loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Choroko; bidhaa yenye soko kubwa ndani, nje

CHOROKO ni zao ambalo lilianza kulimwa nchini tangu miaka ya 1880 likiwa limeletwa na wafanyabiashara wa Kiarabu lakini inasemekana asili ya zao hili ni India.

Moja ya sifa kuu ya zao hili ni kustahimili ukame kwa maana halihitaji mvua nyingi kama mazao mengine na pia linakomaa kwa muda mfupi.

Choroko ni chakula chenye kiwango kikubwa cha protini na madini ya phosphorus na calcium na hivyo husaidia kwa kiwango kikubwa kuimarisha mifupa mwilini.

Inaelezwa na wataalamu kwamba choroko husaidia afya ya moyo kutokana na mafuta yaliyopo ndani yake kuwa ni salama na pia husaidia umeng’enywaji wa chakula tumboni.

Choroko ina vitamin B1, B2 ambayo husaidia kuimarisha mfumo wa fahamu na tafiti zinaonesha kwamba watu wengi ambao hutumia choroko katika mlo wao ni miongoni mwa watu ambao fahamu zao zimekaa vyema. Choroko pia inatajwa kuwa lishe na kinga muhimu kwa  mjamzito.

Katika kutambua umuhimu wa zao hili, watafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kituo cha Ilonga kilichopo mkoani Morogoro wamejikita katika utafiti wa mbegu mpya ya choroko yenye madini mengi ya chuma.

Mtafiti wa Mikunde wa Kituo cha Tari Ilonga, Dk Beatrice Mwaipopo anasema hivi sasa kuna mahitaji makubwa ya soko la choroko nchini na nje ya nchi.

Lengo la kufanya utafiti huo anasema ni katika harakati za kusaidia kundi kubwa la  wajawazito ambao baadhi yao huwa wanakabiliwa na  upungufu wa damu kutokana na miili yao kukosa au kuwa na upungufu wa madini chuma.

Na kwamba ulaji choroko hizi zenye madini ya chuma ya kutosha ni faida pia kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.

Dk Mwaipopo anasema kwa kutambua mahitaji ya soko, Tari Ilonga chini ya idara yake imefanya tafiti kwenye zao hilo na kwamba tayari wametafiti aina 28 za mbegu na kwamba kati ya hizo zimepatikana mbegu mbili za choroko zenye madini mengi ya chuma.

Anasema kwa sasa tayari aina mbili za mbegu za choroko zimepelekwa kwenye  Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), kwa ajili ya kuidhinishwa ili ziweze kuzalishwa zaidi na kusambazwa kwa wakulima nchini.

“Madini ya chuma ni chanzo kikuu cha kuzalisha damu mwilini na kwa Tari Ilonga tunajikita kwenye kazi kubwa ya utafiti wa eneo hili la choroko,” anasema Dk Mwaipopo.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Dk Geofrey Mkamilo anasema ulaji wa vyakula vitokanavyo na mikunde ikiwemo choroko ni muhimu kwa wananchi ikiwa ni pamoja na watu wenye umri mkubwa.

Anasema wakati huu ambao tafiti nyingi zinaonesha nyama nyekundu ina madhara kadha wa kadha mwilini, ulaji wa choroko kwa ajili ya kujipatia protini unakuwa muhimu zaidi.

“Inashauriwa watu wenye umri mkubwa wapende kula vyakula vya jamii ya mikunde ili kujipatia protini badala ya kupenda kula nyama ambayo mara nyingi pia ni ghali kulinganisha na mimea jamii ya kunde,” anasema Dk Mkamilo.

Dk Mkamilo anasema mkakati wa Tari ni kuendeleza utafiti kwenye mazao mengine ya jamii ya kunde katika vituo vyake vilivyopo nchini.

Anasema licha ya kutenga bajeti ya zaidi ya Sh bilioni 15 zitakazotumika kuendeleza utafiti wa upatikanaji wa mbegu bora za mazao hususani ya alizeti, mahindi na maharage kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya soko la ndani ya nchi mkakati huo ni pamoja na zao hilo la choroko.

Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) linatilia mkazo uzalishaji wa vyakula vyote vya jamii ya kunde kutokana na kuwa na kiwango kikubwa cha protini na hivyo matumizi yake kuwa badala ya nyama.

Shirika hilo lilibainisha hayo miaka kadhaa iliyopita kwenye uzinduzi wa mwaka wa kimataifa wa vyakula jamii ya kunde.

FAO inasisitiza kwamba kilimo cha mazao jamii ya kunde huchangia kulinda uhai wa ardhi na kuimarisha kipato cha wakulima na kwamba vyakula jamii hiyo vinakuwa na asilimia hadi 25 ya protini.

Katika suala la lishe ya mama na mtoto, Mganga Mkuu mkoa wa Morogoro, Dk Kusirye Ukio, anabainisha kuwa suala la lishe bora bado ni tatizo kubwa katika jamii ikiwemo wakazi wa mkoa huo.

Kutokana na ukosefu wa lishe bora, Dk Ukio anasema wamekuwa wakipokea wagonjwa ambao kama wangezingatia ulaji mzuri wa vyakula wasingelazimika kufika hospitali, ikiwa ni pamoja na upungufu wa damu. Anafafanua kwamba upungufu wa damu ni tatizo kubwa kwa wajawazito.

“Mama asipokuwa na damu ya kutosha na akicheleweshwa kupata huduma  hili ni tatizo kwa mama mwenyewe na hata kwa mtoto anakuwa na damu ndogo,” anasema Dk Ukio.

Hivyo anasema ulaji wa vyakula bora husaidia kujenga mwili na kurekebisha seli za mwili zilizoharibika na hivyo anashauri wananchi kupendelea kula kwa wingi maharage, njegere, kunde, karanga, soya, njugu mawe, dengu, choroko na fiwi.

Vyakula vingine anavyohimiza daktari huyo ni pamoja na nyama, samaki, dagaa, maziwa, mayai, jibini, maini, figo, senene, nzige, kumbikumbi na wadudu wengine wanaoliwa.

Jukwaa la Chakula nchini (PANITA) limekuwa likitahadharisha watu juu ya njaa iliyofichika kwa maana miili yao kukosa baadhi ya virutubisho muhimu licha ya kula na kushiba.

Panita limekuwa likisema Watanzania wengi wanapenda kula kinachowavutia kwenye midomo yao na siyo kinachohitajika na miili yao na hivyo wengi kuwa na upungufu wa aina nyingi za virutubisho katika miili yao. Jukwaa hilo limekuwa likisisitiza kwamba Watanzania wengi wanaweza kupata vyakula vya wanga na hata protini lakini wamekuwa na upungufu wa madini na vitamini.

 

MCHICHA ni aina nyingine za ...

foto
Mwandishi: John Nditi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi