loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JPM aagiza vijiji 61 Uvinza vipate umeme

RAIS John Magufuli amemuagiza Waziri wa Nishati, Dk Merdad Kalemani ahakikishe vijiji 61 katika Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, vinapata umeme kwa kuwa katika miaka mitano vijiji 17 tu vimepata nishati hiyo.

Alitoa agizo hilo jana akiwa njiani kutoka Uvinza kwenda Tabora kwenye mikutano ya kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akifafanua kuhusu umeme, Rais Magufuli alisema mwaka 2015 vijiji vilivyokuwa na umeme nchini, vilikuwa 2,500 lakini ndani ya miaka mitano jumla ya vijiji 7,200 vimepata nishati hiyo.

Kwa kuzingatia idadi hiyo hadi sasa vijiji vyenye nishati hiyo ni 9,700 na vilivyobaki ni 2,018.

“Sasa ukiangalia vijiji vingi vimefikiwa na umeme lakini hapa Uvinza ndani ya miaka mitano sasa ni vijiji 17 tu vyenye nishati hiyo, bado vijiji 61, hii niseme wazi haijanifurahisha, ni kero, na Waziri wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako uko hapa, kamweleze Waziri Nishati sijafurahishwa,”alisema Rais Magufuli.

Aliongeza: “Hapa Uvinza hatujafanya vizuri kwenye umeme, niachieni hili. Nitawabana vizuri watu wangu, Waziri wa Nishati kama ananisikia, hii ni changamoto, kwa sababu bado ni waziri,”

Alisema Wilaya ya Uvinza imebadilika na imekuwa na maendeleo zaidi, huku viwanda vikijengwa kikiwemo kiwanda cha chumvi.

Magufuli alisema serikali itakiboresha kiwanda hicho na kuhakikisha umeme unakuwa wa uhakika, ili kitoe fursa nyingi za ajira na kuzalisha chumvi nyingi itakayouzwa ndani na nje ya nchi.

“Hapa Uvinza ni pa tofauti, kuna kiwanda cha chumvi, tunataka tukiboresha tuuze hadi nje na ajira ziwepo, Waziri wa Viwanda na Biashara naye asikie hili alibebe”alisema.

Alisema suala la tatizo la umeme wilayani Uvinza ni kubwa na lipo tangu Uhuru, lakini serikali imeliona na ndio maana mikakati  ya kuongeza uzalishaji wa umeme inaendelea, ukiwemo ujenzi wa bwawa katika Mto Rufiji, utakaozalisha zaidi ya Megawati 2,100. Alisema wilaya hiyo itaunganishwa kwenye Gridi ya Taifa.

“Hili tatizo la umeme litaisha, tukianza kupata umeme kutoka mradi wa kuzalisha umeme kwenye Mto Rufiji ambao tunategemea kuzalisha zaidi ya megawati 2,100 tutaunganisha wilaya hii kwenye gridi, kwa sababu fedha zipo zaidi ya Sh bilioni  2.18”alisema.

Akizungumzia changamoto za wananchi wa Uvinza, Magufuli alisema pamoja na mkoa wa Kigoma kuwa na Ziwa Tanganyika, bado unakabiliwa na changamoto ya maji na kwamba serikali imeliona hilo na kutoa Sh bilioni 11.06 kwa ajili ya miradi ya maji.

Alisema miradi hiyo baadhi imekamilika na mingine inaendelea kujengwa na iko katika maeneo ya mbalimbali na baadhi yake ni Nguruka, Kandaga, Katete, Mgambazi na Kazuramimba.

Aidha kwenye sekta ya elimu, Magufuli alisema madarasa 84 yamejengwa, huku pia maabara, vyuo vya mafunzo na hosteli kwa ajili ya wanafunzi zimejengwa kwa kutumia Sh bilioni 5.04. Fedha nyingine shilingi bilioni 7.63 zimetumika kugharamia elimu bure.

Akiwa eneo la Nguruka, Magufuli alisimama na kuzungumza na wananchi kisha kuomba kura. Alimuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, ahakikishe  anashughulikia suala la kituo cha afya cha Nguruka kipande hadhi.

“Nataka nitoe agizo hapa, nazungumza kama Rais, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, niliahidi hapa nitapandisha hadhi Kituo cha Afya cha Nguruka ili kiwe kinatoa huduma kwa watu wengi na hawawezi kwenda pengine kwa sababu ya umbali, sasa kipandishe hadhi, kiongeze wataalamu na madaktari, ili hata tiba kwa upasuaji zifanyike hapa,”alisema Magufuli.

WASIMAMIZI wa vituo na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi,wameonywa kujiepusha na ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi