loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Safari za ndege Tanzania, Kenya zarejea rasmi

S AFARI za ndege kati ya Tanzania na Kenya zimerejea upya kuanzia jana, baada ya ndege za Kenya kuanza safari zake za kila siku jijini Dar es Salaam.

Aidha, ndege za nchi hiyo zitaanza safari zake kuelekea Kilimanjaro Oktoba 3, mwaka huu mara tatu kwa wiki ; na safari za Zanzibar zinatarajiwa kuanza Septemba 26, mwaka huu mara mbili kwa wiki.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari, akizungumza na HabariLEO jana alisema kwa sasa mambo yako shwari, baada ya Tanzania na Kenya kukubaliana safari za ndege kuanza rasmi kuanzia jana asubuhi.

Alisema kwa upande wa Tanzania, ndege za mashirika ya hapa nchini ikiwamo Precision Air, zilishaanza safari zake juzi. Ndege nyingine zinatarajia kwenda nchini humo hivi karibuni kama ilivyokuwa awali.

Wiki iliyopita, Tanzania iliondoa marufuku dhidi ya safari za ndege za Kenya nchini, ikiwa ni siku moja tu baada ya Kenya kuwaruhusu raia wa Tanzania kuingia Kenya bila kutakiwa kukaa karantini ya lazima ya siku 14 kwa ajili ya virusi vya corona.

Taarifa iliyotolewa Jumatano iliyopita na TCAA, ilieleza kuwa safari zote za ndege kutoka Kenya, sasa zinaruhusiwa katika anga ya Tanzania na kuwa ilikuwa inasubiri maombi ya kuanza safari pamoja na ratiba za ndege za nchi hiyo.

umanne iliyopita Kenya iliiweka Tanzania katika rodha ya mataifa ambayo raia wake wakiingia nchini humo, sio lazima wawekwe karantini ya siku 14 kwa hofu ya maambukizi ya virusi vya corona.

Mataifa mengine yaliyowekwa katika orodha hiyo ni Ghana, Nigeria na Sierra Leone. Kufuatia hatua hiyo, Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) limeeleza kuwa kurejeshwa kwa safari za anga kwa nchi hizo mbili, kutakuza ushirikiano wa kibiashara kwani zinategemeana katika sekta hiyo.

Baraza hilo lilisema hatua hiyo pia itasaidia kukuza utalii na biashara baina ya Tanzania na Kenya. Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Kenya, mwaka jana thamani ya biashara ya nje kutoka Kenya kwenda Tanzania, ilikuwa kwa wastani wa dola za Marekani milioni 336, huku ikiingiza bidhaa za dola za Marekani milioni 275.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa EABC, Dk Peter Mathuki, alisema wamekuwa wakihamasisha ushirikiano na kufungua anga kwa zaidi ya miezi miwili tangu nchi wanachama wa EAC zilipoanza kufungua mipaka yao.

Alisema wanaamini hatua ya kufungua anga baina ya Tanzania na Kenya, itaongeza wasafiri na kurahisisha mwingiliano wa watu, usafirishaji bidhaa na fursa za upatikanaji wa masoko na utalii kikanda.

Hata hivyo, Dk Mathuki alizitaka nchi wanachama wa EAC kuangalia upya ada za kutua ndege, kupunguza ushuru kwa mafuta ya ndege, kutua, maegesho na ada nyingine zinazohusiana na covid-19, ili kupunguza gharama kubwa za usafari wa anga.

Wakati Uganda ikitarajia kuanza safari za kimataifa Oktoba Mosi mwaka huu, Rwanda ilifungua anga lake kimataifa Agosti Mosi .

Agosti mwaka huu Tanzania ilifuta kibali cha ndege za Shirika la Ndege la Kenya (Kenya Airways) kutua nchini, baada ya serikali ya Kenya kutoiweka Tanzania katika orodha ya nchi ambazo raia wake wanaruhusiwa kuingia nchini humo.

Watanzania 4,247 wamepata ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi