loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mwanafunzi aliyekufa akiogelea azikwa Dar

MWANAFUNZI mmoja kati ya wawili waliofariki dunia Septemba 19, mwaka huu wakiogelea katika bwawa la kuogelea jijini Dar es Salaam, amezikwa jana huku wakiacha simanzi kwa wazazi, ndugu na jumuiya ya shule walikokuwa wakisoma.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka familia ya mmoja wa watoto hao, Gabriel Johannes (10) mkazi wa Goba na mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi ya St Claret ya Kimara Michungwani, alizikwa jana makaburi ya King’ongo njiapanda ya Goba jijini humo.

Taarifa hiyo ilisema mtoto huyo alikuwa akilelewa na familia ya Charles Igonda inayoishi Goba. Ibada ya kuaga mwili, ilifanywa jana katika Kanisa la Moravian Ushirika wa Adonai.

Mwanafunzi wa pili aliyefariki ni wa kike ametambuliwa kuwa ni Frahina Swalo (12) mkazi wa Kimara Bucha, aliyekuwa akisoma shuleni hapo darasa la sita.

Watoto hao kwa pamoja walidanganya nyumbani kwao wanakwenda kwenye mahafali shuleni, ilhali hawakuchaguliwa kwenye programu za mahafali.

Taarifa ya uongozi wa shule hiyo ilisema taarifa za mazishi kwa mtoto wa pili zitatolewa, pindi familia itakapoamua siku ya kuzika.

Awali uongozi wa shule hiyo, ulitoa taarifa kwa jumuiya ya wazazi kuwa vifo vyao vimetokana na ajali ya maji, ambapo walikuwa wanaogelea kwenye bwawa hilo ambalo ni la biashara, linalomilikiwa na mtu binafsi na wao walikwenda kwenye kina kirefu na kuzidiwa maji.

“Wanafunzi hawa jana (juzi), waliaga nyumbani wanakwenda shuleni kwenye mahafali lakini hawakufika, nia yao walipanga kwenda kuogelea na baadhi ya wanafunzi wenzao kwani hawakuchaguliwa kwenye programu za mahafali kama barua zilivyoelekeza na ndipo wakafikwa na umauti,”ilisema taarifa hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Edward Bukombe alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema wanamshikilia mmiliki wa bwawa hilo, Baraka Mtewele (37) na msimamizi wa bwawa hilo.

Kamanda Bukombe alisema tukio hilo lilitokea Septemba 19, mwaka huu saa 5 asubuhi katika bwawa la kuogelea liitwalo Jordan lililopo Kimara Michungwani.

“Tunawashikiliwa watu wawili hadi sasa, mmiliki huyo Mtewele na msimamizi wa bwawa kwa ajili ya uchunguzi, kwa sababu kuna sheria na kanuni za kufuata wakati wa kutoa huduma hiyo, lazima awepo mwangalizi au msimamizi ambaye kama angekuwepo angeona watoto hao wanazidiwa maji na kuwaokoa, au angewaelekeza waogelee kwenye kina kifupi kwa umri wao,”alisema Bukombe.

Alisema wanaendelea na uchunguzi wa kina kubaini iwapo kuna uzembe ulitokea na kujua ukweli wa vifo hivyo.

Katika hatua nyingine, Kamanda Bukombe aliwataka wazazi kuwa na taarifa sahihi za watoto wao wako wapi na kuwafuatilia ili kudhibiti madhara kama hayo yasitokee.

Aidha, aliwataka wamiliki wa maeneo hayo kuzingatia sheria na kuhakikisha wasimamizi wanakuwepo wakati wote kama inavyoelekezwa.

Watanzania 4,247 wamepata ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi