loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

TRA ilivyoipa jeuri serikali kujenga miradi mikubwa

ONGEZEKO la ukusanyaji mapato kutoka shilingi trilioni 10.67 katika mwaka wa fedha 2014/2015 hadi kufikia shilingi trilioni 17.87 mwaka wa fedha 2019/2020 ni moja kati ya mambo ambayo serikali inajivunia kupitia mamlaka iliyopewa jukumu kukusanya kodi nchini, Mamlaka ya Mapato (TRA).

Tangu mwaka 2015 baada ya uongozi wa Serikali ya Rais John Magufuli kuingia madarakani makusanyo yalianza kuongezeka mwaka hadi mwaka.

Kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa TRA, Dk Edwin Mhede makusanyo hayo ni ongezeko la wastani wa kutoka shilingi bilioni 850 zilizokuwa zinakusanywa kwa mwezi kabla ya serikali ya Magufuli kuingia madarakani hadi kufikia wastani wa shilingi trilioni 1.5 kwa mwezi, sawa na ongezeka la asilimia 76 kwa mwezi.

Dk Mhede anasema mafanikio ya ongezeko la ukusanyaji kodi uliofanywa na TRA ndiyo pia umeipa jeuri serikali ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na huduma za jamii.

Kati ya miradi hiyo ipo ambayo kwa miongo kadhaa ilishindwa kutekelezwa kutokana na kukosekana kwa fedha na kwamba kama ingetekelezwa ingelifanya taifa kuwa na deni kubwa kwa kuwa lingelazimika kukopa kutoka mataifa tajiri.

Ipo miradi mikubwa kama ya ujenzi wa bwawa la kufua umeme wa maji la Nyerere, ujenzi wa reli ya kisasa, ujenzi wa hospitali na vituo vya afya lukuki katika maeneo mbalimbali, ujenzi wa meli zikiwemo tatu katika bandari ya Kyela, Ziwa Nyasa, utoaji elimu bure na kadhalika.

Ongezeko hilo la makusanyo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na jitihada za dhati za serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli. Serikali katika ngazi zote imekuwa ikitoa ushirikiano wa hali na mali kwa mamlaka,” anasema.

Anafafanua kwamba ushirikiano ambao TRA inapata ni pamoja na kuiongezea uwezo wa kiutendaji kwa kuboresha sheria na mifumo ya usimamizi wa kodi, kudhibiti nidhamu na uadilifu, kuzuia mianya ya ukwepaji kodi, kuhamasisha matumizi ya mashine za kielektroniki za kodi na ulipaji kodi kwa ujumla.

“Sambamba na hilo, miradi mikubwa ya maendeleo inayoendeshwa na serikali kwa fedha zetu za ndani imekuwa ni chachu ya kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari kwa kuwa walipakodi wanaona thamani ya kodi wanayolipa. Hapa unaweza kuona watumishi ni walewale, wafanyabiashara ni walewale lakini kiwango cha makusanyo kimeongezeka jambo linaloonesha kuna mabadiliko makubwa ndani ya taasisi yetu,” anasema.

Pamoja na mikakati ya serikali, jitihada pia za ubunifu zinazofanywa na TRA zimechangia chombo hicho kuimarisha ukusanyaji kodi sambamba na kujiimarisha chenyewe ili kiwatumikie wananchi kwa tija zaidi.

Kamishna mkuu huyo wa TRA anasema katika miaka ya hivi karibuni mamlaka imefanya uwekezaji mkubwa katika kuanzisha na kuboresha mifumo ya usimamizi wa mapato ili kurahisisha ulipaji wa kodi, kuzuia mianya ya upotevu wa mapato na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.

Miongoni mwa uwekezaji katika maboresho ya mifumo anasema ni pamoja na kuanzishwa kwa mfumo wa uwasilishaji ritani za kodi kwa njia ya kielektroniki yaani E- filing System, kuboreshwa kwa mfumo wa usimamizi wa forodha (TANCIS) ili kudhibiti ukwepaji kodi kwa kuingiza bidhaa za biashara kwa kutumia TIN zisizo za biashara (Non-Business TIN) na kuanzishwa kwa mfumo wa mnada kwa njia ya kimtandao, yaani Online Auction.

Mingine ni kuboreshwa kwa mfumo wa usimamizi wa magari, yaani CMVRS, kuanzishwa kwa mfumo wa ukusanyaji kodi kwenye mabenki na kampuni za simu (eRCS), kuanzishwa kwa mfumo wa Stempu za Kielektroniki za Kodi (Electronic Tax Stamps) katika vinywaji na kuunganisha mifumo ya Mamlaka ya Mapato na mifumo mingine ya Serikali Mfano: GePG.

“Pia Mamlaka imekuwa ikitoa mafunzo mbalimbali kwa watumishi wake na kutoa elimu kwa walipakodi na wadau wengine juu ya matumizi sahihi ya mifumo hii ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.”

“Mamlaka inatambua kuwa kazi ya ukusanyaji wa mapato inahitaji kufanywa na watumishi wenye viwango vya juu vya uwajibikaji, uadilifu na weledi. Kwa kutambua hilo, Mamlaka imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kuhakikisha watumishi wake wanafanya kazi kwa kuzingatia uadilifu na uwajibikaji, ikiwa ni pamoja na kuunda idara mahsusi inayosimamia masuala ya maadili na uadilifu.

“Kama ilivyo kwa taasisi nyingine za umma, Mamlaka inatekeleza sera ya kitaifa ya kupambana na rushwa (NACSAP) kwa kuunda kamati za kudhibiti uadilifu katika ngazi ya makao makuu, idara na mikoa ili kusimamia vyema maadili na uadilifu wa watumishi wake. Sambamba na hilo, mamlaka imekuwa ikiendesha mafunzo mbalimbali ndani na nje ya nchi ili kuwajengea weledi watumishi wake.”

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila anarudi kusisitiza kwamba matumizi sahihi ya fedha yanayofanywa na serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli ndiyo chachu ya mafanikio katika ukusanyaji kodi unaofanywa na TRA.

Chalamila  alikuwa akifungua kikao kazi cha tathmini ya utendaji kazi wa idara ya kodi za ndani (TRA) kilichofanyika kwa siku nne mkoani Mbeya kikihudhuriwa na mameneja wa mamlaka hiyo wa mikoa yote nchini, mameneja wawakilishi wa wilaya moja kutoka kila mkoa na maofisa wengine kutoka makao makuu.

Chalamila anasema kumekuwepo na matumizi sahihi ya fedha zinazokusanywa ikiwemo ujenzi wa miradi mikubwa inayoonekana, hatua inayowapa moyo maofisa wa TRA kuendelea kuchapa kazi kwa kuwa matokeo ya kile wanachokusanya wanakiona.

“TRA ni chombo muhimu sana kinachotegemewa kukusanya kodi na kisha fedha hizo zikarejea tena kwa wananchi kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo. Hii ndiyo inayompa jeuri Rais Magufuli kuwa na miradi mikubwa inayotekelezwa kwa fedha za ndani. Lakini kama chombo hiki kitatekeleza jukumu lake halafu upande wa pili kwa maana ya utawala ukatumia vibaya kinachokusanywa kunawavunja moyo ninyi.”

Mkuu huyo wa mkoa anasema ni muhimu ukaendelezwa ushirikiano wa karibu baina ya TRA, viongozi wa Serikali na vyombo vya dola ili kuwezesha Taifa kuendelea kuwa na makusanyo yenye tija na kuwezesha kuwepo kwa miradi yenye kuleta unafuu katika maisha ya wananchi.

Chalamila anasisitiza umuhimu wa watumishi wa Mamlaka kuendelea kuwa na uadilifu akisema kuna wakati mapato yamekuwa yakipotea kutokana tu na baadhi ya maofisa kukosa uadilifu.

Anahimiza TRA kuendelea na mpango wa utoaji elimu kwa mlipa kadi kuwa endelevu ili kuwezesha walipaji wa kodi kutoona kama ni mzigo bali walipe kwa hiari na ukusanyaji kodi ufanywe kwa kufuata misingi iliyowekwa isiyolenga kuwaumiza walipaji.

Anasema Mkoa wa Mbeya utaendelea kutoa ushirikiano kwa TRA kwa kuweka mazingira rafiki ya kufanyia kazi sambamba na kuhakikisha kunakuwepo na mahusiano ya karibu baina ya mamlaka hiyo na wateja wake ambao wengi wao ni wafanyabiashara.

Pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka hii mitano, TRA inasema bado zipo changamoto inazokabiliana nazo.

Dk Mhede anazitaja changamoto hizo ni pamoja na na uwepo wa vitendo vya ukiukwaji wa maadili miongoni mwa watumishi wachache wa Mamlaka Pamoja. Kingine anasema ni baadhi ya wafanyabiashara kutotumia kwa usahihi mashine za kielektroniki za kodi (EFDs) na vitendo vingine vya ukwepaji kodi vikiwahusisha baadhi ya walipakodi kwa kushirikiana na washauri wao wa kodi.

“Sambamba na changamoto hizo, Mamlaka ya Mapato pia inakabiliwa na tatizo la uwepo wa biashara za magendo zinazofanywa na wafanyabiashara wasio waaminifu katika maeneo ya mipaka ya nchi yetu, ikiwemo Mbeya, hali inayoikosesha Serikali mapato stahiki na kuathiri maendeleo ya taifa kwa ujumla.” 

Anasema licha ya biashara hiyo kuikosesha serikali mapato, pia inahatarisha afya za watumiaji na usalama wa taifa na kuathiri uzalishaji wa viwanda vya ndani kwa kuleta uwiano wa biashara usio sawa.

“Kutokana na changamoto hiyo ipo haja ya kulishughulikia suala hili kwa pamoja ili kulitokomeza kabisa katika maeneo yetu ya mkoa wa Mbeya kwenye mipaka ya nchi yetu na nchi za Malawi na Zambia.” 

Kaimu Kamishna wa Idara ya Kodi za ndani wa TRA, Abdul Yusuph Mapembe anasema ili kukabiliana na changamoto ya matumizi yasiyo sahihi ya EFDs kitengo cha upelelezi kimeendelea kufanya kazi yake ya kubaini wakwepa kodi.

Anasema wanaobainika wanachukuliwa hatua za kisheria na kupewa adhabu kali.

Kaimu Kamishna huyo wa Idara ya Kodi za ndani anawataka wafanyabiashara kutambua kuwa miongoni mwa faida za matumizi sahihi ya EFDs ni pamoja na kuiwezesha TRA kufanya makadilio sahihi ya kiasi cha kulipa kodi kwa mfanyabiashara husika.

Kwa upande wake Meneja wa TRA mkoa wa Mbeya, Eunice Liheluka anasema Mbeya ni miongoni mwa maeneo ambayo bado wapo wafanyabiashara wachache wanaofanya udanganyifu kwenye matumizi ya EFDs na kuongeza kuwa jitihada za kuwafuatilia na kuwachukulia hatua zinaendele kila inapobainika.

Watanzania 4,247 wamepata ...

foto
Mwandishi: Joachim Nyambo

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi