loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wakala wafanya operesheni kukagua vipimo vya dhahabu

WAKALA wa Vipimo nchini (WMA), unaendesha operesheni za kushtukiza kukagua mizani inayotumika kupima dhahabu ili kuhakikisha serikali inapata kodi stahiki.

Aidha, wakala huo unafanya operesheni hizo ili kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria, wanaofanya udanganyifu kwa kuchezea mizani ili wajinufaishe zaidi kinyume na sheria na taratibu.

Ofisa Vipimo wa WMA Geita, Chrispinus Aloyce alibainisha hayo wakati akizungumzia ushiriki wa taasisi yake katika Maonesho ya Tatu ya Madini yanayofanyika katika Viwanja vya Bombambili Mwatulole, mkoani Geita.

Alisema miongoni mwa majukumu na mchango mkubwa wa WMA katika sekta ya madini nchini, ni pamoja na kuhakikisha biashara hiyo haifanyiki bila kuwa na mizani sahihi na iliyohakikiwa na wakala ili kutambua uzito halisi wa dhahabu inayonunuliwa au kuuzwa.

Alisema jukumu lingine kubwa la WMA katika sekta hiyo ni kuhakikisha mizani yote inayotumika kuuzia na kununulia vito na madini inahakikiwa na inapima madini kwa usahihi.

Kwa mujibu wa Chrispinus, taasisi hiyo pia inatoa ushauri wa kitaalamu mintarafu mizani zinazopaswa kutumika kuuzia madini.

“Alama zinazowekwa katika mizani iliyohakikiwa ni stika pamoja na lakiri ambayo inakuwa na nembo ya taifa pamoja na tarakimu mbili za mwisho za mwaka husika mfano (20) ikiashiria imehakikiwa 2020,” alisema.

Aidha, Chrispinus alibainisha kuwa lengo lingine la WMA kufanya uhakiki wa mizani ya kuuzia na kununulia madini ni kuhakikisha matumizi ya mizani sahihi iliyohakikiwa yanazingatiwa na kunakuwa na biashara ya usawa na haki hali itakayowezesha serikali kukusanya mapato kwa usahihi na wauzaji wa madini wanapata fedha stahiki.

Alisema baada ya uhakiki wa mizani inayotumika kuuza na kununulia madini, Wakala wa Vipimo hufanya ukaguzi wa kushtukiza mara kwa mara katika masoko ya kuuzia madini ili kujiridhisha kama mizani bado ipo sahihi na inatumika kwa usahihi kama inavyostahili.

Watanzania 4,247 wamepata ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Geita

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi