loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Z’bar na athari za corona kwenye utalii, ujasiriamali

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema mchakato wa kufanya tathmini za athari za ugonjwa wa Covid-19 uliozorotesha shughuli za maendeleo kwa makundi mbali mbali ya vijana, wajasiriamali pamoja na sekta ya utalii upo katika hatua ya mwisho kukamilika nchini.

Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa anasema Serikali imepunguza kodi za leseni kwa wafanyabiashara ndogo na mama lishe ambao sasa wanapaswa kulipa Sh 30,000 kwa mwaka na kupewa kitambulisho ambacho kitawapunguzia usumbufu uliokuwepo awali.

Anasema Serikali inafahamu kuwepo kwa maumivu makubwa ya wafanyabiashara na wajasiriamali ikiwemo vijana ambao shughuli zao za kuwaingizia kipato zimeathiriwa na ugonjwa wa covid-19 kwa zaidi ya miezi minne sasa.

Balozi Ramia anasema uchumi wa Zanzibar umeyumba kama zilivyo nchi nyingine kutokana na athari za ugonjwa huo wa covid-19 ambapo ukuaji utakuwa kwa asilimia 3.5.

Akifafanua zaidi anasema Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zipo katika hatua za mwisho za kufanya tathmini ili kujua athari zilizowapata wajasiriamali hao ikiwemo vijana katika kipindi cha zaidi ya miezi minne kutokana na ugonjwa huo.

Balozi anakiri kwamba utalii umeathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na watalii kutokuja nchini kwa zaidi ya miezi minne kufuatia janga la ugonjwa wa covid 19.

Anasema sekta ya utalii Zanzibar imeajiri zaidi ya vijana 20,000 wanaofanya kazi katika hoteli za kitalii huku wengine 15,000 wakijiajiri kwa kutegemea sekta hiyo wakiwemo wale wanaopeleka bidhaa hotelini vikiwemo vyakula na samaki. 

''Tumepokea malalamiko mengi kutoka kwa wawekezaji na waajiriwa katika hoteli za kitalii... Wameathirika sana na ugonjwa wa corona ambapo wapo vijana wetu wanaotoa huduma za usambazaji wa vyakula mahotelini wamesitisha huduma hizo huku wengine wakidai fedha nyingi,” anasema.

Tayari Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefungua milango kuruhusu watalii kuingia na ndege kuleta wageni kwa ajili ya shughuli za utalii huku wakitakiwa kufuata masharti ya kujikinga na ugonjwa wa corona.

Uamuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuangalia uwezekano wa kuwasaidia wajasiriamali na wafanyakazi katika sekta ya utalii limepokewa kwa mikono miwili.

Juma Iddi ambaye ni mtembezaji wa watalii katika maeneo ya Mji Mkongwe anasema kwa zaidi ya miezi minne sasa hajafanya kazi hizo kutokana kukosekana kwa watalii kutoka nje baada ya kuzuka ugonjwa wa covid-19.

“Nimeathirika kiuchumi tangu Serikali kufunga shughuli za kupokea watalii kwa zaidi ya miezi minne sasa... Hata familia yangu imeyumba kwa sababu mimi nina mke na watoto watatu ambao wote wananitegemea mimi,” anasema.

Aidha Hamad Ali, ambaye huuza vyakula vinavyopendwa na wageni ikiwemo urojo wa pweza na ngisi pamoja na kamba, anasema kwa zaidi ya miezi minne sasa eneo la Forodhani limefungwa baada ya kukosa watalii ambao hupendelea kufika eneo hilo kupata vyakula vya Kizanzibari hususani nyakati za jioni.

''Nilikuwa ninaingiza kwa siku Sh 150,000 kwa kupika vyakula vinavyowavutia watalii... Lakini katika kipindi cha miezi minne cha corona nimeshindwa kufanya biashara hivyo kuyafanya maisha yangu kuwa magumu,” anasema akiitaka Serikali kufanya tathmini kwa watu walioathirika na ugonjwa huo ikiwemo wajasiriamali na kuona namna ya kusaidia.

Akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2020-2021, Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Mahmoud Thabit Kombo alisema Serikali tayari imefungua milango kwa watalii kuja nchini kwa kufuata masharti ya kujikinga na ugonjwa wa covid-19.

Aliyataja masharti hayo kuwa ni pamoja na wageni wanaokuja nchini kutakiwa kufanya vipimo katika nchi zao na wanapoingia nchini pia wanafanyiwa tena vipimo.

Aidha watalii watakaotembelea nchini wanatakiwa kuvaa barakoa, ikiwa ni moja ya hatua ya kujikinga na ugonjwa huo katika kipindi chote watakapokaa nchini.

''Tumefungua milango na kuwataka watalii waje nchini baada ya kupata afuweni kubwa katika ugonjwa wa corona... Lakini tumeweka masharti ya kujikinga na ugonjwa huo ili kuepuka maambukizi mapya,” anasema.

Sekta ya Utalii Zanzibar huchangia pato la taifa kwa asilimia 27 lakini moja ya mafunzo yanayopatikana kwenye corona ni umuhimu wa uwekezaji katika miradi ya ujenzi wa viwanda ili kutoa ajira kwa kundi kubwa la vijana.

Uongozi wa Kanisa la Anglikana lililopo Mji Mkongwe wa Zanzibar lipo katika matayarisho ya kuanza kutoa ruhusa ya watalii kutembelea eneo hilo ambalo ni la kihistoria hususani lilipokuwa kichocheo cha kuondoshwa kwa biashara ya utumwa duniani.

“Tunakusudia kuanza kupokea wageni katika kanisa letu ambapo mipango yote imekamilika... Tumepata athari kubwa za corona katika kipindi cha miezi minne tulichositisha huduma za kupokea watalii,” anasema Askofu wa Kanisa la Anglikana, Michael Hafidh.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Khamis Mussa anasema Serikali katika bajeti ya mwaka wa fedha 2020-2021 inakusudia kukusanya Sh bilioni 580 kutoka katika vyanzo vyake vya ndani, huku jumla ya Sh bilioni 921 zikikusanywa katika kodi ya mapato.

“Tumejipanga kukusanya kiwango cha Sh bilioni 580 katika vyanzo vyetu vya kodi ingawa kiwango hicho kinatarajiwa kushuka kwa sababu ya mapato mengi ya utalii kukosekana,” anasema.

Mussa anasema Serikali inatarajiwa kutumia bajeti ya Sh trilioni 1.579,200, ambapo kati ya fedha hizo Sh bilioni 969.3 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida wakati Sh bilioni 609.9 ni kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

Wajasiriamali mbalimbali ikiwemo wanaozalisha bidhaa za sabuni ya maji ambao walipata mafunzo katika mradi wa kuwawezesha wajasiriamali WEZA III kwa kushirikiana na Tamwa Zanzibar, wao walitumia janga la corona kutengeneza fedha kwa kuuza sabuni kwa ajili ya watu kunawa mikono.

Mjasiriamali Fatuma Haji kutoka Chaani mkoa wa Kaskazini, Unguja anasema wakati wa kipindi cha ugonjwa wa covid-19 bidhaa zake za sabuni ya majii zilikuwa na soko zuri na la uhakika.

 

MCHICHA ni aina nyingine za ...

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman, Zanzibar

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi