha karibu shehena nyingi za mizigo inayoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam, inasafirishwa katika nchi za SADC kupitia mpaka wa Tunduma," alisema Dk Shekhalage.

Kutokana na hilo, Shekilage alisema eneo hilo la viwanda litakuwa limewasogeza wazalishaji wa bidhaa karibu na soko la SADC wakati huo huo, bandari kavu ikipokea shehena kutoka Reli ya Tanzania Zambia (Tazara) na kuchukua kwenye bandari kavu iliyo karibu katika Mji wa Tunduma kabla ya kusafirishwa kwenda nchi za nje.

"Hali hii itakuza biashara zaidi na kutoa ajira kwani hivi sasa, malori 120 ya mafuta na malori 80 ya mizigo husafirisha bidhaa katika nchi za Zambia, Malawi, Zimbabwe na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kila siku kupitia hapa," alisema.

Katibu Tawala huyo wa Mkoa wa Songwe alisema mradi huo utakuza utalii wa kiafya kwani mji huo ndani ya miaka mitano utakuwa Jiji la Tunduma na Serikali tayari imetenga Sh bilioni tano kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya kiwango cha juu cha tiba itakayohudumia pia nchi za SADC.

Kwa sasa, Kituo cha Afya cha Tunduma kinahudumia takriban wagonjwa 250 wa kigeni kwa siku.

Mkurugenzi wa Uwekezaji na Uhamasishaji wa EPZA, James Maziku, alisema Mji wa Tunduma ni lango kwa nchi za Ukanda wa SADC  na Afrika kwa jumla kwani biashara nyingi za kimataifa zinafanywa na nchi za Asia na hutumia Bahari ya Hindi kama ukanda muhimu wa biashara.

 

 

 

 

Watanzania 4,247 wamepata ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi